Thursday, October 14, 2010

HABARI ZA UHALIFU WA KIMAFIA TANZANIA HIZI HAPA

Mengi awalipua polisi



• ABAINI NJAMA ZA KUMBAMBIKIA MWANAE DAWA ZA KULEVYA DAR

TANZANIA DAIMA LA Jumatano, 13 Oktoba 2010

na Mwandishi wetu



MWENYEKITI Mtendaji wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi, amedai kubaini njama chafu za kutaka kumbambikia mwanae dawa za kulevya.

Mengi alifichua njama hiyo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Akifafanua kisa hicho cha kusikitisha, Mengi alisema mpango huo umefadhiliwa na mmoja wa watu aliopata kuwataja siku za nyuma kwamba ni mafisadi papa, kutokana na kujihusisha na matukio ya ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).



Waliotajwa na Mengi katika sakata hilo lililotikisa nchi ni pamoja na mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia, Yusuf Manji, Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, Jeetu Patel, ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi ya EPA mahakamani na Tonil Sumaiya.



Huku akizungumza kwa kutulia na kujiamini, Mengi alisema mfanyabiashara huyo ambaye hakumtaja jina, amefadhili mkakati huo kwa kuwahusisha baadhi ya maofisa wa polisi wa ngazi ya juu nchini na Polisi wa Kimataifa (Interpool) ambao kila mmoja angelipwa dola za Marekani 40,000, sawa na sh milioni 47.



Kwa mujibu wa Mengi, mpango huo ambao umegharimiwa kwa sh bilioni tatu, pia umewahusisha maofisa wawili ambao hakuwataja majina kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere na maofisa kutoka kampuni moja ya simu za mkononi nchini.

Akisimulia mpango mzima wa mkakati huo, Mengi alidai kuwa siku ya tukio, mwanae akiongozana na watu wengine wanne, walitarajiwa kusafiri hadi nchini India kwa shughuli za kikazi.

Alisema walipofika katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere, alipambana na mazingira ya ajabu na hatimaye kujinasua kwenye mtego uliosukwa ili wamnase na dawa za kulevya.



“Kwa mapenzi ya Mungu, kijana wangu alibaini mbinu hiyo chafu na kwa mapenzi ya Mungu aliahirisha safari. Tulipofanya uchunguzi, tukabaini mpango huo na kuwajua wahusika ambao nitawataja pamoja na kiasi cha fedha walichoahidiwa na walichokwisha kuchukua kama malipo ya awali kwa kazi hiyo haramu,” alisema Mengi.



Mfanyabiashara huyo maarufu nchini, aliwataja aliodai kuhusika katika mpango huo kuwa ni pamoja na Kamishna wa Polisi Msaidizi wa kitengo cha kukabiliana na dawa za kulevya, Godfrey Nzowa, aliyeahidiwa dola za Marekani 40,000, sawa na sh milioni 47 na kulipwa dola za Marekani 20,000, sawa na sh milioni 23.5.



Mwingine ni ofisa wa polisi, Charles Mkumbo na polisi wa Interpool, aliyemtaja kwa jina moja la Henry. Wote waliahidiwa kiasi kama hicho cha Nzowa na kupata malipo ya awali yanayofanana.



“Mkumbo alionekana kwenye ofisi za mfanyabiashara huyo akiwa anaendesha gari lake aina ya Rav4, lenye rangi ya silver, siku hiyo ya Septemba 26, majira ya saa nne asubuhi na alikwenda kuchukua malipo yake ya awali,” alisema Mengi.

Watuhumiwa wengine katika mpango huo ni maofisa wawili wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere na ofisa kutoka kampuni moja ya simu za mkononi ambao hata hivyo hakuwataja kwa majina. Hao wanadaiwa kuahidiwa sh milioni 15 na wote walilipwa malipo ya awali ya sh milioni saba kila mmoja.



Mengi alisisitiza kuwa anajua anachokisema na amejiandaa kutoa ushahidi wa kutosha, hivyo aliwataka wahusika waende mahakamani ili akatoe ushahidi zaidi juu ya mpango huo aliouita kuwa ni wa kigaidi.



“Huu ni unyama, maisha ya mwanangu na heshima yangu ingekwisha, kwani kila mmoja angesema Mengi ni muuzaji wa dawa za kulevya. Namfamu mwanangu, hana tabia hiyo na hawezi kujihusisha na biashara hiyo haramu na kama mtego huo usingegunduliwa, huo ungekuwa mwisho wa maisha ya mwanangu,” alisisitiza Mengi.



Mengi alisema Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri na analiheshimu, lakini alidai kuna watu wachache wanaotaka kuharibu heshima ya jeshi hilo.

“Ndani ya Jeshi letu la Polisi, kuna viongozi wazuri, waadilifu, ukianzia na IGP Mwema, wasaidizi wake, kina Kamanda Venance Tossi, Suleiman Kova, Elias Kalinga, Chilogile na wengine, ni wachapa kazi wazuri, waadilifu, lakini wapo wachache kwa sababu ya tamaa ya fedha, wanataka kuliharibu jeshi letu,” alisema Mengi.



Akijibu tuhuma hizo, Nzowa, kwanza alishangaa kusikia taarifa hizo na kuongeza kuwa katika kipindi alichotaja Mengi alikuwa nje ya nchi kikazi.

“Kwanza mimi katika kipindi anachotaja Mengi sikuwepo nchini. Lakini pia sijui kama Mengi au huyo mwanae wananijua. Binafsi huyo mwanae wala simjui, sasa sijui nimehusikaje hapa,” alisema Nzowa.

Kamanda huyo wa kikosi cha kudhibiti dawa za kulevya nchini alisema kauli ya Mengi ina lengo la kumchafulia, kwani kiasi anachokitaja ili kumhujumu mwanae ni kidogo sana ikilinganishwa na ahadi alizowahi kupewa na wahalifu, lakini alizikataa na kusimamia misingi ya sheria.



Kwa upande wake, Kamanda Mkumbo, naye aliruka ‘kimanga’ kwamba hajawahi wala hawezi kuthubutu kumbambikia dawa za kulevya mtu, kwa sababu ya kulipwa pesa.



“Mimi kwanza huyo mtoto wa Mengi simjui na hata sasa sijui tuhuma hizi zinatokea wapi. Hata mbele ya Mwenyezi Mungu niko tayari kukana kuhusika na mpango huo,” alisema.



Kamanda huyo alisema anashangazwa zaidi kuhusishwa na Nzowa kwenye mpango huo, kwani vitengo vyao havihusiani kikazi.



Chanzo: Gazeti la TanzaniaDaima

No comments:

Post a Comment