Friday, October 22, 2010

TAMKO LA FEM-ACT KUHUSU TISHIO LA SERIKALI DHIDI YA TAMWA NA VYOMBO VYA HABARI TANZANIA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI - Posted here on 23/10/2010

TAMKO LA FEMACT KUHUSU TISHIO LA SERIKALI DHIDI YA TAMWA NA VYOMBO VYA HABARI 21/10/2010

Sisi Mashirika yapatayo 50 yanayotetea Usawa wa Kijinsia, Haki za Binadamu, Maendeleo na Ukombozi wa Mwanamke Kimapinduzi (FemAct) tunalaani kauli ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo, kuwatishia wanaharakati kuwa wasizungumzie masuala ya uchaguzi. Katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010, tumebaini dhamira na hatua za makusudi za Serikali kukiuka haki za binadamu kwa kutishia na hatimaye kunyamazisha sauti za vyombo vya habari na raia; mtu mmoja mmoja, wanafunzi wa elimu ya juu, asasi za kiraia, na makundi mengine ya kijamii yanayotoa elimu ya uraia kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inapata viongozi bora na kuendelea kuongozwa kidemokrasia, na kujihakikishia mabadiliko chanya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 31, 2010.



Kwa kuzingatia haki na wajibu wetu kama kiraia chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977, kunako Oktoba 6, 2010 tulitoa tamko kwa vyombo vya habari tukilaani kitendo cha vyombo vya usalama vikiongozwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuingilia mchakato wa uchaguzi jambo ambalo lingeweza kusababisha vitisho dhidi ya wananchi, vurugu na hatimaye kuchafua hali ya amani na usalama ambayo ni tunu ya Tanzania.



Vyombo vya habari, kwa kuzingatia maslahi ya umma, vilichapisha na/au kutagangaza Tamko la FemAct. Tumeshangazwa kusikia Serikali kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamadauni na Michezo Ndugu Seth Kamuhanda akikishambulia Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), ni mwanachama wa mashirika ya FemAct, kwamba kwa kutoa tamko hilo TAMWA imeacha malengo yake na inajihusisha na siasa. Tunaona kuwa kitendo cha Serikali kutishia na kuishambulia TAMWA ni sawa na kutishia na kushambulia FemAct na watanzania wote kwa ujumla. Huu ni uonevu usiostahili kuvumiliwa. Ni jambo la kushangaza zaidi kuona Serikali inajiingiza katika masuala ya kampeni za uchaguzi wakati washiriki rasmi wa kampeni za uchaguzi, kwa mujibu wa sheria, ni vyama vya siasa.



Kadhalika tumesikitishwa na kitendo cha Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo kutishia kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mwanahalisi, ambayo yamekuwa yakitoa taarifa za matukio ya uchaguzi kama vyombo vingine vya habari, kwa kwa madai kwamba yanaandika habari za uchochezi dhidi ya serikali iliyoko madarakani. Aidha tunalaani hatua ya Serikali kukifungia kituo cha Redio SAUT FM cha Mwanza.



Tunapenda serikali ifahamu kuwa FemAct tunaendelea kufuatilia na watanzania wako macho dhidi ya hujuma yoyote itakayotokea kufifisha sauti za wananchi zinazochagiza na kuhimiza kupanua uelewa, uhuru na ushiriki wa wananchi katika kampeni za Uchaguzi Mkuu na hatimaye kupata uangavu wa kutosha kuchagua viongozi wanaojali na kusimamia maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla. Tunatoa wito kwa wananchi kuunganisha nguvu zao na kudai uwajibikaji kutoka serikalini na kwa viongozi tuliowaweka madarakani.



Ibara ya 18 na Ibara ya 20 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatamka na kusimamia uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa kujumuika. Haki hizi zimetolewa ufafanuzi katika kesi mbali mbali ikiwamo kesi maarufu ya BAWATA. Katika kesi hii, uhuru wa kujumika umefafanuliwa na tabia ya viongozi kufungia mashirika ya kiraia bila kufata taratibu vimekemewa hata na mahakama kuu ambayo nayo ni chombo cha Katiba kilichopewa jukumu la kusimamia haki kwa wananchi.



Madai yetu:-

1. Serikali iache kutishia mashirika ya kijamii na mtu mmoja mmoja katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa madai kuwa wanaingilia masuala ya kisiasa. Wananchi wana haki ya kutoa maoni na mawazo mbadala kwa maslahi ya Taifa.

2. Serikali irejee maamuzi ya Kesi ya “BAWATA” juu ya haki ya wananchi kujumuika na izingatie sheria za nchi kabla ya kufanya maamuzi ya kutoa karipio au vitisho kwa taasisi za kiraia na vyombo vya Habari. Utawala bora unahimiza watanzania wote wakiwemo viongozi wetu tunaowapata kwa demokrasia kuzingatia sheria za nchi.

3. Tunahimiza wananchi kuwa macho na viongozi wanaotaka kutumia nguvu nyingi kuziba midomo wananchi na kuendelea kuwa macho kulinda na kutetea maslahi ya taifa wakati wote.

4. Sisi kama mashirika yasiyo ya kiserikali tutaendelea kufanya kazi ya kutoa elimu ya uraia kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi bila kuogopa wala kupendelea mtu yeyote wala chama chochote cha siasa.



MUNGU IBARIKI TANZANIA

.












Ananilea Nkya
Executive Director
Tanzania Media Women's Association (TAMWA)
P. O. Box 8981, Sinza-Mori
Dar es Salaam, TANZANIA
Tel: +255-22 2772681 Fax +255 22 2772681 E-mail:ananilea_nkya@yahoo.com
Cellphone:+255-754-464-368

No comments:

Post a Comment