Sunday, October 17, 2010

RASILIMALI ADIMU ZA TANZANIA NA DUNIANI

Imeandikwa na Beda Msimbe; Tarehe: 14th October 2010 Habari Leo

MSITU WA MAZUMBAI WA LUSHOTO, TANZANIA

Eneo la kupumzikia wageni wa SUA ndani ya msitu wa Mazumbai.

NDANI ya milima ya Usambara kuna misitu miwili mikubwa inayotumika kwa utafiti.

Misitu hiyo ni ya Amani na Mazumbai. Msitu wa Amani upo Muheza na ule wa Mazumbai upo Lushoto. Nilifika msitu wa Mazumbai wenye
ua linalopatikana kiasili Tanzania pekee, ‘African Violet’.

Nilikuwa sijawahi kuona ua la African Violet, lakini nilipata kulisoma sana katika mtandao na nilipofika Mazumbai kitu cha kwanza kuuliza na kutaka kuoneshwa ni ua hilo, Meneja wa Hifadhi ya Msitu wa Mazumbai, Said Kiparu alikuwa zaidi ya tayari kunionesha, yalikuwa yamepandwa nje ya nyumba ya kupumzikia iliyo hapo.

Nyumba hiyo hutumika na watu wanaozuru msitu huo pamoja na watafiti na siku ambayo nilifika kulikuwa na wazungu kadhaa waliofika
kutalii na walitarajiwa kuwapo hapo kwa siku nne au zaidi walikuwa msituni wakivinjari.

Kuwapo kwa ua hilo si tu fahari ya Tanzania, lakini ua hilo lenyeugumu mkubwa wa kuota na kumea lililopewa jina na Mjerumani mmoja aliyepeleka taarifa kwao kuhusu kuwapo kwa ua hilo la urujuani wakati akivinjari milima ya Usambara.

African Violet au tuseme Ua la Usambara ambalo wenyeji wa Usambaani huliita ‘Dughulishi’, lilijulikana kwa Wazungu mwaka 1892 kupitia Baron Walter von St. Paul na tangu wakati huo mpaka leo zaidi ya aina 20 za maua haya zimebainika.

Kusema kweli pamoja na kutawanyika kwa African violet duniani, Wazungu wanatambua kwamba makao yake makuu yapo Usambara wakati wakielezea historia ya maua hayo ambayo watu wengi wa Ulaya hupenda kuyaweka majumbani kwao kutokana na uzuri wake.

Kwa historia, Baron huyu ambaye alikuwa na hisia za masuala ya mimea ya bustani (unaweza kumuita botania) ndiye aliyewezesha mimea hii kufika Ulaya kwa kumtumia baba yake Baron Ulrich von Saint Paul-Illare, ambaye wakati huo alikuwa ni Rais wa chama cha miti nchini Ujerumani (Dendrological Society of Germany).

Juhudi hizo zilifanya kuanzia mwaka 1893 ua hilo kupatikana nje ya usambara na watu kuanza kulizalisha kwa wingi kwa kutumia mbegu hizo zilizotoka Tanzania.

Sehemu kubwa ya maua ya African Violet katika bara la Ulaya na Marekani si orijino ni haibridi. Kimsingi ua hilo lilitawanyika dunia kupitia Ujerumani na pamoja na kupendwa sana Marekani yalifika huko mwaka 1926 yakitokea Ujerumani.

Sasa hivi nchini Marekani kuna jumuia nyingi zinazojihusisha na African Violet. Botani huyu Baron Walter von Saint Paul, alikuwa ni Gavana wa Kijerumani jimbo la Kaskazini Mashariki la Tanganyika na aliyaona maua hayo yakijiotea katika vipenyo vya majabali.

Ndani ya Msitu wa Mazumbai ambao kimsingi unamilikiwa na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na kutumiwa nadra na watalii lakini sana na watafiti kuna zaidi ya maua, ipo miti aina tofauti zaidi ya 100 ambayo inamea vyema ikiangaliwa isifanyiwe
uharibifu.

Watu wa SUA walikabidhiwa msitu huo na mzungu anayeitwa John Tanner ambaye alikuwa na mashamba yake ya chai katika eneo hilo na aliitunza misitu ya asili aliyopukuta kwa sababu za shughuli yake aliyokuwa akiifanya.

Mzungu huyo aliyezaliwa Tanga mwaka 1918 aliishi Mazumbai kuanzia mwaka 1946 hadi mwaka 1982, kwa sasa yupo nchini kwao Uswisi na habari zinasema yungali hai.

Kuwapo mashamba ya chai kunaonesha kwa nini kulikuwa na misitu kwani utengenezaji wa chai hutumia miti mingi kwa hiyo kulikuwa na haja ya kuwa na miti ya kutosha (misitu) kwa ajili ya kazi hiyo.

Ndani ya msitu huo pia mzungu huyo alikuwa ametengeneza mfumo wa kufua umeme ambao ndio unaotumiwa hadi sasa na nyumba ya SUA kupata nishati. Umeme huo wa maji unaofuliwa katika nyumba kuukuu ni moja ya vivutio ambavyo vinaweza kutoa taswira ya neema katika harufu nzuri ya misitu na maua yake.

Ndani ya msitu huo mnene yapo magogo makubwa ambayo yamechomoza kwa namna inayopendeza zaidi, ingawa huwezi kuona kila kitu kilichopo katika msitu huo pamoja na nyoka wa aina mbalimbali, ndege, kuna mandhari inayokonga moyo hasa kwa wale wanaopenda asili na vitu vinavyofuatana navyo.

Kuna miti ambayo mizizi yake iliyojitokeza nje ina urefu wa zaidi ya futi tano ikitengeneza mandhari ya kustaajabisha zaidi. Ni kama jengo lililofumwa. "Hii ni hifadhi, inasaidia vitu vingi sana na watu hawaruhusiwi kuingia ndani ya msitu na kuvuna," anasema Meneja Kiparu.

Akaongeza kwamba, pamoja na kuwatembeza watalii ni kazi yao kutoa nafasi ya watu kujifunza masuala ya misitu na namna hifadhi
inavyoweza kuokoa misitu na katika hilo watafiti wa ndani na nje hufika kujifunza kwenye msitu huu ambao kimsingi ulikuwa binafsi.

Katikati ya msitu huu wa hifadhi wa hekta 300 kuna mbega na ndege mbalimbali ambao hupendezesha sauti katika msitu unaozizima kwa utulivu.

No comments:

Post a Comment