Saturday, June 5, 2010

WAZIRI MWAKYUSA KATOA KAULI ZA KEBEHI NA BEZO KWA WANAWAKE WA TANZANIA

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Prof. David Mwakyusa alipotoka sana tena sana kwa kauli yake ya kwamba "Suala la kujifungua kwa wanawake kuwa starehe badala ya majonzi" yanayotokana na vifo vya kinamama hapa nchini Tanzania; aliyoitoa tarehe 5 Aprili, 2010 jijini Dar es Salaam, TANZANIA, na kunukuliwa na Gazeti la NIPASHE.

Kwa kweli haiwezi kupita bila kutolewa kauli ya marekebisho na sisi wanawake wenyewe tuliopitia na tunaoendelea kupitia MTULINGA wa kujifungua.

Profesa kwa kuwa ni mwanaume hawezi kupata chembe ya hisia za machungu anayopitia mama anayejifungua. Haijalishi endapo mzazi huyo ataishi au atapoteza maisha. Hivyo Profesa tunamtaka arekebishe kauli yake kwa sababu inaleta hisia za kubeza na kukejeli masaibu ya uchungu yanayotukuta wanawake wakati wa kujifungua.

Tunamhakikishia Profesa Mwakyusa kwamba hakuna starehe yeyote katika zoezi zima la kujifungua na hivyo ni kauli ambayo haikustahili kutolewa na mzungumzaji Kiswahili kama yeye aliyelelewa chini ya uongozi wa Baba wa Taifa. Ikumbukwe kwamba Profesa Mwakyusa alikuwa Daktari binafsi wa Mwalimu Nyerere kwa miaka mingi na hivyo tungetaraji kwamba yeye angekuwa mstari wa mbele katika kutumia misamiati mwafaka katika hotuba zake.

Suala la kujifungua sio suala la kulitafutia lugha ya kibiashara kama hii, kwa sababu linaleta hisia kali sana kwa wanawake waliojifungua na wanaoendelea kujifungua popote pale walipo.

No comments:

Post a Comment