Saturday, June 19, 2010

MAJAJI WAMEPOTOKA RUFAA YA SHAURI LA MGOMBEA BINAFSI

Dk Mwakyembe: Majaji wamepotoka
Friday, 18 June 2010 23:01
Imeandaliwa na Fidelis Butahe, Hussein Issa, Geofrey Nyang'oro na Freddy Azzah
Chanzo : Gazeti la Mwananchi 18/6/2010.

NI KWELI WATANZANIA WANASHERIA WOTE TUNAJIULIZA MAHAKAMA YA RUFAA NI YA KAZI GANI KAMA SIO KUAMUA HAKI ZA WATU KAMA ILIVYOAINISHWA KATIKA IBARA YA 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977???


WANASIASA na wasomi nchini wamesema kuwa majaji saba waliotoa hukumu ya mgombea binafsi wamepotoka na kujichanganya kwa kuliachia Bunge jukumu hilo.

Alhamisi, tarehe 17/6/2010 Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilitupilia mbali uwezekano wa kuwepo kwa mgombea binafsi licha ya Mahakama Kuu kuamua katika kesi iliyofunguliwa na Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila kuwa sheria inayozuia mgombea binafsi inakiuka Katiba ya nchi.

Kutokana na hali hiyo Mahakama ya Rufaa imerudisha hoja hiyo bungeni ambapo katika hukumu yake ilieleza kuwa suala hilo lazima liwekwe na Bunge ambalo lina uwezo wa kisheria wa kufanya marekebisho ya kikatiba na si mahakama ambazo hazina uwezo huo kisheria.

Mbunge wa Kyela, Dk Harison Mwakyembe ndiye amepinga vikali suala hilo na kusema kuwa haikustahili kupelekwa bungeni kwa ajili ya kujadiliwa.

Alisema yeye kama mwanasheria anafahamu kuwa suala hilo ni la haki, kilichotakiwa kutolewa na mahakama ni mwongozo kwamba nini Bunge linatakiwa kufanya, kwa sababu mahakama ndio inayosimamia sheria badala ya Bunge kuzitunga na kuzipitisha.

"Nikisema suala hili la mgombea binafsi sio haki nikiwa kama mwanasheria, wenzangu na hata wanafunzi wangu watanishangaa sana, ukweli ni kwamba ni haki ya kuwa na mgombea binafsi, ila haina manufaa kwani hawana nguvu, mfano Marekani wanao wagombea binafsi, lakini hawafahamiki," alisema.


Mwakyembe ambaye alisema hayo katika mahojiano ya moja kwa moja na kituo chaTBC jana asubuhi, aliongeza kuwa mahakama ni zao la katiba, hivyo kilichotakiwa ni kusimamia katiba kama ilivyotungwa na Bunge na sio kurudisha tena majadiliano bungeni badala ya kumaliza kesi hiyo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye kitaaluma ni mwanasheria, Dk Sengondo Mvungi alisema maamuzi ya mahakama hiyo yameiidhihirishia dunia kuwa Tanzania haiheshimu haki za msingi za binadamu na utawala bora.

"Uamuzi wa jana (juzi), ulimaanisha kuwa Watanzania wote tumepoteza, tumeipoteza miaka zaidi ya 48 ya kupigania uhuru, utawala bora na kuheshimu haki za binadamu," alisema Dk Mvungi ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya katiba.

Dk Mvungi aliendelea kufafanua kuwa, makosa ya Bunge na serikali ya kutomtambua mgombea binafsi, kisheria yalipaswa kurekebishwa na mahakama.

Mvungi alifafanua kuwa, haki za msingi za binaadamu, zilikuwepo tangu siku ya kwanza aliyoumbwa na kuongeza kuwa mahakama inapaswa kulizilinda haki hizo za kiasili.


"Haki za binadamu hazijaundwa na dola wala katiba, mahakama wamekopeshwa tuu kulinda haki hizi, katika utawala bora mahakama lazima iwe na mamlaka ya asili ya kulinda haki za binadamu, kitu ambacho hawa waheshimiwa walikisahau," alisema na kuongeza;

"Kwa hukumu iliyotolewa na mahakama hiyo imedhihirisha kuwa Tanzania katika suala la utawala bora na kuheshimu haki za msingi za binadamu iko nyuma sana, katika hili mahakama imejipiga risasi yenyewe wala hakuna aliyeishinikiza na imejipotezea heshima yake mbele ya wananchi,".

Naibu Katibu Mkuu wa CUF upande wa Zanzibar, Juma Haji Duni alisema kwa hatua hiyo ya Mahakama ya Rufaa imeonyesha kuwa kwa sasa wananchi hawana mahali pa kupata haki zao za msingi.

"Kama Mahakama na Bunge vimeshindwa kuwasaidia wananchi sasa sijui watakimbilia wapi, unapoona nchi nyingine zina machafuko usidhani kuwa yameanza siku moja, machafuko hayo yanatokana na wananchi kuelemewa na mambo kama haya,"
alisema Duni.

Duni alidai kuwa wananchi wameshavulimilia kwa muda mrefu kukaa bila kupata haki zao za msingi na kwamba hivi sasa wamechoka na hatma ya nchi iko mikononi mwao.

Alidai uamuzi wa mahakama hiyo ulikuwa na shinikizo la serikali na CCM.

Duni alisisitiza kuwa, duniani nzima Mahakama na Bunge vinatakiwa kulinda haki za binadamu na kuwa kwa Tanzania vyombo hivyo vimeshindwa kutimiza majukumu yake hayo ya msingi.

Kwa upande wake mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chadema , Halima Mdee alisema kuwa kesi ilitakiwa iishe kwa mujibu wa sheria na si kuipelekea Bunge kwa kuihusisha na siasa.

Alisema anachokifahamu yeye kama mwanasheria mahakama ni mlinzi wa matakwa ya watu.

"Hili sio suala la kisiasa zaidi kwani kila mtu analifahamu kilichokuwa kinatakiwa hapa ni kutoa maelezo kwa Bunge tu lifanye nini ,"alisema Mdee

Alisisitiza kuwa mahakama inafahamika kuwa ni zao la katiba na sheria, hivyo ilichokuwa inatakiwa ni kutoa maelekezo kwa kufuata vifungu vya sheria.

Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema hatua hiyo ni sawa na kesi kupelekwa mahakamani halafu mahakama ikatoa amri kuwa kesi hiyo ikasikilizwe kifamilia na kufafanua kuwa hatua hiyo haiwezi kutoa haki kwa anayeshitaki na aliyeshitakiwa kwa kuwa familia itapendelea upande mmoja.

Wakati huohuo na wanaharakati wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), wameibuka na kuipinga vikali hukumu hiyo.

Wanaharakati hao sasa wanajianda kulifikisha suala hilo kwenye mahakama (African court of Justice and Human right) yenye makao makuu mjini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Mkurugenzi wa kituo hicho, Francis Kiwanga alisema maamuzi hayo yanayonyesha mahakama kushindwa kufanya kazi yake ya kutafsiri sheria kama ilivyopewa mamlaka hayo na katiba.

“Ikumbukwe kuwa msingi mkuu wa utawala bora ni kutofautisha majukumu na mamlaka ya mihimili ya nchi ambayo ni Mahakama, Serikali na Bunge, kama mahakama inakiri kutokuwa na mamlaka ya kutoa haki ni chombo gani kingine kinaweza kuwa na mamlaka hiyo?”alihoji Kiwanga na kuongeza;

“Kituo kinaanda jopo la wataalamu wa sheria ili kupeleka suala hili kwenye vyombo vya kimataifa vya utoaji haki,”alisema Kiwanga.
Kiwanga alisema mahakama ndio chombo peke kikatiba kinachotakiwa kutafiri sheria na kutoa maamuzi bila upendeleo wowote.

No comments:

Post a Comment