Monday, May 4, 2015

PICHA ADIMU ZA TANU YA TANGANYIKA 1954 - 1961

PICHA ADIMU ZA TANU, JULIUS NYERERE NA WAZALENDO WALIOSAHAULIKA KATIKA HISTORIA YA KUDAI UHURU WA TANGANYIKA 1954 - 1961

Written By Mohamed Said on Saturday, May 2, 2015 | 11:25 AM


Abdulrahman Ali Msham sasa ni mtu mzima na ana umri wa miaka 65. Wakati TANU inaasisiwa Dar es Salaam mwaka 1954 yeye alikuwa mtoto wa miaka minne. Majuma machache yaliyopita alikisikia kipindi kilichorushwa na Radio Kheri 104.10 FM kuhusu safari ya Mwalimu Nyerere UNO mwaka 1955. Kwa kauli yake mwenyewe anasema kipindi kile kilimrudisha  nyuma sana akamkumbuka marehemu baba yake Ali Msham ambae alikuwa moja wa wazalendo waliokuwa mstari wa mbele katika kupambana na ukoloni. Abdulrahman Ali Msham akawa na hamu kubwa ya kukutana na aliyekuwa akieleza safari ile ya kihistoria. Alikuwa na hamu kwa kuwa na yeye alikuwa na machache angependa kueleza nini baba yake Mzee Ali Msham alifanya katika TANU katika ile miaka ya 1950. Abdulrahman alianza kwa kueleza kuwa baba yake alikuja Dar es Salaam kutoka Kilwa katika miaka ya 1950 akiwa fundi seremala na likuwa akifanya shughuli zake za kutengezeza samani Mtaa wa Kariakoo na Congo. TANU ilipoasisiwa mwaka wa 1954 baba yake alijiunga na kuwa mwanachama kwa kukata kadi ya TANU. Makazi yake yalikuwa Mtaa wa Jaribu Magomeni Mapipa ambako alikuwa akiishi kwenye nyumba yake mwenyewe. Katika hamasa zile za kupambana na ukoloni baba yake alitoa chumba kimoja katika nyumba yake akafungua tawi la TANU na yeye mwenyewe akiwa mwenyekiti. Katika harakati zile za kupambana na ukoloni alisikitiswa na hali ya ofisi ya Mwalimu Nyerere pale New Street kwa kuwa hakuwa na samani za maana katika ile ofisi yake. Baba yake alirejea kwenye kiwanda chake pale Mtaa wa Kariakoo na Congo akatengeneza meza ya ofisi ya hadhi ya rais wa TANU pamoja na viti kadhaa. Mzee Ali Msham alimwalika Mwalimu Nyerere kwenye tawi la TANU la Magomeni Mapipa ili makabidhi samani mpya kwa ajili ya ofisi yake. Mwalimu Nyerere alifika pale kwenye tawi la TANU na katika sherehe fupi Mwalimu Nyerere akakabidhiwa samani ile. 
Kumaliza mazungumzo yetu Abdulrahman Msham alikabidhi picha za baba yake za wakati ule wa kupigania uhuru. Picha hizo nami naziweka hapa kwa ajili ya kuhifadhi na kuthamini mchango wa wazee wetu mashujaa waliopigania uhuru wa Tanganyika lakini kwa bahati mbaya michango yao haijathaminiwa. 
Picha hiyo hapo chini inamwonyesha Mwalimu Nyerere akipokea samani hiyo iliyotengezewa na Mzee Ali Msham. Aliyesimama wa kwanza kulia ni Mzee Ali Msham mwenyekiti wa tawi la TANU Magomeni Mapipa wakati TANU inawaunganisha wananchi kupigania uhuru wa Tanganyika.




Ali Msham aliyekaa katikati katika moja ya mikutano ya ndani ya TANU aliyokuwa akifanya uani nyumbani kwake Mtaa wa Jaribu, Magomeni Mapipa
Kushoto Wakwanza Ali Msham


Ali Msham (kushoto aliyesimama) akiwahutubia wanachama wa TANU uani nyumbani kwake katika mkutano wa ndani

Tawi hili la TANU Magomeni Mapipa lilikuwa na nguvu na viongozi mashuhuri wa TANU walifika mara nyingi kuzungumza na wanachama na viongozi wao. Picha ya chini wanaonekana Zuberi Mtemvu (aliyeshika tama) aliyekuwa Katibu Mwenezi wa TANU akiwa na Sheikh Suleiman Takadir Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU na kushoto yake Mzee John Rupia Makamu wa Rais wa TANU wakiwa katika moja ya hafla za TANU katika tawi hilo. Rais wa TANU Mwalimu Nyerere haonekani amezibwa na John Rupia lakini mlinzi wake katika vijana wa BANTU Group anaoenakana amesimamakaribu yake amevaa lubega.

Kushoto: John Rupia, Julius Nyerere, Zuberi Mtemvu
Waliosimama nyuma yao ni BANTU Group Vijana Walinzi wa Viongozi wa TANU
Ofisi ya TANU Mtaa wa Jaribu Magomeni Mapipa kama ilivyokuwa ikionekana katika miaka ya 1950 ikiwa imezungikwa na wanachama wake.


No comments:

Post a Comment