Wednesday, January 13, 2010

MASUALA YA SIASA ZA ZANZIBAR NA MUUNGANO

IMECHANGIWA NA MOHAMED KHELEF


Khatib, kuruwiji na uraisi wa Zanzibar



Na Dhamiri Mkanga Silima



Waziri wa Nchi, Afisi ya Makamo wa Rais (Muungano), Muhammed SeifKhatib, aliwahi kuandika kuhusu Kuruwiji. Kuruwiji ni ndege kichaka na visasili vinamnasibisha ndege huyu na tabia ya kukitia aibu kichaka anacholalia kila asubuhi na kukisifu kila jioni.



Jua linapozama na Kuruwiji akawa anataka pahala pa kumsitiri, huanza kukiimbia nyimbo za kukibembeleza kichaka hicho: “Kichaka udi, kichaka manukato, kichaka miski, kichaka pompia, kichaka mpachori, kichaka kilua, kichaka asumini, kichaka waridi, kichaka zamaradi!” Lakini akiamka tu asubuhi, kitu cha mwanzo anachofanya ni kukishambulia kwa matusi: “Kichaka uvundo, kichaka mkojo, kichaka kinyesi, kichaka mbu, kichaka mateso, kichaka balaa!”



Khatib ni miongoni mwa mawaziri wa muda mrefu kwenye Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Labda anaweza kuwa anashikilia rekodi ya Mzanzibari aliyewahi kuhudumu kwa muda mrefu kwenye Baraza hilo, maana amekuwa sehemu ya chombo hicho muhimu cha maamuzi ya Jamhuri hii tangu awamu ya pili hadi hivi leo. Na sasa, waziri huyu anatajwa kuwa mmoja wa watu wenye nia ya kuomba ridhaa ya Chama chake cha Mapinduzi (CCM) kugombea uraisi wa Zanzibar.

Lakini swali linaloulizwa na kila mtu hapa Zanzibar, hasa ndani ya CCM yenyewe, ni ikiwa waziri huyu anamaanisha nini kwa mustakabali wa Zanzibar. Je, ni kielelezo cha kiongozi anayehitajiwa na Zanzibar ya sasa? Je, katika utumishi wake kwenye Serikali ya Muungano, amethibitisha kuwa mwana wa kweli wa Zanzibar ambaye nchi inaweza kumtwisha dhamana ya kuviongoza visiwa hivi kwa maslahi ya Wazanzibari?



Kwa kuwa tayari tumeshaona magazeti kadhaa yakiandika kuhusu wagombea watarajiwa wa uraisi wa Zanzibar, akiwemo huyu Khatib, nimeonelea nami nishike kalamu angalau niweke rekodi sawa kuhusu baadhi ya watarajiwa hao, ili hapo vikao vitakapokaa kufanya maamuzi, vijuwe nani ni nani na anamaanisha nini kwetu.



Nami nisivunganyie maneno. Niseme wazi na mwanzoni kabisa, kwamba ikiwa maamuzi ya Wazanzibari ni muhimu katika kuamua nani awe kiongozi wao, basi CCM itakuja kufanya kosa la mwaka kumteua Khatib kuwa mgombea wake. Nina sababu tatu kubwa za utabiri huu.



Kwanza, Khatib ana udhaifu wa kutokuujua mwenendo wa siasa za Zanzibar. Nakusudia kuwa, huyu ni aina ya mwanasiasa anayeishi sana kwenye ukale kiasi ya kushindwa kusoma alama mpya za nyakati hata kama zimebandikwa mbele yake. Hili limemfanya awe si mdomo, si masikio wala si macho ya Zanzibar, na hivyo rikodi yake ya kuwa Mzanzibari aliyekaa muda mrefu kwenye Baraza la Mawaziri la Muungano, haina maana yoyote kwa Zanzibar. Kinyume chake, hili limemfanya awe pia anashikilia rikodi ya mgombea mtarajiwa asiyependwa zaidi hapa Zanzibar!



Kwa hivyo, hilo la kutokuujua mwenendo wa siasa linamzalishia pia udhaifu mwengine wa kisiasa, nalo ni kukosa himaya. Siasa ni watu. Na watu ndio ambao Khatib hanao hapa Zanzibar. Na kinachomkosesha watu ni vile kukosa kwake mguso wa hisia za pao. Uweledi wake wa siasa anaotamba nao, ikiwa kweli anao, basi unakomea huko huko Bara ambako amekuwa akikutumikia kwa takribani umri wake wote wa kisiasa. Kwa Zanzibar, Khatib anahisabika kama mwana aliyekukana kwao. Haiimbi nyimbo za hapa, hachezi ngoma ya hapa wala haongei lugha ya hapa. Huyu ni mgeni kwa hakika.



Ndiyo maana, mara nyingi sio tu kwamba ameshindwa kuwa sauti ya Wazanzibari, bali amekuwa sauti dhidi ya Zanzibar. Na hapa kuna mifano ya karibuni kabisa. Kuelekea mwishoni mwa uraisi wa Dkt. Amani Karume, umekuwa msimu wa hisia za uzalendo wa Wazanzibari ndani ya Muungano. Ndani ya miaka hii, Wazanzibari walisimama pamoja kulinda heshima ya nchi yao ndani ya mipaka ya Tanzania kwa kutamka wazi kwamba Zanzibar ni nchi. Ndani ya kipindi hiki pia walishirikiana kudai nishati za mafuta na gesi asilia ziondolewe kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Ndani ya kipindi hiki pia, Dkt. Karume alionyesha ukomavu wa kiuongozi pale alipoamua kukutana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kwa lengo la kuzungumzia maslahi ya Zanzibar!



Mambo hayo ndiyo yanayoumba siasa za Zanzibar. Mwanasiasa anayekuwa sehemu ya mambo hayo, huhisabika kuwa amesimama upande wa Wazanzibari na ndiye mwenye turufu. Kinyume chake, yaani mwanasiasa aliyejitenga kando na mchakato huo na, au, anayepinga kila linaloungwa mkono na Wazanzibari, hana nafasi kwa Zanzibar. Na hivyo ndivyo alivyo Khatib!



Kwake, Zanzibar si nchi wala haipaswi kuwa. Kwake, Zanzibar haijawahi kuwa na haki ya kumiliki nishati ya mafuta na gesi asilia wala haipaswi kuwa nayo. Kwake, Rais Karume hakuwa na sababu ya kuzungumza na Maalim Seif kumaliza miongo mitano ya siasa za uhasama katika visiwa hivi. Kwake, kila lenye maslahi kwa Zanzibar kwa ujumla wake, lina hasara kwake peke yake. Na bado, huyu huyu ndiye anayeutaka uraisi wa Zanzibar!



Kutokuujuwa kwake muelekeo wa siasa na kukosa kwake himaya hapa Zanzibar, kwa pamoja, kunaunganika na udhaifu wa tatu wa Khatib; nao ni kuendekeza kwake chuki za ukabila na uzawa. Udhaifu huu haustahmiliki hata kidogo katika ulimwengu wa sasa. Ambako Marekani, mtoto wa Mkenya sasa ni raisi, msamiati wa Wazanzibari wenye asili ya Pemba na au wenye asili ya Kiarabu na Kihindi kushikilia nafasi katika serikali ya Zanzibar hauna nafasi kabisa katika mawazo ya Khatib.



Kuthibitisha hili, pitia makala zake za Kipanga, uone muakisiko wa chuki hizo. Na hili limeigharimu sana Zanzibar kwa ujumla wake. Kwa mfano, wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kutangaza kwamba Zanzibar kuna magaidi. Kila mtu anajua kuwa ule ulikuwa ni uzushi wenye malengo ya kisiasa. Matokeo yake, kauli hii ilizifanya nchi nyingi ambazo raia wake hutembelea Zanzibar kama watalii, zitoe onyo la kutoitembelea nchi yetu na, hivyo, biashara ya utalii, ambayo inategemewa na uchumi wa Zanzibar, ikaporomoka. Hasara ikawa kwetu.



Mfano mwengine. Wakati wa huo huo uwaziri wake wa Mambo ya Ndani, jeshi la Polisi likiwa chini yake lilifanya mauaji ya Januari 2001, Unguja na Pemba. Pamoja na u-CCM wangu, lazima niseme kwamba lile lilikuwa kosa kubwa kufanyika na yeye hawezi kujivua dhamana hiyo. Hasara ya kisiasa, kiuchumi na kijamii iliyopata Zanzibar haijaweza kufidiwa hadi leo.



Isitoshe, ikiwa leo hii upepo wa mambo utabadilika na ikafunguliwa kesi kuchunguza mauaji yale, ni wazi kuwa Khatib atapanda kizimbani kujibu mashtaka dhidi yake. Kwa hivyo, mgombea huyu mtarajiwa ni pia mshtakiwa mtarajiwa wa The Hague!



Lakini, hata kama hakushitakiwa, rekodi hiyo ya 2001 inasema ukweli mmoja: kwamba mtu huyu akipata uraisi wa Zanzibar, na namna alivyo mtu wa chuki na ubaguzi, atakuwa tayari kufanya lolote kulazimisha kukubalika kwake. Hapa ikumbukwe kuwa sizungumzii kuwafanyia lolote watu wa vyama vya upinzani tu, bali hata sisi wa CCM ambao leo hii tunampinga. Kwamba baada ya Januari 2001, inaonesha hakuna linaloweza kumshinda Khatib!



Nihitimishe uchambuzi huu kukumbushia kwamba Khatib ana udhaifu wa aina tatu, ambao kama utazingatiwa vyema basi hatufai kuwa mgombea wetu ndani ya CCM, vyenginevyo tuwe tumejikubalisha kufeli vibaya kama Chama kikongwe chenye heshima ya kisiasa barani Afrika na duniani kwa ujumla. Moja, haijui Zanzibar na siasa zake na hivyo, mbili, anakosa himaya ya kisiasa hata huku kwao na, tatu, matokeo yake anaongozwa na chuki na hamasa za kibaguzi.



Kwa ukosefu wake wa kuyajua mapigo ya moyo ya Wazanzibari, amekuwa akitumia nyimbo zile zile kongwe kuzungumzia Zanzibar mpya. Wakati Zanzibar mpya inadai mamlaka zaidi ndani ya Muungano, yeye ameendeleza nyimbo za kuwatisha wale wanaoukosoa mfumo uliopo wa Muungano. Wakati Zanzibar mpya inataka siasa za maelewano na umoja, yeye bado anatumia vyombo vya habari anavyovimiliki kusambaza kasumba za eti sisi wana-CCM tunaojenga mahusiano mema na wapinzani wetu, tunahatarisha uhai wa Chama chetu na wa Muungano.



Kwa kukosa kujuwa nini hasa muelekeo wa Zanzibar kwa miaka ijayo, ndiyo maana amejiteulia kundi la watu wanaojuilikana kwa siasa za kimajimbo na kibaguzi kuwa wasaidizi wake. Kuna msemo wa Kiyunani: “Niambie marafiki zako, nikwambie wewe ni nani?” Angalia marafiki na wapiga debe wa Khatib, halafu utamjua yeye ni nani: kwenye orodha wamo Vuai Ali Vuai, Naibu Katibu Mwenezi wa CCM na Hafidh Ali Tahir, Mbunge wa Dimani. Wote wanafahamika kwa siasa zao za chuki, ambazo ni miongoni mwa sababu za Zanzibar kurudi nyuma kimaendeleo.



Hii maana yake ni kwamba, ikiwa Zanzibar itakuja kukabidhiwa mikononi mwa Khatib na kundi lake, Wazanzibari watapaswa kuhesabu miaka mingine ya siasa za uhasama, ugomvi na kutokuaminiana. Na ukweli ni kuwa Zanzibar ya aina hiyo haina maslahi kwa yeyote, si kwa Wazanzibari wenyewe wala kwa ndugu zetu wa Tanzania Bara na majirani wengine!



Hatua ya karibuni ya Rais Karume kuonesha uongozi halisi kwa kuamua kutumia muda wake uliobakia madarakani kuwaunganisha Wazanzibari, imewachukiza sana watu wa kundi la akina Khatib. Kwao wao, mgogoro wa Zanzibar ndio unaojengea uhalali wao wa kupata vyeo. Wamepata vyeo si kwa sababu ya uwezo wao wa kiuongozi, bali kwa ustadi wao wa kuyasawiri matusi dhidi ya Wazanzibari wenzao wenye asili ya kisiwa cha Pemba na au ya Kiarabu. Soma vitabu vyake vya Kipanga utafahamu namaanisha nini. Zanzibar kuikabidhisha kwa Khatib ni sawa na kurudi tena kwenye zama za giza.



Giza si hili la umeme, bali giza la nyoyo na roho. Na akili ipi isiyo busara inayotaka kuirudisha nchi yetu huko!?



CHANZO: NIPASHE, 6 Januari 2010

1 comment:




  1. Brothers/Sister's. Are you looking for loan to finance your large or small business,we'll help you get the large amount of loan you desire for your business,we offer first class business and commercial loan to enable small scale business attain success in obtaining start up or refinance their business Bad credit rating accepted and poor business performance are accepted.apply today via email( arabloanfirmserves@gmail.com

    ReplyDelete