Monday, January 18, 2010

MALUMBANO YA SIASA ZA TANZANIA NA ZANZIBAR

From: yussuf_salim@hotmail.com, January 18, 2010


Makamba sikia : Amani atimiza ahadi kwa Marehemu Baba yake

Makamba anazidi kukiaibisha chama chake kwa mara nyengine tena, kwa kutoa kauli zisio na mvungu. Katika mtindo wake wa kawaida wa kusema kwanza halafu kufikiri baadae, anarejea tena kuwafanya viongozi wengine wa nchi, kukenya –kenya huku wakigubika nyuso zao zisionekane. Kwa viongozi wengine wa CCM hali hii kwa mara nyengine tena imewafanya wajionee aibu upya. Kauli za kuvurumisha maneno ovyo, hulengea aliyekuwemo na asiyekuwemo. Mwenyewe Makamba, akijiona stadi wa kusema, hatambui kwamba hajirejeshi yeye mwenyewe tu nyuma au sio kuirejesha CCM tu nyuma , bali heshima ya Tanzania nzima inaathirika wakati kiongozi wa juu kama yeye nchini, kila kukicha, heshi kuteleza na kujiona kapwetereka kwenye matope na kuipaka nchi nzima matope.

Hivi punde shehe Makamba aliushangaza ulimwengu wa waungwana alipotoa kauli za kuwakashif Watanzania wanaoheshimiwa Ulimwengu kote. Kauli hizo zilikuwa sawa na matusi mazito kwa Watanzania wote, Waafrika na jumuia ya Kimataifa kwa jumla ambao walikuwa wakiwathamini na kuwa enzi viongozi hao wakiwemo Mwana Diplomasia mashuhuri Salim Ahmed Salim na Mheshimiwa Jaji Warioba, wote wawili wakiwahi kushika nyadhifa nzito za Uwaziri Mkuu wa Tanzania. Vipaji viwili hivi vimeshaweka rikodi sio Tanzania tu bali hata Ulimwengu mzima wa Kimataifa. Leo Katibu Mkuu wa CCM anawatukana Viongozi hao hadharani bila kuona hata haya au vibaya.

Kipi chema mtu utatarajia kitatoka katika mdomo wa Katibu Mkuu huyu, ikiwa bwana huyu wakati huo huo atajiweka mstari wa mbele kutaka kuwafyeka wale Wabunge mashujaa wa CCM waliojitolea kutetea maslahi ya Watanzania wasiojiweza na kutetea mali ya Tanzania kwa jumla, lipi jengine hatalifanya. Badala ya desturi ya Kiongozi wa juu wa chama kujivunia kuwa na Wabunge wapenda nchi na walinda mustakbal kama hawa, kinyume chake tunamuona anatumia kila mbinu, pamoja na kubadili katiba, kuhakikisha anawaangamiza Wabunge hao. Mshangao mkubwa na bumbuwazi linampiga mtu akitanabahi kwamba kuna Kiongozi kama huyu: na kujiuliza ni maslahi ya nani mtu huyu anayatetea? Ya mafisadi waliopita au ni ufisadi ujao? Na ufisadi huo una majoka gani ndani ya mapango yake? Kama itakavyokuwa, majoka hayo hayataleta maendeleo Tanzania bali yatazidi kurejesha maendeleo nyuma na kuzidisha umasiki kwa wengi na kuzidisha utajiri kwa wachache. Ama kweli, wale waliosema kwamba kuna wanajeshi fulani hutumia vichwa vyao na wengine kutumia BUNDUKI zao, hawajakosea.

Hivi punde Wazanzibari wameamua kuchoshwa na kupigana na kuchingana wenyewe kwa wenyewe na wameamua kurudi kwa Mola wao, kumuomba msamaha kwa yaliyopita na kuamua kusameheana na kuheshimiana kama ni Wazanzibari sawa bila ya kujali mirengo yao. Wazanzibari wametanabahi kwamba hakuna yoyote kati yao aliye bora ya mwenziwe mbele ya Nchi yake na mbele ya Mola wake. Wote wamezaliwa sawa na wana haki sawa katika nchi yao ya Zanzibar. Viongozi, Rais Amani na Maalim Seif, wameamua kuchukuwa dhamana zao walizopewa na wafuasi wao, nayo ni kuwaongoza wao na nchi yao ielekee kwenye Mustakbal bora wa Zanzibar na Wazanzibari wote.

Laa, kwa Makamba hayo haiwezekani, jambo jema na usalama kwake ni marufuku kwa Zanzibar. Kila watu wakitesana, kuuwana, kunajisiana, kufanya watoto wadogo mayatima na wanawake vizuka ndio akina Makamba wanavyofurahi. Wanageuka kama wale Waspeni wanaofurahishwa na mchezo wa n´gombe na kuona raha pale n´gombe anapochirizika damu na hatimae kutiwa upanga wa roho na kufyatua fyatua miguu huku wakikata roho wakizungukwa na dimbwi la damu. Hali kama hiyo huwa wanaifurahia kina Makamba wanapowaona Wazanzibari wakikata roho wakimiminika na kuogelea katika madimbwi ya damu zao wenyewe.

Akina Makamba hawachoki kutumia vibaraka na vitimba kwiri vyao vinavyo vikiwemo vile vinavyo gombania tiket za Uraisi wa Zanzibar kuvusha wanajeshi na polisi kutoka Bara kwenda Zanzibar kuuwa, kunajisi n.k. na wao wakikaa juu ya majukwaa na kupiga makofi.

Viongozi wema mfano wa akina Mwanadiplomasia Salim Ahmed, Jaji Warioba, Wabunge washupavu wanaopigania walalahoi, ni viongozi wanao hatarisha maslahi ya akina Makamaba na Msekwa. Viongozi wanaowatakia mema Watanzania ni maadui kwa watu kama Makamba na Msekwa. Kina Makamba hawaoni raha kama madimbwi ya damu za Wazanzibari hayamwagiki kila kukiwa na uchaguzi. Kwa hivyo kwao Viongozi kama Rais Amani na Maalim Seif ni watu wanaowaogopa sana na sifa kwao kuwawekea kila vizingiti.

Lakini Makamba kasahau kwamba kuna jambo linaloitwa ”Ya Mbayana”, na hili lina ashirika wazi pale Makamba anapojaribu kumnukuu Mwenyekiti Mao na kusema kwamba ”ukimuona adui anakusifu ujue ana lake. ” Kauli hii ina ukweli kabisa na kumdhihirisha nani ni adui wa Wazanzibari na adui wa kutaka kumuangamiza Rais Amani, yule wa msatri wa mbele kabisa wa kutaka kuafanya hivyo ni Makamba akifuatiwa na Msekwa. Wanajaribu kumramba kisogo Rais Amani wakidhani hawaoni. Wamejionyesha kwamba ni wao ndio hasa MAADUI wenyewe, kama alivyosema Mwenyekiti Mao. Huyu wa pili, yaani Msekwa, vile vile anamuonea choyo cha kisiasa Rais Amani kwa kuwa ingawa ni Makamu Mwenyekiti kama yeye, lakini mwenziwe ni Rais wa nchi nzima, ingawa walifanya mbinu za kuinyan´ganya Zanzibar U-Makamu wake wa U-Rais.

Napenda kumkumbusha Katibu Mkuu Makamba kwamba, Mwenyekiti Mao katika mengi aliyosema, alisema vile vile kwamba, ”kuna kutofautiana kwa kimgongano na kutofautina kusiko kwa kimgongano” yaani ”antagonistic contraditions na non-antagonistic contradictons” au msemo huo haujui ? Kutokana na msemo huo ndio maana Mwenyekiti Mao na Chang Kai Chek wakaamua kuungana na kumtoa Mjapani NCHINI mwao. Sasa inaonyesha Rais Amani na Maalim Seif wamesoma somo hilo vizuri, ila Katibu Makamba bado anataka damu imwagike akidhani vitimbwa kwiri wake watamsaidia kwa njama hizo.

Somo jengine muhimu Mheshimiwa Makamba inafaa ajifunze ni kwamba Rais Amani anatekeleza lile Marehemu Baba yake alilolianza lakini kutowahi kulimaliza. Sidhani kama hili analijua ndugu Makamba, kwani ni wale tu wanaojua shina na kina cha historia ya Zanzibar ndio wanaoweza kujua undani huo. Makamba akae ajue kwamba kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume na Sh. Ali Muhsin walikuwa na mazungumzo ya siri kabisa kutaka kufanya serikali ya MSETO Zanzibar. Kwa bahati hii au ile Mapinduzi yakatokea kabla mpango huo kutekelezwa na ndio maana wakati Sh. Ali Muhsin akishindikizwa kuingia katika kambi ya Rahaleo alipokamatwa baada ya Mapinduzi Mzee Karume akamwambia kwamba ”haya Mapinduzi yameharibu mpango wetu Serikali ya Kitaifa”.

Hio ni sababu moja wapo ya kumfanya Rais Amani akawa na deni la kutimiza ahadi kwa Marehemu Baba yake.

Wasalaam

Dr. Yussuf S. Salim

Copenhagen

Denmark

No comments:

Post a Comment