Wednesday, January 20, 2010

HABARI ZA MAENDELEO YANGU KATIKA MASOMO YA UZAMIVU

1. Nilipoomba kwenda kusoma kwa kutumia Udhamini wa Serikali ya nchi ya Marekeni (USA) chini ya Ufadhili wa Mfuko wa Hubert Horatio Humphrey (HHH Fellowship) mwaka 2007, nilielezea nia yangu ya kwenda kusomea masomo yatakayonielekeza katika kuja kuanzisha Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wananchi (MZUMBE UNIVERSITY LEGAL AID CLINIC - MULAC)kwetu Chuo Kikuu, Mzumbe, Tanzania.

2. Nilibahatika kupata fursa ya kwenda kusoma nchini USA katika Chuo cha American University, Washington College of Law (WCL); kilichopo mjini Washington, DC; ambao ni mji mkuu wa Serikali ya nchi hiyo.

3. Niliondoka na kwenda USA kufanya masomo hayo kuanzia Agosti 2, 2008 hadi Juni 12, 2009. Wakati nipo masomoni, nilitayarisha Andiko lililoeleza namna ya kuanzisha Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wananchi (Starting a Legal Aid Clinic at Mzumbe University, Tanzania).

4. Niliporejea Juni 13, 2009 na kuripoti ofisini wiki iliyofuata, nilimuona Mkuu wangu wa Kitivo, Bw. Eleuter Gabriel Mushi na kumfahamisha juu ya masomo yangu yaliyonichukua miezi kumi huko USA. Yeye alinielekeza kwamba jambo hilo kiutaratibu huanzia katika Idara yangu husika (Idara ya Sheria za Kimataifa - Dept. of International Law). Baada ya kulishughulikia katika Idara kwa kuitisha mkutano wa Wanataaaluma na kuelezea juu ya Andiko langu na kujadiliwa (Paper Presentation), nipokee maoni na mapendekezo ya wasomi ili niyaingize katika Andiko hilo kwa nia ya kuliboresha.

5. Nilipofikisha Andiko langu kwa Mkuu wangu wa Idara; wakati huo Profesa Padma Sabaya, akaahidi kulishughulikia jambo hilo. Nilipolifuatilia baada ya wiki moja, nikaarifiwa na Katibu Muhtasi kwamba huyu Profesa kaenda India kwao kwa likizo ya mwezi mmoja. Nikauliza aliyemuachia ofisi. Nikaambiwa kuwa hakumuachia ofisi mtu yeyote na hivyo Andiko langu analo yeye na hajalifanyia kazi.

6. Kwa bahati wakati huo huo, ikatoka orodha mpya ya Walimu wa Kitivo cha Sheria na Idara zao zilizopangwa upya. Nikajikuta nimepangwa katika Idara ya Sheria za Madai na Jinai (Civil and Criminal Law Dept.) nami sikuwa na neno juu ya hilo. Mkuu wa Idara hii ni Bw. Ignas Punge. Hivyo nikachukua hatua ya kumuona mkuu wangu huyo mpya na kumweleza juu ya azma yangu ya kutoa Andiko kwa Wanataaluma wa Mzumbe kwa Kujadiliwa kwa ujumla. Yeye aliliafiki moja kwa moja na kuniagiza nimfikishie andiko hilo mapema iwezekanavyo.

7. Tarehe 15/10/2009 nilifikisha andiko hilo kwa Mkuu wangu wa Idara Bw. Ignas Pungem kupitia kwa Katibu Muhtasi wa Kitivo cha Sheria. Hii ilikuwa tayari mwezi mmoja umepita tangu nifikishe andiko langu kwa Mkuu wa Idara wa Kwanza Profesa Padma Sabaya. Safari hii kwa bahati mbaya Andiko langu halikumfikia Mkuu wa Idara yangu kama nilivyotaraji.

8. Mkuu wangu huyo wa Idara akishirikiana na Wakuu wa Idara wenzake Bw. Benjamin Jonas na Bw. Cosmas Julius walifanya bidii kubwa kuona kwamba Andiko langu linajadiliwa na Wanataaluma ipasavyo tarehe 1/9/2009; na kuniongoza jinsi ya kufanya matayarisho muhimu ya maandalizi ili jambo hilo lifanyike ipasavyo. Mojawapo ya mambo hayo ilikuwa kumtafuta Mjadili Mkuu (Main Discussant), kuandaa ratiba na kutoa matangazo chuoni juu ya tukio hilo; mambo ambayo niliyafanya kwa ufanisi mkubwa chini ya uongozi na maelekezo yao.

9. Nililazimika kuanza mara moja kazi ya kuingiza mapendekezo na maoni ya wachokozi (critics) walioshiriki katika Mjadala wa tarehe 1/9/2009. Pamoja na kwamba sikuweza kupata fedha mara moja za kufanyia kazi hiyo. Baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na wachokozi hao ni kuwa ni muhimu kwa mimi kushirikisha vyombo na asasi na wadau mbalimbali wa kisheria juu ya jambo hili; na pia kufanya utafiti mdogo (situational analysis) kujionea na kujihakikisha katika Mahakama za ngazi ya chini kabisa nchini zinaamua kesi za aina ipi, ili nasi hatimaye tutakapokuja kuanza Kituo Chetu cha Msaada wa Sheria kwa Wananchi, tujue tutaanzia na kesi za aina ipi.

10. Nilianza na kuwaona wadau mmoja mmoja na kufika katika mahakama za Mwanzo za karibu na Chuoni kwetu. Pia nilijitahidi kuwahoji binafsi Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu Raymond Mwaikasu (tarehe 19/9/2009) wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO) na Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu James Mwalusanya aliyeko Dodoma.

11. Nilitembelea pia Mahakama za Wilaya ya Morogoro Vijijini (Tawa Mkuyuni,Mikese, Ngerengere, Manispaa ya Morogoro (Nunge, Chamwino, Kingolwira), Mvomero (Mgeta, Mkongeni(Vikenge) na Dodoma Manispaa(Makole). Wakati wote nitembembelea Mahakama hizi mbalimbali, nilishaomba Masurufu kazi yaliyofikia Tshs.992,200.500/= ili kuifanya kazi hiyo kikamilifu. Hadi leo hii niandikavyo Ufupisho huu, tarehe 20/1/2010, Fomu hiyo ya Masurufu iliyosainiwa na Mkuu wangu wa Idara Bw. Ignas Punge toka tarehe 18/9/2009, iko mezani kwa Mkuu wangu wa Kurugenzi cha Mafunzo Endelevu (Institute of Continuing Education - ICE); ambaye ndio mwenye mafungu husika ya kufanyia utafiti wangu; na hivyo ndio muidhinishaji wa mwisho wa kutolewa masurufu hayo chini ya Kurugenzi yake. Yaani miezi minne (4) baadaye, bila kufahamu ni lini fomu hiyo itaridhiwa na kuelekezwa ikaandikiwe malipo hayo.



12. Kwa uzoefu wa kujua tatizo nililolielezea hapo juu, hata hivyo; tulishirikiana vizuri sana na viongozi hao waliotajwa na kufanikwa kumpata Mjadili Mkuu (Discussant) wa Andiko langu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mhadhiri Msaidizi, Bi Asina Omari; na kazi hiyo ya kitaaluma ya kutoa Andiko hilo kwa Wanataaluma wa Mzumbe ilifanyika vizuri tarehe 1/9/2009 katika Darasa la LT.3 Chuoni Mzumbe kuanzia saa 4.00 asubuhi. Walioshiriki katika kufanikisha siku hiyo ni pamoja na Bw. Thobias Mnyasenga wa Kitivo Cha Sheria na Bw. Evans Kautipe na Bw. Barnabas Chomboko; wote wa Idara ya Huduma za Kiufundi ya Maktaba Kuu ya Chuo Kikuu Mzumbe.

13. Mara baada ya zoezi hili; ili jambo hili lifikie linakotakiwa; nililazimika mara moja kuanza kuingiza maoni na mapendekezo mbalimbali kutoka katika Wachokozi walioshiriki (critics) katika Andiko langu. Pia niliingiza yale niliyoyashuhudia katika Mahakama za Mwanzo mbalimbali nilikotembelea na maoni na mapendekezo ya wadau nilioweza kuwahoji. Wakati huo huo sijakata tamaa kwamba nitaendelea kuwahoji wadau wengine zaidi na kutembelea Mahakama na Ofisi nyingine zaidi katika kufanikisha zoezi hili.

14. Tarehe 28/10/2009 kulikuwa na Mkutano wa Kitivo cha Sheria (Internal Examiners Board of the Faculty of Law). Nilitaraji kwa nia njema kabisa kwamba Andiko langu lingekuwa moja ya Ajenda ya Mkutano huu kwa kuwa hakukuwa na fursa ya mkutano mwingine Kitivoni kujadili jambo hili. Kwa bahati mbaya, Andiko langu halikuwahi kumfikia Mkuu wangu wa Idara Bw. Ignas Punge; badala yake Katibu Muhtasi Grace Nyamhagata, alifikisha lile Andiko langu kwa mwalimu mwingine kwa makosa (Prof. Khan). Baada ya kugundua kosa hili siku hiyo ya mkutano, nikahakikisha safari hii nimefikisha Andiko langu kwa Mkuu wangu kwa mikono yangu miwili. Mkuu wangu wa Idara amenifahamisha kwamba Andiko hilo litajadiliwa katika kikao kijacho cha Kitivo kabla ya kwenda kwenye vikao vya juu zaidi.

15. Hivyo, leo niandikavyo Ufupisho huu wa jambo hili; tarehe 20/1/2010; haijatokea fursa nyingine ya kufanyika Mkutano katika Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu Mzumbe. Na hiyo ndio fursa inayosubiriwa ili Andiko langu lijadiliwe kabla ya kufikishwa na Kitivo katika Mkutano wa Kitivo (Faculty of Law Board), ili hatimaye likikishwe katika Kamati ya Seneti (senate). Fursa inayoonekana kujitokeza hivi karibuni ni Mkutano wa Kitivo Ujao utakaojadili Matokeo ya Mitihani ya Kitivo cha Sheria unaotarajiwa kufanyika baada ya kusasahihishwa Mitihani ya Semesta ya Kwanza ya Chuo kwa mwaka 2009/2010, kunako mwishoni mwa mwezi Februari au mwanzoni mwa Machi, 2010. Nami naisubiri fursa hiyo kwa hamu sana, ili hatimaye jambo hili liweze kupiga hatua inayofuata.

16. Hadi hapa, nilidhamiria kuelezea mtulinga nipitiao katika kufanikisha jambo hili ambalo si tu kuwa ni kwa manufaa ya Chuo Kikuu Mzumbe, bali ni kwa manufaa yangu kitaaluma kwa sababu hatimaye nataraji kulichapisha Andiko hilo litakapopitishwa na Seneti, ili iwe sehemu ya kufikiriwa kwangu kupandishwa cheo; pamoja na Maandiko mengine. Kigezo kimojawapo cha kupandishwa cheo katika ngazi za kitaaluma katika vyuo vya kitaaluma ni kutoa machapisho ya kitaaluma.

Zainab Mwatawala, Chuo Kikuu Mzumbe, 21/1/2010.

No comments:

Post a Comment