Saturday, January 16, 2010

MALUMBANO JUU YA SIASA ZA ZANZIBAR

MAJIBU YALIYOJIBU BARUA YA ABDALLAH HASHIM WA ZANZIBAR (katika internet)

Katika barua yako iliyojaa falsafa umeandika hivi:



“Sasa ndugu yangu - Jee jitihada za kuwaletea Wazanzibari maendeleo ya kiuchumi na kijamii hayafungamatani kama chanda na pete kwenye masuali haya ya haki za binaadam? Ikiwa si hivyo ninaomba unitaalamishe”.



Ningelipenda kusema tu kuwa huna haja ya kwenda mbali sana katika dunia yetu hii ya leo kupata mifano halisi (best practices) ambayo inatuonesha kwa vitendo jinsi maendeleo ya kiuchumi na kijamii yalivyoweza kupatikana nje ya mifumo yenye kuendeleza utawala bora na haki za binaadamu.



Kwa mfano, Singapore, South Korea, Indonesia na Taiwan ni nchi ambazo zimepiga hatua kubwa sana kimaendeleo na kiuchumi wakati wa tawala za kidikteta zilizokuwa haziheshimu haja ya kuendeleza utawala bora na haki za binaadamu katika miaka ya sabini hadi thamanini. Hivi sasa, nchi zote hizi zinaendelea kupiga hatua kubwa sana kiuchumi na kimaendeleo inagawaje kidogo kidogo zimeanza kujenga mihimili mipya na taasisi zinazosisitiza umuhimu wa kuendeleza tawala bora na kuheshimu haki za binaadamu. Lakini, China, kwa sababu zinazojuulikana, bado inaendeleza sera ile ile ya kidikteta yenye muelekeo wa kutoheshimu utekelezaji wa dhana ya utawala bora na haki za binaadamu. Hata hivyo, nani atakataa kuwa China ya leo imepiga hatua kubwa sana kimaendeleo na kiuchumi kuliko wakati mwingine wowote katika historia yake? Lakini, angalia rekodi yake katika nyanja za utawala bora na haki za binadamu, Tibet, na mengi mengineyo..





2) Kwa namna nionavyo mimi kikabwera, ni kwamba katika jamii yeyote ile (any given society) ambayo inayo ukosefu wa kuheshimu, kutetea na kulinda haki za kibinaadamu na za kijamii na ikiwa nchi hiyo ina vikwazo vyenye misingi ya ubaguzi wa aina yeyote ile, basi katu wizani wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii utakuwa unakwenda pero.



Nafikiri jibu la suala hili utalipata katika jibu langu la awali. Sina uhakika wa aina ya ubaguzi unaokusudia hapa; lakini, utakumbuka kuwa Singapore na Malaysia waliwahi kuendeleza sera maarufu iliyokuwa ikijuulikana kama “positive discrimination” kwa maana ya kujaribu kuweka uwiano sawa baina ya makabila fulani nchini humo katika kutoa elimu. Hata kule Marekani kuna kitu kinachojuulikana kama “Affirmative Action”.





3) Umesema katika andiko lako kwamba, mambo yanayohusiana na haki za binaadam hayo yanaihusu na kushughulikiwa na Jumuiya ya Zanzibar Legal Service. Nyinyi hamashughuliki nayo. Kwa mmuriko wangu mimi, jumuiya hii husika inaweza kuwa kama ni "jicho" "masikio" na "mdomo" wa kuchunguza na kutetea kama haki hizo za kimsingi za kiraia zinanaheshimiwa na kutekelezwa kufuatana na katiba ya nchi /taifa, na ndipo hapo, miongoni mwa niliyoandika katika andiko langu kwako jana; ili kukumbushana zile sheria za mabavu za 1964, 1967 na 1968 zilizoweka kikatiba theluthi ngapi ya kila kabila hapo kijiweni lina haki ya elimu za juu na zile nafasi za kazi za kimadaraka/kutawala etc.



Ni kweli kabisa, ZIRPP kwa mujibu wa katiba yake, haina “mandate” ya kushughulikia masuala ya haki za binadamu. Hilo ni jukumu la Zanzibar Legal Services. Sisi tunaamini dhana ya “division of labour” ili kuepukana na uwezekano wa kujiingiza katika kila kitu na hivyo kujikuta tunaanzisha jumuiya zenye majukumu yanayofanana. Hii itasababisha kuwepo kwa “duplication of efforts” na “overlapping mandates”.



Kwa mfano, UN ilipoanzishwa mnamo mwaka 1945, jukumu lake kubwa lilikuwa ni kushughulikia masuala ya “conflict resolution” kwa madhumuni ya kuiepusha dunia na uwezekano wa kutokea vita vyengine vikuu. Lakini, baada ya muda kupita, ilionekana haja ya kuzishirikisha nchi wanachama kushughulikia kwa pamoja masuala mbali mbali ya kiuchumi na kijamii. Ndio maana “Specialized Agencies” na “Funds and Programs” kama vile WHO, UNESCO, FAO, UNDP, UNICEF, UNFPA, WFP na kadhalika zilipoanzishwa.



Kwa upande wa NGOs, nako kulijitokeza jumuiya kama vile International Peace Academy (IPA), Amnesty International, Human Rights Watch na kadhalika, ambazo zilianzishwa kwa madhumuni ya kukabiliana na masuala ya haki za binaadamu tu; na Save the Children Fund, Medicines Sans Frontieres, Action Aid, na kadhalika kwa ajili ya kukabiliana na masuala ya kiafya, kiuchumi na kijamii.



Na hapa kwetu, kama ilivyo katika nchi nyingi duniani, kila NGO inayoanzishwa huwa inalenga katika kukabiliana na madhumuni fulani. Kwa mfano, ZIORI inajikita zaidi katika masuala ya Historia na Bahari ya Hindi; Zanzibar Legal Services imejikita zaidi katika masuala ya sheria, utawala bora na haki za binadamu; Jumuiya ya Walemavu nayo inajihusisha zaidi katika kuendeleza haki za watu wenye ulemavu; na ZIRPP, kama nilivyokwisha kukueleza awali, tunajikita zaidi katika masuala ya sera za kiuchumi na kijamii.



Hii haina maana kuwa ZIRPP iko “neutral” au haiguswi kabisa na sera za kibaguzi na/au uvunjaji wa haki za binadamu; la hasha. Tunachosisitiza hapa ni kuwa ni vyema kuiachia Jumuiya yenye malengo yanayolingana na shughuli hizo; yenye mabingwa wa fani husika, na yenye utaalamu wa kutosha katika masuala hayo. Kwa upande wa ZIRPP, ni vyema nayo ikajikita katika kushughilikia masuala yanayoihusu kwa mujibu wa katiba yake, utaalamu ulionao na mabingwa wenye sifa zifaazo. Kwa mtaji huu, nafikiri tutakuwa “much more efficient and effective” katika utekelezaji wa majukumu yetu; badala ya kujiingiza katika kila fani, inayotuhusu na isiyotuhusu. Kwa msemo maarufu; tusingelipenda kuwa "Jack of all Trade, but Master of None".



4) Sifikiri wala siamini kwamba, kidhati taasisi yenu Sheikh Muhammad, itaweza kujitowa au kujitorosha kwenye mikakati na mijadala hiyo inayohusika na haki za kibinaadam. Kuamini na kuikiri fikira kama hiyo, itakuwa ni udanganifu wa kibinafsiya. Clinging on political neutrality on issues of Human Rights in a developing nation like ours, is not only naive and wish full thinking, but ribaldious or subtlely strategic (to be polite) in the light of the prevailing political structure. Possibly, hii ndio ile hali halisi uliyoitaja kutokana na ile "mandate" ya taasisi yenu na ile hoja yako uliyoileta kwenye andiko lako; au vipi ? Samahani ikiwa nimekoseya!!!





Hukukosea hata kidogo. Ni kweli kabisa ZIRPP haiwezi kujitowa kwenye mikakati na mijadala inayohusu haki za binadamu. Kila inapohitajika kushiriki, ZIRPP inafanya hivyo. Wawakilishi wetu, ikiwa ni pamoja na mimi binafsi, tumeshawahi kushiriki katika mijadala, warsha au kongamano mbali mbali zinazohusiana na masuala ya utawala bora na haki za binaadamu. Lakini, tumekuwa tukifanya hivyo kama waalikwa/washiriki katika mijadala iliyoandaliwa na kutayarishwa na taasisi husika; siyo ZIRPP. Na ndio maana nikasema, sisi kama ZIRPP hatuna “mandate” ya kujadili na kuyatolea maamuzi masuala hayo. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tunakwenda nje ya mipaka yetu. Kwani nani aliyedai kuwa “Zanzibar Legal Services” imeshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo?





6) Kwa kumalizia, na mimi vile vile ningependa kutumia lugha nyepesi kama wewe ndugu yangu na kufuata nyao zako za mifano ya gari na abiria wake. Gari nitakalopendeleya kupanda ni lile gari la maendeleo ya kiuchumi na kijamii ambalo halina ubaguzi wowote ule; linakwenda kila pande za taifa; sitapanda gari la taasisi yako ambalo linakwenda upande mmoja tu; hilo sijalipandapo. Natumai tumefahamiana - au vipi ?



Nimekufahamu sana ndugu yangu. Nakubaliana na wewe mia juu ya mia. Mimi binafsi sina dasturi ya kurukia gari bila ya kujua liendako. Hilo, ni kosa kubwa sana. Na, kwa hivyo, sitegemei wewe au mtu mwengine yoyote kufanya kosa kama hilo.



Mzanzibari Mwenzako,





Muhammad Yussuf
Interim Executive Director
Zanzibar Institute for Research and Public Policy
P.O. Box 416
Zanzibar
TANZANIA
Tel: 0777 707820 Cellular
Tel: 0242 233526 Office
Email: yussufm@gmail.com
Weblog: www.zirppo.wordpress.com

No comments:

Post a Comment