Wednesday, March 18, 2015

TANZANIA DENIED BIOMETRIC VOTERS REGISTRATION by NIGERIANS AND KENYANS !!!!

Kenya, Nigeria zagoma kuiazima Tanzania BVR

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva  
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi

Posted  Jumanne,Marchi17  2015  saa 9:16 AM

Kwa ufupi
Uamuzi wa NEC wa kutaka kuazima vifaa hivyo ni kutokana na mchakato wa uandikishaji kukwama kwenda kama ulivyopangwa kutokana na BVR 250 zilizopo kutokuwa na uwezo wa kuandikisha wapiga kura wote nchini.

Dar es Salaam.
 Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva amesema ofisi yake ilijaribu kuazima vifaa vya kielektroniki vya Biometric Voters Registration (BVR) katika nchi ya Kenya na Nigeria kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura, lakini nchi hizo zilikataa.Uamuzi wa NEC wa kutaka kuazima vifaa hivyo ni kutokana na mchakato wa uandikishaji kukwama kwenda kama ulivyopangwa kutokana na BVR 250 zilizopo kutokuwa na uwezo wa kuandikisha wapiga kura wote nchini.

Kitendo hicho kinaweza kusababisha Kura ya Maoni iliyopangwa kufanyika Aprili 30, 2015 mwaka huu kushindikana kwani mpaka sasa ni mkoa wa Njombe pekee ambako uandikishaji unaendelea kufanyika na unatarajiwa  kumalizika Aprili 12, 2015.

“Tulitaka kuazima Kenya lakini wakasema wanavitumia hata kama wamemaliza uchaguzi lakini mchakato wao wa uandikishaji unaendelea kutokana na kwamba watu wao wanapofikisha umri wa kuandikishwa wanawaingiza katika daftari lao,” alisema Jaji Lubuva na kuongeza:

“Tulikwenda Nigeria nako walitueleza wanazitumia. Kuazimana siyo jambo geni kwetu na huu ndiyo ukweli wake.”

Kuhusu mchakato wa uandikishaji mkoani Njombe alikoweka kambi alisema: “Uandikishaji huku unakwenda vizuri licha ya kauli mbalimbali na mimi nimekuwa nikiwahamasisha kujitokeza na tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa.”

Katika uchaguzi wa Ghana uliofanyika mwaka 2013 mfumo wa BVR ulitumika na kuonyesha mafanikio makubwa. Hata hivyo, Malawi iliukataa mfumo huo katika uchaguzi wa mwaka 2014 baada ya kuonyesha udhaifu mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2005.

Katika mahojiano maalumu na viongozi, wahariri na waandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen makao makuu ya kampuni hiyo Tabata Relini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema, NEC ilianza mchakato huo bila vifaa ikitegemea kuazima.

“Tulipokwenda Kenya na TCD (Kituo cha Demokrasia Tanzania) kuangalia walivyofanikisha mchakato huo wakatueleza kuwa NEC walikuja hapa kuazima BVR za kuandikisha... tulikuwa na mawaziri pale yaani ilikuwa aibu na walitueleza kama hadi Novemba hamjanunua hamuwezi kuandikisha. Walisema walikuwa na BVR 15,000 Kenya na waliandikisha wapiga kura milioni 14 kwa zaidi ya siku 45 hadi 60, sisi tuna matatizo.

“Wanatupa wasiwasi mkubwa, ikiwa lengo ni kuandikisha wapiga kura wote haiwezekani tukawa na kura ya maoni Aprili 30, 2015  lakini ukiwa unahitaji lazima uandikishe kwanza halafu ufanyike uhakiki wake, lakini muda huo hautoshi?

 Kauli hiyo ya Profesa Lipumba kuhusu kusimamishwa kwa kura ya maoni pia ilitolewa Februari 12, 2015 na viongozi wa vyama 22 vya siasa walipokutana na NEC kujadili mchakato huo wa uandikishaji kwa kutumia BVR.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema: “Mchakato huu ni muhimu na kama hautafanyika vizuri tutaichafua nchi yetu. Wadau washirikishwe na waridhike kwani kusipokuwa na uwazi kutaleta shida huko mbele.”

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema: “Ilitakiwa kutuhusisha katika hili mwanzo hadi mwisho. NEC wanatuonyesha hardware (vifaa vya kompyuta) badala ya software (programu ya kompyuta) zinavyofanya kazi ambayo tuna haja ya kuifahamu. Nani anatuuzia hizo hardware na nani anatuuzia software hizo?”

Profesa Lipumba alisema: “Serikali inatakiwa kujikita zaidi katika uandikishaji wapiga kura lakini Serikali haina fedha, bajeti ya Sh144 bilioni haipo sasa itakuwaje tunaingia katika kura ya maoni?

Mchakato wa Katiba 

Kuhusu mchakato wa Taifa kupata Katiba Mpya chini ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, Profesa Lipumba alisema hakuna matumaini hayo na kinachofanyika ni kutaka kuhalalisha utaratibu ambao haukuwa na uhalali kutoka kwa wananchi.

Alisema Februari mwaka 2013 wakati Rais Kikwete akizindua Vitambulisho vya Taifa, alisema vitambulisho hivyo vingeweza kutumika pia katika kupiga kura lakini hakuna utaratibu wowote uliotumika kuhakikisha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na NEC wanashirikiana.

Profesa Lipumba alisema baadaye Jaji Lubuva alinukuliwa akisema kazi ya uandikishaji itafanywa na tume yake na si mtu yeyote kwani haiwahusu.

Alisema bajeti ya mchakato huo ni Sh297 bilioni lakini alipotizama katika kasma ya tume kulikuwa na Sh7.01 bilioni, fedha za maendeleo na fedha za tume hazikuonekana.

“Ukienda kuchambua fedha ziko wapi huzioni, mimi nikauliza mbona bajeti ni kubwa lakini haijulikani iko wapi? Hata ukifanya ukaguzi unatakiwa kujua fedha hizo, katika maombi yake Tume iliomba Sh144 bilioni kwa ajili ya Kura ya Maoni lakini nayo haionekani katika vitabu vya Serikali sasa unajiuliza mchakato huo utakwendaje na fedha zimekwenda wapi?” alihoji na kuongeza:

“Suala la muda halitekelezeki, awali tume ilisema uandikishaji ungeanza Septemba, 2014, lakini ilishindwa, Desemba, 2014 ikafanya majaribio ya uandikishaji na katika Jimbo la Kawe wameandikisha wapiga kura kama 15,000 na ushee katika maeneo ya Bunju na Mbweni.

Walisema wamevuka malengo lakini ukienda katika takwimu za Sensa za mwaka 2012 za Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) haziendani. Bunju wapo 51,000 lakini hawa wameandikisha 15,000 wanasema wamevuka lengo sasa hapa kuna ukweli wowote?”

“Makambako walisema wataandikisha wapiga kura kama 31,000 lakini kwa Sensa ya mwaka 2012 ina wapiga kura zaidi ya 53,000 sasa utasemaje umevuka lengo na Jaji Lubuva alishatamka kwamba daftari la mwaka 2010 limechakaa hivyo wakisema tutumie daftari hilo haiwezekani.”

No comments:

Post a Comment