Saturday, March 30, 2013

MAONI YA C U F KWA TUME YA KATIBA TANZANIA

IMETUNDIKWA HAPA LEO HII  30  Machi, 2013. 


 THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF - Chama Cha Wananchi)

 MAONI YA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF- CHAMA CHA WANANCHI) KWA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA-  07 JANUARI,  2013

 UTANGULIZI;

Kwa niaba ya The Civic United Fronf (CUF-Chama Cha wananchi), na kwa niaba
 yangu binafsi napenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe Mwenyekiti wa
 Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na
  wajumbe  wako kwa kutualika rasmi Chama Cha CUF mbele ya Tume yako kutusikiliza na
 kupata maoni ya chama chetu juu ya mchakato huu muhimu kwa mustakbali mwema
 wa Taifa letu la Tanzania pamoja na watu wake.

 Aidha, tunampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Jakaya  Mrisho Kikwete kwa kuanzisha mchakato huu wa mapitio makubwa na kukusanya
 maoni ya katiba ya nchi yetu ili ikidhi matakwa ya wakati wa sasa na
 kutupeleka mbele zaidi kwa ustawi wa Taifa letu na watu wake. Madai haya ya
 kuandaa mchakato wa kuwa na katiba mpya inayokidhi matakwa ya wakati
 tulionao ni madai ya msingi ambayo chama chetu cha CUF kimekuwa
 kikiyasisitiza tangu kurejeshwa tena kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi
 vya siasa nchini mwaka 1992 na mara zote kuainisha suala hili katika
 manifesto zake za uchaguzi.

 Kutokana na muongozo wa Tume ya Mabadiliko ya katiba maoni yetu yamejikita
 katika maeneo yafuatayo:

(i)     Misingi na Maadili ya Kitaifa, Madaraka ya
(ii)    Wananchi, Muundo wa Nchi na Taifa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
(iii)    Haki za Binadamu na Wajibu wa Wananchi,
(iv)    Ardhi, Maliasili na Mazingira
 (v)    Mihimili ya Nchi (Ardhi, Watu na Utawala),
(vi)    Mihimili ya Utawala (Serikali,
(vii)    Bunge na Mahakama),
(viii)   Muundo na Mamlaka ya Serikali za Mitaa, na
(ix)    Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

 Kwa muhtasari maudhui haya Chama Cha Wananchi CUF kinapendekeza yafuatayo
 katika mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya Mwaka 1977;

 1. Muundo wa serikali tatu za muungano; yaani serikali ya Zanzibar, serikali
 ya Tanganyika na Serikali ya Mungano.

2. Uanzishwaji wa Tume huru za uchaguzi mapema iwezekanavyo. Kwa kuwa Tume
 ya uchaguzi inapaswa kuanza kazi zake mapema ili kufanikisha uchaguzi wa
 mwaka 2014/15, Tume haiwezi kusubiri mabadiliko ya katiba yakamilike ndio
 ianze kazi zake kwa Muundo mpya utakaopendekezwa.

3. Katiba yenye misingi ya mfumo wa uwajibikaji kwa watendaji wote wa umma
 na uainishwaji wa wazi wa Dira ya Taifa.

 4. Katiba itakayotoa haki kwa wagombea binafsi kushiriki katika uchaguzi.

5. Katiba itakayotoa uhuru wa vyama vya siasa kuungana muda wowote
 vitakapoona inafaa bila kupoteza usajili wa kawaida wa vyama hivyo.

6. Katiba itakayoweka muundo wa kuwa na Rais mtendaji "Executive President"
mwenye madaraka yanayopimika na kukubalika yasiyobana wala kuingilia au
 kuondoa uhuru wa utendaji kazi wa mihimili mingine ya dola. Rais achaguliwe
 kwa kupata asilimia 50+1 au zaidi ya kura zilizopigwa.

 7. Katiba yenye kuweka mfumo sahihi wa kulinda rasilimali za Taifa na
 kuhakikisha zinawanufaisha Watanzania wote kwa haki na usawa.

 8. Katiba itakayompa kila Mtanzania kwa nafasi yake kushiriki katika
 maendeleo ya nchi yake kwa kuwa na muundo wa serikali itakayoshirikisha
 kila   Mtanzania mwenye uzalendo wa kweli na uwezo wa kutoa mchango wake kwa ajili
 ya maendeleo na ustawi wa taifa.

 9. Katiba itakayoweka muundo wa uwakilishi wa uwiano (propotional
 representation) ili kila kura itakayopigwa kuwa na thamani tofauti na
 utaratibu wa sasa wa mshindi kuchukua vyote (winner takes all) hata kama ameshinda kwa kura moja.

 10. Katiba itakayo hakikisha uwepo wa mgawanyo wa madaraka kati ya serikali
 kuu na serikali za mitaa kwa kuondoa mfumo wa kuziburuza serikali hizo
 zilizokaribu na wananchi. Wilaya zisianzishwe kiholela. Vigezo vya
 halmashauri ya wilaya, miji, manispaa na majiji vitawekwa na sheria.
 Utawala wa mikoa uondolewe.

 11. Katiba itakayoweka msingi wa kuzuia ufisadi mkubwa wa rasilimali za
 nchi  hasa kwa njia ya uingiaji wa mikataba, Bunge likiwa ni chombo cha
 uwakilishi  wa wananchi lazima lishirikishwe.

 12. Katiba itakayoweka Muundo wa Tume huru za Taifa za uchaguzi tangu ngazi
ya uteuzi wake kuanzia ngazi ya Taifa hadi ngazi ya chini. Katiba
 itakayoto fursa matokeo ya uchaguzi kwa ngazi zote kuhojiwa mahakamani ikiwemo
  matoke ya uchaguzi wa Rais.

13. Katiba itakayopambanua mgawanyo wa madaraka na mamlaka ya mihimili yote
 mikuu katika nchi kwa maana ya Bunge, Serikali na Mahakama.

 14. Katiba itakayoeleza wazi kuhusu haki na wajibu wa dola kuhakikisha
 elimu ya watoto wetu, matumizi ya rasilimali za taifa, huduma za msingi za afya,
 ulinzi wa nchi yetu na sera za ardhi na kilimo zinasimamiwa na kutekelezwa
 kwa manufaa ya wananchi wote. Katiba ndiyo yenye nafasi ya kulinda haki hizi
za mwananchi na si huruma ya mtawala atakaye kuwepo kwa wakati huo au chama
 cha siasa. Sera za kitaifa lazima zifuate na kuheshimu haki zilizoainishwa
 ndani ya katiba.

15. Kuhakikisha kwamba wananchi wana madaraka ya kujiamulia wenyewe masuala
 ya maendeleo yao kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.;

16. Katiba yenye kulinda haki za binaadamu, na kupinga aina zote za ubadhilifu, ukandamizaji, ubaguzi wa aina yeyote iwe wa kidini, kikabila, kijinsia au kikanda.

17. Katiba yenye kuweka misingi endelevu ya kulinda amani ya nchi yetu.

 18. Masuala ya Ardhi yawe na sura kamili katika katiba mpya. Ardhi ni mali
 ya Watanzania wote. Mtanzania peke yake ndiye anayeweza kumiliki ardhi moja
 kwa moja.

 19. Katiba inayohakikisha kuwa haki za msingi za makundi maalum, wanawake,
 watoto, wazee wasiojiweza na walemavu zinalindwa kwa kuanishwa ndani ya
katiba.

Chama cha CUF kipo tayari kutoa ushirikiano unaostahiki kwa Tume katika
 kipindi chote cha mchakato huu pamoja na kushirikiana na Watanzania wote
 bila kujali itikadi za kisiasa na tofauti nyinginezo, kuhakikisha kuwa kwa
 pamoja nchi yetu inakuwa na katiba bora yenye kukidhi haja na matakwa ya
 hali ya kisiasa, kiuchumi na ustawi mwema wa jamii ya Watanzania.
 Ni matarajio ya Chama Cha Wananchi CUF kuwa maoni haya yatazingatiwa na
 kuingizwa katika rasimu ya mabadiliko ya katiba kwa mjadala na hatimaye
 kufanyiwa maamuzi yanayofaa kwa mustakbali mwema wa Taifa letu la Tanzania.

 Mungu Ibariki Tanzania na watu wake.

 HAKI SAWA KWA WOTE

 Prof Ibrahim Haruna Lipumba,
 Mwenyekiti wa CUF Taifa

 Contact;
 P.O.Box 10979
 Dar es salaam, Tanzania.
 lipumba@yahoo.com

No comments:

Post a Comment