Tuesday, March 26, 2013

SHEIKH BILAL REHANI WAIKELA ATINGA MAHAKAMANI KISUTU, DAR ES SALAAM, TANZANIA.


Imetundikwa hapa leo hii tarehe 26/3/2013.

Kutoka:  tz_muslim_community@yahoogroups.com, 25/3/2013.

Asalaam aleikum warahmatullah wa barakatuh,


Haya ndio yaliyojiri mahakama ya Kisutu pale Sheikh Bilal Rehani Waikela ambae alipanda kizimbani kutoa ushahidi wake upande wa washtakiwa.

Sheikh Waikela alikuja kutoka Tabora.

Hakika mahakama jana walisikia ambayo si wengi wamepata kuyasikia katika maisha yao yote.

Sheikh Waikela ameanza kwa kutaja umri wake wa miaka 87 na akaieleza mahakama kuwa ameanza kuutumikia Uislam mwaka 1940 akiwa katika Anjuman Muslim na ilipokuja East African Muslim Society ( EAMWS) akawa kiongozi.

Akaeleza pia yeye ni muasisi wa Mabaraza ya Misikiti Duniani makao makuu yake Makka.

Akasema yeye Tabora ni mtu wa tatu kujiunga na TANU na katika Tanganyika ni mtu wa 264.

Sheikh Waikela akaeleza kuwa yeye alikuwa bega kwa bega na Nyerere katika kuipigania uhuru wa Tanganyika na akimchukua Nyerere ndani ya gari yake Tabora na wakila chakula nyumbani kwake.

Waikela aliichekesha mahakama aliposema wakati ule alikuwa kijana ana fedha na akicheza tennis.

Akaeleza kuwa Gavana Edward Twinning aliingiza fitna nchini kuhusu Waislam kutaka kuwachonganisha na Wakristo katika suala la elimu ili avunje juhudi za TANU kudai uhuru.

Nyerere alimsihi Waikela kuwa katika hutuba zake ajitahidi sana kuliweka suala hilo vyema ili pasiingie mtafaruku na nchi ikawa kama India na Pakistani Waislam na Wahindu wakagawana nchi katika misingi ya dini.

Waikela akasema hilo walilifanyia kazi na hali ikabaki shwari hadi uhuru ukapatikana.

Matatizo yakaja baada ya uhuru kupatikana.

Waikela akaieleza Mahakama jinsi Sheikh Hassan bin Amir alivyomtahadharisha kuhusu njama zilizokuwa zinapikwa serikali dhidi ya EAMWS na akamweleza kuwa wanafiki ndiyo wanaotumiwa.

Sheikh Waikela aliwataja Mahakamani wanafiki hao kwa majina mmoja baada ya mwingine.

Akaeleza mkutano wa EAMWS katika Ukumbi wa Aga Khan Girls mwaka 1963 alipomsomea Nyerere risala ya Waislam kuhusu fitna iliyokuwa ikienezwa nchini dhidi ya Waislam na Uislam.

(Risala hii kwa sasa ni maarufu inajulikana kama ''Moto wa Waislam Ukiwaka.'')

Anasema hotuba hii ndiyo iliyosabaisha yeye kuwekwa kizuizini mwaka uliofuatia 1964 na alipotoka jela alipewa hati ya kifungo ambayo Sheikh Waikela aliieleza Mahakama kuwa ameitundika nyumbani kwake ukutani kama pambo.

Mahakama ilifahamishwa kuwa mmoja wa washitakiwa ni binti yake aitwae Dentation Waikela ambae alizaliwa baba yake ikiwa jela.

Sheikh Waikela akaeleza jinsi Nyerere alivyowawezesha kundi la Adam Nasib kwa fedha na ushirikiano wa serikali kupita majimboni kuwashawishi Waislam kujitoa EAMWS lakini hawakufanikiwa.

Katika majimbo 20 ni majimbo 8 tu ndiyo yaliyokubali kujitoa.

Hata hivyo serikali ilikatumia nguvu na kuitisha mkutano wa wanasiasa Waislam Iringa na Bakwata ikaanzishwa na serikali ikaweka askari wenye silaha katika ofisi zote za EAMWS na kuzifunga na makufuli na minyororo.

Binafsi Sheikh Waikela akaeleza Mahakama kuwa alihongwa shs: 40, 000 na Geoffrey Sawaya aliyekuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, hongo ambayo aliikataa.

Hao waliokubali hongo ile ndiyo walioshirikiana na serikali katika kuiweka BAKWATA madarakani.

Kuhusu kiwanja cha Markaz Chang'ombe anasema kile kiwanja ni mali ya EAMWS na madhumuni yake ilikuwa ni kujenga Chuo Kikuu.

Kwa hakika alisema mengi na mwisho alimuomba hakimu awape Waislam haki yao



No comments:

Post a Comment