Sunday, July 22, 2012

UAMSHO ZANZIBAR WAJIBU MAPIGO

IMEINGIZWA HUMU TAREHE 22/7/2012 Majibu ya Uamsho Zanzibar kuhusu kauli ya kwamba wamo serikalini. http://uamshozanzibar.files.wordpress.com/2012/06/zanzibar.jpg? Jana tulisikia kauli zenu na mukasema Uamsho wapo Serikali. Sisi tunayakubali maneno yenu na tunakiri kuwa ni kweli Uamsho wapo Serikalini. Ila nyinyi mumeshindwa kuwataja kwa majina sisi tutawataja kwa majina na vyeo vyao. Muamsho wa kwanza ni Rais Jakaya Kikwete. Yeye ametuamsha kwa kutwambia wazi Wazanzibari kuwa Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba haitoratibu Muungano. Hivyo ametuamsha na kutuwekea bayana Wazanzibari kuwa Tume hiyo haituhusu, sisi Wazanzibar kinachotuhusu kwenye Katiba ni Muungano. Katuamsha kuwa Tume hii ya Katiba si ya Muungano. Kikwete huyo huyo ametwambia kuwa Muungano ushavunjwa na CCM NEC, na alisema NEC imeshaamuwa kuwa Rais wa Zanzibar asiwe Makamu wa Rais wa Muungano. Hivyo ametuamsha kuwa NEC imeenda kivyume na Hati ya Muungano na kwenda kivyume na makubaliano ni kuyavunja makubaliano, hivyo NEC imeuvunja Muungano. Muamsho mkubwa zaidi ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda. Yeye alituamsha pakubwa tena akatutowa kwenye usingizi mzito pale alipotwambia kuwa Zanzibar si Nchi. Hata alipoambiwa ni nchi amekosea, akasema: “Sijakosea wala sijalewa. Zanzibar si nchi.” Kwa hakika, Pinda ametuamsha pakubwa. Muamsho mwengine ni Mwalimu Julius Nyerere alipotwambia amechoka na sisi Wazanzibari; na hapa namnukuu: “Tumechoshwa na Wazanzibar i na Uislaam.” Kama si Muamsho, huyu ni nani? Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Marehemu Mzee wetu Abeid Amani Karume, alituachia uswiya kwamba “Muungano ni kama koti, likitubana tutalivuwa!” Naye pia ni Muamsho. Muamsho mwengine ni Mansour Yussuf Himid. Naye katuamsha si haba pale aliposema ndani ya Baraza la Wawakilishi kuwa serikali moja hataki kuisikia, mbili ni butu, anataka serikali tatu au vyenginevyo. Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita, Shujaa Amani Karume ndiye aliyezidi sio tu kutuamsha, bali pia akatuletea Umoja wa Kitaifa na Mabadiliko ya 10 ya Katiba ya mwaka 2010 tena akaifanya iwe shoka la kuvunja Muungano. Isomeni vizuri Katiba ya Zanzibar na hapo mutajuwa kuwa Karume ni Muamsho au si Muamsho. Kwa hiyo, Stephen Wassira na UVCCM hamjakosea kusema Muamsho wapo Serikalini. Ni kweli. Tena wapo serikali ya Chama chenu. Wala msimtafute mchawi. Wachawi wenyewe. ---- http://uamshozanzibar.wordpress.com/2012/06/06/ni-kweli-uamsho-wamo-serikalini-jibu-la-vjana-wa-uamsho-kwa-wassira-na-uvccm/

No comments:

Post a Comment