Sunday, July 22, 2012

SERIKALI YAPIGA "STOP" UJENZI WA SEKONDARI ZA KATA !!!

Viwango duni vya elimu: Serikali kusitisha ujenzi wa Shule za Sekondari za Kata: NYAMBURETI SHULE YA SEKONDARI HAIKO PEKE YAKE. ZIKO ZA MATOKEO MABAYA KIBAAAAOOO! 17/07/2012 Serikali imesitisha ujenzi wa shule za sekondari za kata, kutokana na kutoridhishwa na kiwango cha elimu kinachotolewa katika shule hizo. Tamko hilo lilitolewa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, katika mkutano wa Taasisi ya Hassan Majaar Trust, iliyokuwa ikikabidhiwa Sh. milioni 26 zilizotokana na michango ya watumiaji wa simu za mikononi, Dar es Salaam jana. Dk. Kawambwa alisema Serikali imesitisha mpango huo ili iweze kupata nafasi ya kurekebisha upungufu uliopo katika shule za sekondari za kata zilizopo. Dk. Kawambwa alitaja upungufu huo kuwa ni pamoja na kuziwekea shule hizo maabara, madawati ya kutosha, walimu mahiri na kuboresha mazingira ya kazi, zikiwamo nyumba za walimu. “Tanzania bado haijafikia kiwango cha utoaji elimu bora katika shule zetu tulizozijenga kila kata, kutokana na changamoto nyingi zinazotukabili sasa. “Tayari Serikali ya awamu ya nne imeliona tatizo hili na imeanza mikakati ya kukabiliana nazo kuanzia sasa katika bajeti ya mwaka 2012/2013 na hata utawala ujao. “Tunakiri walimu wanafanya kazi katika mazingira magumu ambayo yanawafanya kushindwa kutoa elimu kama inavyostahili na ndiyo maana tumeamua kushughulikia matatizo yao, pia katika kupata walimu mahiri tumeongeza usajili katika vyuo vyetu wanafunzi walio na uwezo mzuri. “Tunaomba taasisi, mashirika na wadau wengine kufanya mawasiliano ya karibu na Serikali ili kuendelea kuchangia katika sekta ya elimu na ndiyo ya sera ya Serikali. “Hizi Sh milioni 26 zilizotolewa leo zitakwenda kutengeneza madawati 748 kwa ajili ya shule za Wilaya ya Makete na Njombe na zitawaondoa wanafunzi 2,255 wanaokaa sakafuni na kukalia madawati na isitoshe shule zetu bado zipo nchini ya halmashauri ili kurahisisha uendeshaji,” alisema. Hata hivyo, alisema katika bajeti yake ya mwaka 2012/2013, imejikita katika kufanya uboreshaji wa shule zote nchini, kufanya ukaguzi na kuboresha mazingira ya walimu. Source: http://www.wavuti.com/4/post/2012/07/viwango-duni-vya-elimu-serikali-kusitisha-ujenzi-wa-shule-za-sekondari-za-kata.html?utm_source=feedburner&utm_medium=email&utm_campaign=Feed%3A+wavuti+%28Wavuti+%29#ixzz20zWyUdMK

No comments:

Post a Comment