Sunday, November 1, 2009

UCHAGUZI TANZANIA UNAVYOJENGEWA MAZINGIRA YA KUFINYANGA DEMOKRASIA TANZANIA

Na Abdallah Bawazir

1st November 2009

http://www.ippmedia.com/images/frontend/headline_bullet.jpg Yahusu Mabalozi wanaoingilia mambo ya nchi

http://www.ippmedia.com/media/picture/large/Memb.jpg

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Vyama vya upinzani vimelaani kauli iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kuwaonya mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini kuwa wanaweza kutimuliwa endapo wataingilia mambo ya ndani ya nchi.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya viongozi wa vyama hivyo, wametahadharisha kuwa endapo onyo hilo la serikali litatekelezwa, Tanzania inaweza kuingia katika orodha ya nchi zenye mgogoro kidiplomasia na nchi fadhili na pia inaweza kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na watakaoathirika ni wananchi wa kawaida kama vile ilivyo Zimbabwe.

Viongozi hao wa vyama vya upinzani wametoa tahadhari hiyo, ikiwa ni siku chache tu, baada ya Membe kuonya kuwa balozi yeyote anayeiwakilisha nchi yake nchini akibainika kushirikiana na vyama vya upinzani kutaka kuking'oa madarakani chama tawala atafukuzwa nchini.

Akizungumzia onyo hilo la serikali kwa mabalozi, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, jana alisema kuwa kauli hiyo ya Membe si ya kiungwana kwa mabalozi na inafaa kulaaniwa na wana-demokrasia wote.

Alisema kuwa mabalozi wapo nchini si tu kwa ajili ya ushirikiano wa kiserikali kati ya nchi zao na Tanzania, bali pia kuangalia masuala mbalimbali kama vile demokrasia, haki za binadamu na utawala bora, na kwamba mambo hayo yanapokiukwa wanaweza kukemea na kwamba jambo hilo si kuingilia mambo ya ndani ya nchi.

Alisema kuwa nchi wafadhili zinachangia zaidi ya asilimia 40 ya bajeti ya serikali, hivyo hawawezi kukaa kimya kuona baadhi ya mambo kama vile ukiukwaji wa demokrasia na haki za binadamu yakitokea.

"Mabalozi wanajua mipaka ya kazi zao hawaingilii mambo hivyo ni mpaka pale wanapoona kuna tatizo, nchi zao zinachangia zaidi ya asilimia 40 ya bajeti ya serikali, hivyo hawawezi kukaa kimya wanapoona kuna ukiukwaji wa demokrasia na uvunjaji wa haki za binadamu", alisema.

Mwenyekiti huyo wa NCCR-Mageuzi, alidai kuwa uzoefu umeonyesha kuwa vyama tawala barani Afrika mara nyingi ndiyo vimekuwa chanzo cha vurugu na machafuko pale vinapominya demokrsia, kukiuka haki za binadamu na kuvuruga chaguzi na kwamba vinapobanwa na wafadhili hapo ndipo vinapowaona wabaya. Aliitahadharisha serikali kutowabana mabalozi pale wanapoingilia kati mambo ambayo yanaonekana wazi kukiuka misingi ya demokrasia na haki za binadamu, kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kuisababishia nchi matatizo makubwa kama vile kuwekewa vikwazo na watakaoathirika ni wananchi wa kawaida.

Alisema anashangaa kuona serikali ikianza kuvibana vyama vya upinzani wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu mwakani, kwa kuweka masharti mbalimbali kama vile kuzuia vyama visipate ufadhili wa nje wakati wa uchaguzi. "Mambo yote haya yanafanyika kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwakani, hili si jambo zuri" alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, alisema serikali haina mamlaka ya kuvizuia vyama vya upinzani kupata misaada kutoka nje ya nchi wala kuwazuia mabalozi kuingilia mambo yanayoweza kuivuruga nchi na kuleta machafuko.

"Kwa mujibu wa mkataba wa Vienna ambao Membe ndiyo ameutumia kuwaonya mabalozi kutoingilia mambo ya ndani ya nchi, serikali haiwezi kuwazuia mabalozi kuingilia mambo ya nchi kama kuna unyanyasaji, ukandamizaji wa demokrasia, ukiukwaji wa haki za binadamu na kuvururuga chaguzi" alisema. Kuhusu dhamira ya serikali kutaka kutunga sheria ya kuvizuia vyama vya siasa kupata misaada ya kifedha kutoka nje ya nchi wakati wa uchaguzi, Dk. Slaa, alisema kuwa sheria hiyo ina lengo la kuvikandamiza vyama vya upinzani.

"Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiyo kinachoongoza kwa kupata misaada mingi ya kifedha wakati wa uchaguzi kutoka kwa vyama marafiki nje ya nchi na ushahidi tunao hivyo sheria hii itakuwa ni ya kibaguzi" alisema.

Mkurugenzi wa Uenezi na Mahusiano na Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Salim Bimani, alisema kuwa, hatua ya serikali kutaka kuwabana mabalozi ni ya kidikteta na isiyofaa kutekelezwa katika nchi ya kidemorasia na kuendeshwa katika misingi ya haki.

"Kwanini wanataka kuwabana mabalozi, hawa jamaa hawaingilii mambo ovyo, wanajua wajibu wao, utakorofishana nao pale tu utakapokiuka haki za binadamu, kwenda kinyume cha misingi ya kidemokrasia na kuharibu uchaguzi, sasa serikali inaogopa nini? labda kama inajiandaa kufanyika kitu kibaya ambacho wanajua mabalozi wataingilia, kwa hiyo wanajihami kabisa", alisema.

Bimani, alisema anatafsiri onyo hilo la serikali kwa mabalozi kama njia ya kuvibana vyama vya upinzani visidai haki pale itakapokiukwa.

"CCM imeishiwa sasa inatumia nguvu kuvibana vyama vya upinzani ikihofu kuwa uchaguzi mkuu ujao unaweza kuwa mbaya kwa upande wake", alidai kiongozi huyo wa CUF.

Kama ilivyo kwa Mbatia, naye alitahadharisha kuwa endapo serikali itamtimua balozi yoyote kwa sababu tu amekemea uvunjaji wa haki za binadamu, uvurugaji wa uchaguzi, basi Tanzania inaweza kuingia katika mgogoro mkubwa wa kidiplomasia nchi fadhili ambalo zinaweza kusitisha misaada na watakaoathirika ni wananchi wa kawaida.

"Umeona Zimbabwe imewekewa vikwazo, wanaoteseka ni wananchi, kila kitu kimevurugika, hii yote ni kutokana na kiburi cha watawala wasiiongitia demokaria, haki za binadamu na kuvuruga uchaguzi, wametimua mabalozi wanaotaka kuona haki inatendeka sasa wanakiona" alisema.

Alitoa wito kwa wananchi, asasi zisizo za kiserikali na wapenda mageuzi wote, kukemea na kulaani onyo hilo la serikali kwa mabalozi, akisema kuwa endapo litatekelezwa linaweza kuleta madhara makubwa kwa nchi na wananchi wake.

Kauli hizo za wanasiasa wa vyama vya upinzani, zimekuja siku tatu tu, baada ya Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kuonya kuwa serikali ya Tanzania itamfukuza nchini Balozi au ofisa yeyote wa kibalozi atakayebainika kushirikiana na vyama vya upinzani kuking’oa chama tawala madarakani.

Serikali pia imesema, nchi zinazotoa misaada kwa Tanzania hazina mamlaka ya kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania.

Membe, alitoa msimamo bungeni ambapo alisema kwamba, mabalozi au ofisi za mabalozi wanaruhusiwa kushirikiana au kuvisaidia vyama vya siasa lakini si kwa lengo la kuking’oa chama tawala madarakani.

Alisema, Balozi au ofisa wa kibalozi atayeshirikiana na vyama vya siasa kuking’oa chama tawala madarakani watakuwa wanaingilia mambo ya ndani ya nchi mwenyeji, kuvunja itifaki na sheria za kimataifa.

Kwa mujibu wa Waziri Membe, kifungu cha tisa cha Mkataba wa Vienna kinairuhusu Serikali kuwafukuza nchini bila hata kutoa sababu yoyote ya kufanya hivyo.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment