Sunday, November 1, 2009

TANZANIA SI NCHI MASIKINI TENA? ha! ha! ha!

Subject: [tanzanet] Tanzania' si masikini' tena

Imeandikwa na Na Joseph Lugendo; Tarehe: 31st October 2009 Habari Leo


TANZANIA imeingia katika kundi la nchi zenye maendeleo ya watu ya kati kutoka katika kundi la nchi zenye maendeleo ya watu ya chini duniani, imebainishwa katika Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo ya Binadamu.

Lakini wakati Tanzania ikiingia katika kundi hilo la nchi zenye maendeleo ya watu ya chini duniani ugumu wa maisha unaotokana na kuongezeka kwa mfumuko wa bei na njaa inayotokana na ukame uliolikumba taifa vikiendelea kuwa changamoto kwa jamii ya sasa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa Octoba 13 mwaka huu, Tanzania ambayo ilikuwa nchi ya 159 katika kundi la nchi zenye maendeleo ya chini kati ya nchi 177 zilizoorodheshwa na ripoti hiyo ya mwaka 2007/2008, mwaka huu imepanda na kuwa nchi ya 151 na kuondoka katika kundi hilo la nchi zenye maendeleo ya chini ambalo nchi ya Niger imeshika mkia.

Ripoti hiyo imeonesha nchi kumi kwa kuwa na maendeleo ya juu zaidi duniani kwa mwaka huu zimeongozwa na Norway na kufuatiwa na Australia, Iceland, Canada, Ireland, Uholanzi, Sweden, Ufaransa, Uswisi na Japan.

Mwaka 2008 nchi kumi kwa kuwa na maendeleo ya juu zaidi duniani ziliongozwa na Iceland na kufuatiwa na Australia, Norway, Canada, Ireland, Uholanzi, Sweden, Japan, Luxembourg na Uswisi.
Hata hivyo imefafanuliwa katika ripoti hiyo kuwa katika nchi hizo zenye maendeleo ya binadamu ya juu, kuna tofauti ndogo sana kati ya nchi moja na nyingine.

Vigezo vilivyotumika kupandisha nchi kutoka nafasi moja kwenda nyingine kwa mujibu wa ripoti hiyo ni kuongezeka kwa umri wa kuishi mwanadamu kwa afya njema, fursa ya kupata elimu na kupata maisha bora.

Vipimo vya vigezo hivyo ni umri wa wastani wa kuishi wa mwanadamu katika nchi husika, wastani wa watu wazima wanaojua kuandika na kusoma pamoja na kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi wanaojiunga na darasa la kwanza na wastani wa kipato cha mtu mmoja mmoja kwa mwaka.

Katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Kenya imeongoza kwa kushika nafasi ya 147 duniani kwa mwaka huu kutoka nafasi ya 148 katika ripoti ya mwaka 2007/2008 na Tanzania kwa kushika nafasi hiyo ya 151 duniani, imekuwa ya pili katika nchi za EAC kutoka nafasi ya tatu mwaka 2007/2008.

Uganda imeshika nafasi ya tatu katika nchi wanachama wa EAC mwaka huu kwa kushika nafasi ya 157 duniani, hata hivyo imeporomoka nafasi tatu kwani mwaka 2007/2008 ilikuwa nafasi ya 154.

Rwanda na Burundi bado ziko katika kundi la nchi zenye maendeleo ya chini ambapo Rwanda ipo katika nafasi ya 167 mwaka huu na imeporomoka kutoka nafasi ya 161 mwaka 2007/2008 na Burundi imeshika nafasi ya 174 mwaka huu wakati katika ripoti ya 2007/2008, ilikuwa ya 167.

Tanzania imepiga hatua hiyo baada ya ripoti ya sasa kutumia takwimu za 2007 ambazo zimeonesha mafanikio katika sekta ya elimu na kuna uwezekano katika ripoti zijazo ikaendelea kupiga hatua kutokana na matarajio ya kuongezeka kwa umri wa wastani wa kuishi mwanadamu. Kwa sasa umri wa wastani wa kuishi mwanadamu Tanzania ni miaka 55.

Kwa mujibu wa Tarifa ya Takwimu za Tanzania (Tanzania in Figures) iliyotolewa mwaka huu na Ofisi ya Takwimu ya Taifa, umri wa wastani wa kuishi mwanadamu unatarajiwa kuongezeka kutokana matarajio ya kupungua vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano na wajawazito vinavyosababishwa na malaria baada ya kufanikiwa kwa usambazaji wa vyandarua vyenye dawa kwa bei nafuu.

Hata hivyo kupiga hatua kwa Tanzania katika ripoti zijazo kutategemea upatikanaji wa takwimu halisi za nchi nyingine kwani ripoti hizo za UN zimebainisha kuwa orodha ya maendeleo ya watu katika nchi husika hutokana na takwimu walizopata kutoka katika nchi hizo kwa wakati huo na kwamba zinaweza zisitoe picha ya hali halisi ilivyo.

Kutokana na hali hiyo, upatikanaji wa takwimu kwa wakati katika nchi husika, unaweza kubadilisha matokeo ya nafasi ya nchi husika katika orodha hiyo ya maendeleo ya watu kwa mujibu wa nchi wanazoishi, lakini mabadiliko hayo yataonekana katika ripoti zijazo.

Wakati ripoti ya UN ikiwa na matokeo hayo, Ripoti ya Bajeti ya Kaya iliyotolewa Januari mwaka huu imeonesha kuwa Watanzania walio wengi bado wanaishi maisha ya chini ambapo wengi nyumba zao zina sakafu ya udongo, kuta za udongo na miti na kupauliwa kwa miti nyasi na udongo.

Ripoti hiyo ya Bajeti ya Kila Kaya pia imeweka bayana kuwa katika mali ambazo Watanzania wanazimiliki kwa wingi ni vifaa vya jikoni, vitanda, viti na meza huku kompyuta ikiwa mali inayomilikiwa na Watanzania wachache zaidi ikifuatiwa na redio za kisasa (Complete music system), magari, simu za mezani (land line) na pikipiki.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya kaya, asilimia 67 ya nyumba za Watanzania zina sakafu za udongo. Hata hivyo nyumba za aina hiyo zimeelezewa kupungua kutoka mwaka 2001 ambapo asilimia 74 ya nyumba za Watanzania zilikuwa na sakafu za udongo.

Pia nyumba nyingi kwa kiwango cha asilimia 68.1 kuta zake zimejengwa kwa fito, udongo na mawe ingawa zimepungua kutoka zilizokuwepo mwaka 2001 ambapo asilimia 74 za nyumba za Watanzania zilikuwa na kuta hizo.

No comments:

Post a Comment