THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF - Chama Cha Wananchi)
MAONI YA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF- CHAMA CHA WANANCHI) KWA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA- 07 JANUARI, 2013
UTANGULIZI;
Kwa niaba ya The Civic United Fronf (CUF-Chama Cha wananchi), na kwa niaba
yangu binafsi napenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na
wajumbe wako kwa kutualika rasmi Chama Cha CUF mbele ya Tume yako kutusikiliza na
kupata maoni ya chama chetu juu ya mchakato huu muhimu kwa mustakbali mwema
wa Taifa letu la Tanzania pamoja na watu wake.
Aidha, tunampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuanzisha mchakato huu wa mapitio makubwa na kukusanya
maoni ya katiba ya nchi yetu ili ikidhi matakwa ya wakati wa sasa na
kutupeleka mbele zaidi kwa ustawi wa Taifa letu na watu wake. Madai haya ya
kuandaa mchakato wa kuwa na katiba mpya inayokidhi matakwa ya wakati
tulionao ni madai ya msingi ambayo chama chetu cha CUF kimekuwa
kikiyasisitiza tangu kurejeshwa tena kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi
vya siasa nchini mwaka 1992 na mara zote kuainisha suala hili katika
manifesto zake za uchaguzi.
Kutokana na muongozo wa Tume ya Mabadiliko ya katiba maoni yetu yamejikita
katika maeneo yafuatayo:
(i) Misingi na Maadili ya Kitaifa, Madaraka ya
(ii) Wananchi, Muundo wa Nchi na Taifa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
(iii) Haki za Binadamu na Wajibu wa Wananchi,
(iv) Ardhi, Maliasili na Mazingira
(v) Mihimili ya Nchi (Ardhi, Watu na Utawala),
(vi) Mihimili ya Utawala (Serikali,
(vii) Bunge na Mahakama),
(viii) Muundo na Mamlaka ya Serikali za Mitaa, na
(ix) Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Kwa muhtasari maudhui haya Chama Cha Wananchi CUF kinapendekeza yafuatayo
katika mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya Mwaka 1977;
1. Muundo wa serikali tatu za muungano; yaani serikali ya Zanzibar, serikali
ya Tanganyika na Serikali ya Mungano.
2. Uanzishwaji wa Tume huru za uchaguzi mapema iwezekanavyo. Kwa kuwa Tume
ya uchaguzi inapaswa kuanza kazi zake mapema ili kufanikisha uchaguzi wa
mwaka 2014/15, Tume haiwezi kusubiri mabadiliko ya katiba yakamilike ndio
ianze kazi zake kwa Muundo mpya utakaopendekezwa.
3. Katiba yenye misingi ya mfumo wa uwajibikaji kwa watendaji wote wa umma
na uainishwaji wa wazi wa Dira ya Taifa.
4. Katiba itakayotoa haki kwa wagombea binafsi kushiriki katika uchaguzi.
5. Katiba itakayotoa uhuru wa vyama vya siasa kuungana muda wowote
vitakapoona inafaa bila kupoteza usajili wa kawaida wa vyama hivyo.
6. Katiba itakayoweka muundo wa kuwa na Rais mtendaji "Executive President"
mwenye madaraka yanayopimika na kukubalika yasiyobana wala kuingilia au
kuondoa uhuru wa utendaji kazi wa mihimili mingine ya dola. Rais achaguliwe
kwa kupata asilimia 50+1 au zaidi ya kura zilizopigwa.
7. Katiba yenye kuweka mfumo sahihi wa kulinda rasilimali za Taifa na
kuhakikisha zinawanufaisha Watanzania wote kwa haki na usawa.
8. Katiba itakayompa kila Mtanzania kwa nafasi yake kushiriki katika
maendeleo ya nchi yake kwa kuwa na muundo wa serikali itakayoshirikisha
kila Mtanzania mwenye uzalendo wa kweli na uwezo wa kutoa mchango wake kwa ajili
ya maendeleo na ustawi wa taifa.
9. Katiba itakayoweka muundo wa uwakilishi wa uwiano (propotional
representation) ili kila kura itakayopigwa kuwa na thamani tofauti na
utaratibu wa sasa wa mshindi kuchukua vyote (winner takes all) hata kama ameshinda kwa kura moja.
10. Katiba itakayo hakikisha uwepo wa mgawanyo wa madaraka kati ya serikali
kuu na serikali za mitaa kwa kuondoa mfumo wa kuziburuza serikali hizo
zilizokaribu na wananchi. Wilaya zisianzishwe kiholela. Vigezo vya
halmashauri ya wilaya, miji, manispaa na majiji vitawekwa na sheria.
Utawala wa mikoa uondolewe.
11. Katiba itakayoweka msingi wa kuzuia ufisadi mkubwa wa rasilimali za
nchi hasa kwa njia ya uingiaji wa mikataba, Bunge likiwa ni chombo cha
uwakilishi wa wananchi lazima lishirikishwe.
12. Katiba itakayoweka Muundo wa Tume huru za Taifa za uchaguzi tangu ngazi
ya uteuzi wake kuanzia ngazi ya Taifa hadi ngazi ya chini. Katiba
itakayoto fursa matokeo ya uchaguzi kwa ngazi zote kuhojiwa mahakamani ikiwemo
matoke ya uchaguzi wa Rais.
13. Katiba itakayopambanua mgawanyo wa madaraka na mamlaka ya mihimili yote
mikuu katika nchi kwa maana ya Bunge, Serikali na Mahakama.
14. Katiba itakayoeleza wazi kuhusu haki na wajibu wa dola kuhakikisha
elimu ya watoto wetu, matumizi ya rasilimali za taifa, huduma za msingi za afya,
ulinzi wa nchi yetu na sera za ardhi na kilimo zinasimamiwa na kutekelezwa
kwa manufaa ya wananchi wote. Katiba ndiyo yenye nafasi ya kulinda haki hizi
za mwananchi na si huruma ya mtawala atakaye kuwepo kwa wakati huo au chama
cha siasa. Sera za kitaifa lazima zifuate na kuheshimu haki zilizoainishwa
ndani ya katiba.
15. Kuhakikisha kwamba wananchi wana madaraka ya kujiamulia wenyewe masuala
ya maendeleo yao kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.;
16. Katiba yenye kulinda haki za binaadamu, na kupinga aina zote za ubadhilifu, ukandamizaji, ubaguzi wa aina yeyote iwe wa kidini, kikabila, kijinsia au kikanda.
17. Katiba yenye kuweka misingi endelevu ya kulinda amani ya nchi yetu.
18. Masuala ya Ardhi yawe na sura kamili katika katiba mpya. Ardhi ni mali
ya Watanzania wote. Mtanzania peke yake ndiye anayeweza kumiliki ardhi moja
kwa moja.
19. Katiba inayohakikisha kuwa haki za msingi za makundi maalum, wanawake,
watoto, wazee wasiojiweza na walemavu zinalindwa kwa kuanishwa ndani ya
katiba.
Chama cha CUF kipo tayari kutoa ushirikiano unaostahiki kwa Tume katika
kipindi chote cha mchakato huu pamoja na kushirikiana na Watanzania wote
bila kujali itikadi za kisiasa na tofauti nyinginezo, kuhakikisha kuwa kwa
pamoja nchi yetu inakuwa na katiba bora yenye kukidhi haja na matakwa ya
hali ya kisiasa, kiuchumi na ustawi mwema wa jamii ya Watanzania.
Ni matarajio ya Chama Cha Wananchi CUF kuwa maoni haya yatazingatiwa na
kuingizwa katika rasimu ya mabadiliko ya katiba kwa mjadala na hatimaye
kufanyiwa maamuzi yanayofaa kwa mustakbali mwema wa Taifa letu la Tanzania.
Mungu Ibariki Tanzania na watu wake.
HAKI SAWA KWA WOTE
Prof Ibrahim Haruna Lipumba,
Mwenyekiti wa CUF Taifa
Contact;
P.O.Box 10979
Dar es salaam, Tanzania.
lipumba@yahoo.com