TATHMINI YA MKUTANO MKUU WA CCM
Karume “mpuuzi”, lakini ukweli wake mchungu
MAKALA
hii itahitimisha tathmini yangu kuhusu Mkutano Mkuu wa 8 wa CCM
uliofanyika Dodoma tangu Novemba 11 hadi Novemba 14 mwaka huu.
Kwa
kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) ni chama dola, vimbwanga vyake huwa
vinachanganya watu na kuamini kuwa kila baada ya Mkutano Mkuu, CCM huwa
inazaliwa upya.
Imani
hii imejengeka kutokana na ukweli kuwa, kabla ya Mkutano Mkuu, huwa
kuna dalili za migawanyiko na mipango kadhaa ya makundi kutaka agenda
zao zishinde.
Kutokana
na udhibiti wa vyombo vya dola pamoja na ushabiki uliopitiliza, mipango
hiyo huwa inakwama na kuwafanya watu wengi kuamini kuwa CCM ina
wenyewe, na wenyewe hao huwa wanaifanya izaliwe upya kila baada ya
Mkutano Mkuu!
Historia
ya dhana hii ni ndefu, na wahanga (victims) wa mkakati huu kwa miaka ya
karibuni ni Salmin Amour (Komandoo), Mzee John Malecela, Dk. Gharib
Bilal, Samuel Sitta na sasa Edward Lowassa.
Kwa
miaka ya nyuma wanakumbukwa Mzee Aboud Jumbe na Sharrif Hamad. Kwa
sababu zilizo wazi, mkakati huu wa kuipa uhai mpya CCM huwa unawaathiri
sana Wazanzibari kuliko Watanganyika.
Rais Karume na “upuuzi” wake
Kama Makamu Mwenyekiti anayemaliza muda wake, rais
mstaafu Amani Karume alikaribishwa kutoa nasaha zake siku ya kufunga
mkutano. Alitoa hotuba, ambayo hivi sasa inaitwa ya kipuuzi huko
Magogoni na mtaa wa Lumumba.
Hakuna
aliyetarajia kuwa Karume angesema maneno aliyoyasema siku hiyo kiasi
cha Mwenyekiti Jakaya Kikwete kukiri kuwa “hajawahi kumwona amefurahi
kiasi hicho” kama alivyomwona siku hiyo.
Mara
kadhaa hotuba yake ilikatishwa na watu waliomzomea na kumtaka amalize
na kukaa. Hii ikakumbusha enzi za
uenyekiti wa Benjamin Mkapa wakati wanamtandao wa Kikwete walipokuwa
wakimzomea kila mtu aliyetaka kuhoji matumizi ya rushwa katika mkutano
huo.
Mzee Joseph Butiku anaikumbuka hii na aliiandikia barua
rasmi kwa Mwenyekiti Mkapa. Hii itukumbushe kuwa zomea zomea haikuanza
na CHADEMA katika mikutano.
Alipozomewa sana, Rais Karume akawafananisha wazomeaji na
vinywa vya samaki! Wapo waliodai, Rais Karume alikuwa kalewa sana
konyagi siku hiyo. Awe alilewa au hakulewa; ni mpuuzi au si mpuuzi;
kwangu mimi si habari. Habari muhimu ni yale aliyoyasema kwa dakika
alizopewa.
Karume
alizungumzia kadi yake ya ASP (Afro Shiraz Party); akaelezea
madhumuni ya ASP; akamwuliza Dk. Shein ikiwa yeye anayo kadi yake ya
ASP. Moja ya madhumuni ya ASP akakumbusha kuwa ni kulinda uhuru wa
Zanzibar na watu wake. Ndipo akahoji wale wanaowazuia wenzao wasitoe
maoni yao kuhusu Muungano.
Akamkumbusha
Rais Kikwete kuwa alitoa ruhusa kila mtu aseme anachotaka wakati wa
mchakato wa kutoa maoni ya katiba mpya. Akahoji iweje sasa wengine
wanakamatwa kwa kutoa maoni yao. Karume akakumbusha jinsi CCM
ilivyopoteza baadhi ya majimbo kwa sababu ya kupuuzia maoni ya wananchi.
Akakumbusha suala la zamu kati ya mbunge na mwakilishi katika jimbo
fulani. Wazomeaji hawakutaka kusikia haya wakamwimbia taarabu ya “uamsho
uamsho”.
Niseme
wazi hata kama nilichoka nikakaa nje ya ukumbi wakati anaongea, Karume
alisema mambo ya maana kuliko hotuba za masaa zilizotolewa na
waheshimiwa wengine. Kwa muda mfupi, Karume aliuzodoa udikteta
unaoabudiwa ndani ya CCM; alibainisha hatari zinazoukabili Muungano;
alikumbusha habari za zamu za kuongoza nchi hii iliyotokana na nchi
mbili; na zaidi sana alisema kutoka moyoni kuwa ASP haijafa kwa sababu
waliokuwa wanachama wake wangali bado hai. CCM tumeze au tuteme, huo
ndio ukweli kutoka kwa Karume, ambao sasa unaitwa ni upuuzi na akina
Nape Nnauye.
Kulialia na kulalama kulizidi mno
Kwa siku tatu, Watanzania walishuhudia wajumbe zaidi ya
2000 wakilialia na kulalamika ndani ya ukumbi. Mwenyekiti alizindua
uliaji huo na kupokewa na wajumbe kwenye vikao visivyo
rasmi katika nyumba za kulala wageni na kwenye magari. Kivuli cha Chama
cha Denokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiliwatesa sana wajumbe na
kuwafanya viongozi kupoteza mwelekeo na kuanza kutukana ovyo ovyo.
Haikutarajiwa kuwa Mwenyekiti naye angeingia katika mtego
huo, pale alipojikuta anawatukana wapinzani na hasa CHADEMA kwa kuwaita
“watu wazima ovyo”, au pale ndani ya NEC alipojikuta anatumia muda
mwingi kumpamba Nape Nnauye kwa kuwa anajua kutukanana na CHADEMA. Hata
pale alipokumbushwa na rafiki yake kuwa kuitukana CHADEMA si lazima
kuijenge CCM, yeye aliishia kusema “wamezidi acha Nape awashughulikie”.
Kazi inayomshinda yeye, anaona ni bora aifanye Nape. Kama Mzee Rashidi
Kawawa alivyokuwa kwa Mwalimu, Nape ndivyo kwa Kikwete!
Mzee
mkorofi kutoka Nyanda za Kusini alihoji, inakuwaje CHADEMA iwe tishio
kwa CCM kuliko ufisadi na rushwa ulivyo tishio? CHADEMA inakuwaje tishio
kuliko “unduguneizesheni” unaotafutiwa nafasi ya kutambuliwa kwenye
katiba ya chama chetu?
Akasema,
inakuwaje washauri wakuu wa Mwenyekiti wa chama chetu kuhusu masuala ya
chama, si vikao bali ni wanausalama waliojaa fitina? Huyu naye alikuwa
analalama sawa tu na wengi waliokuwa wanalalamika kwa siku tatu za
mkutano.
Membe: Alimzamisha Mangula; Amemuibua tena.
Nafasi ya Bernard Membe kwa siasa za taifa hili kwa siku
za usoni
ilikuwa katika mtihani mgumu sana. Kambi ya rafiki yake wa zamani
Edward Lowassa ilipania kumzamisha lakini akaokolewa na Kikwete na
familia yake.
Kikwete alimsaidia kwa kubadili ratiba za upigaji kura,
wakati familia yake (mkewe na mtoto wake) walihaha kila kona kumtafutia
kura Bernard Membe. Taifa hili siku moja litadai kujua ukweli wa uhasama
na urafiki wa watu hawa watatu – Membe, Kikwete na Lowassa. Jina
Kikwete limekaa katikati kwa makusudi. Yeye ni ufunguo wa kitendawili
hiki. Hili tuliache kwa sasa.
Mzee
Philip Mangula, akaibuka ghafla kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara. Ni
huyu huyu ambaye kundi la mtandao lililomwingiza Ikulu Kikwete lilidai
alilitesa sana wakati wa kampeini na kuamua kumtosa mara baada ya
Kikwete
kuapishwa.
Yasemekana,
Benard Membe, kachero mzoefu na kiini cha mikakati ya wana mtandao
asilia, alimwambia Kikwete kuwa Mangula aliwapa taabu sana hivyo
aondolewe kwenye nafasi ya ukatibu mkuu wa chama. Haikuishia hapo, Mzee
Mangula alipojaribu kuibukia Iringa kama Mwenyekiti wa Mkoa
alishughulikiwa vikali na kuangushwa na mtu asiyefanana na CCM kwa
vigezo vyote.
Mzee
Mangula alikiri baadaye kuwa ndani ya CCM uongozi uko mnadani na wapiga
kura hawataki tena vipeperushi vya wagombea, bali wanataka
“vipeperushwa”. Mzee Mangula, kila anapokumbushwa harakati za wana
mtandao, huwa anatania kuwa yeye aliponzwa na “faili maalumu”.
Kuna
habari kuwa Mzee Mangula kaibuka kwa mkono wa Membe. Kwamba, vikao
kadhaa vilifanyika Makambako kati ya wawili hawa. Iwe kwa Membe kujituma
au kutumwa, ni kwamba walikutana na agenda ilikuwa ni uchaguzi katika
Mkutano Mkuu wa 8.
Aliombwa
radhi au hakuombwa, hilo sasa si habari. Habari ni kuwa, Mkutano Mkuu
umempitisha Mzee Mangula kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM lakini mshenga
mkuu alikuwa Membe. Kama ushenga huu ulikuwa ni kwa manufaa ya chama au
kwa manufaa ya mtandao wake anaouunda kwa ajili ya 2015, ni suala la
wakati.
Ikiwa
ni kweli, basi itakuwa vigumu kukemea mitandao ndani ya chama hiki
kikongwe. Kama mtandao wa Membe ni halali, wa Lowassa hauwezi kuwa
haramu. Kama Kikwete aliingia kwa mtandao, ni vigumu kuifikiria CCM na
urais bila mtandao. Na tumejifunza kwa uchungu kuwa mtandao hauishii
katika uchaguzi kwa sababu, baada ya mtu wao kuchaguliwa, kinachofuata
ni kufaidi jasho na matunda ya kazi.
Kwa walioshindwa, kuna kazi ya kutathmini ni wapi
wamekwama na kuazimia aluta continua. Ni ndoto kuambiana kuvunja makundi
wakati anayeshinda na kuingia Ikulu anaendelea na kundi lake.
Jambo moja tu Mzee Mangula alizingatie. Membe anayedaiwa
kumzamisha baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 mbele ya Kikwete, hawezi
kugeuka leo na kumtetea kuwa ni mtu mzuri anayekifaa chama. Kwa nini
hakufaa mwaka 2005 chini ya Mwenyekiti huyuhuyu? Membe ni yule yule,
Mwenyekiti ni yule yule, chama ni kile kile na Mangula ni yule yule! Ni
kitu gani kimebadilika kumfanya Mangula asiyefaa mwaka
2005, afae mwaka 2012?
Kinachoonekana
lakini hakizumguziwi waziwazi, ni ukweli kuwa Kikwete na Membe
wanamwona swahiba/hasimu wao Lowassa kuwa sasa ni zaidi ya mgombea urais
wa CCM 2015. Kwao, Lowassa amegeuka kuwa chama; ameiteka CCM mbele ya
macho yao na wanadhani Mangula atawasaidia kuiokomboa CCM iliyo mateka
mikononi mwa Lowassa. Kikwete na Membe hawajiulizi ni kitu gani
kimemjenga Lowassa na kumfanya kuiteka CCM.
Kitendo
cha kumkimbilia aliyekuwa “adui” yao na chama chao kuwa aje kuwasaidia
kukijenga chama walichokibomoa kwa mikono yao, hakieleweki. Wengi
tulidhani, Mkutano Mkuu ungepata nafasi ya kutathmini hali hii, badala
yake tukaambulia kulialia na vijembe visivyo na mpangilio. Tusubiri
Mkutano Mkuu mwingine maalumu au ule wa
2017.
Chanzo: Gaezeti la RaiaMwema
No comments:
Post a Comment