Saturday, December 15, 2012

MAONI KWA TUME YA KATIBA YA DAR ES SALAAM

Imetundikwa hapa leo hii 16/12/2012.

Maoni  kwa Tume ya Katiba Mpya  Dar es Saaam, Jumatano,  tarehe 12 Disemba, 2012.  

Tume hivi sasa iko mkoa wa Dar es Salaam. Leo niliikuta maeneo ya Magomeni karibu na ofisi za Manispaa kiongozi wa msafara akiwa Dr. Salim A. Salim.

Baadhi ya maoni waliyotoa wananchi ni kama ifuatavyo:

1. Mgombea binafsi awepo kwenye ngazi zote za uchaguzi.
2. Muungano uwe wa serikali tatu: Tanganyika, Zanzibar na Muungano.
3. Viongozi wasomeshe watoto wao shule na vyuo vya serikali, na watibiwe hospitali za serikali.
4. Rasilimali zinufaishe wananchi. Mmoja alitoa mfano kuwa dhahabu ikishachimbwa 70% iwe ni mali ya Tanzania, mwekezaji aachiwe 30% tu.
5. Upatikanaji wa taarifa katika vyombo mbali mbali vya serikali uboreshwe.
6. Kiswahili kiwe lugha rasmi ya kufundishia toka ngazi ya chekechea mpaka chuo kikuu. Na pia itumike makazini. (Ila mmoja yeye alisema kinyume, akapendekeza Kiingereza ndio iwe lugha kuu ya kufundishia)
7. Timu ya Taifa Stars ifutwe kwa sababu inapoteza hela bure hakuna cha maana inachofanya.
8. Mkono wa dola uingie kwenye sekta ya michezo. FIFA waache kutubabaisha kuwa mambo ya soka yasipelekwe mahakamani.
9. Kuwe na ukomo wa mtu kuwa mbunge mwisho miaka 10 au 15.
10. Serikali iwabane wazazi toka ngazi ya nyumba kumi kumi ili kuzuia watoto wa mitaani. Mtoa hoja alisema watoto wengi wako mitaani kutokana na ugomvi tu kati ya wazazi wao, lakini wazazi pamoja na ndugu zao unakuta wana uwezo kabisa wa kuwalea ila ndio hivyo tena hawaelewani. Alisema ikifanyika hivyo watabaki watoto wachache sana mitaani ambao kweli ni yatima na wanahitaji msaada.
11. Wala rushwa na mafisadi wanyongwe mpaka kufa (kama China)
12. Watanzania walioko nje ya nchi waruhusiwe kupiga kura kwenye uchaguzi wa raisi.
13. Umri wa kugombea uraisi upunguzwe toka miaka 40 mpaka 35 kwa kuwa asilimia kubwa ya wananchi ni vijana.

HOJA ZA WAISLAM. Eneo hili lina Waislam wengi kwa hiyo kulikuwa na mapendekezo mengi pia yenye mrengo wa Kiislam kama ifuatavyo:

1. Mahakama ya Kadhi iwepo, na itengenewe bajeti kwa pesa za walipa kodi kama vile serikali inavyotumia pesa za walipa kodi kumlipa balozi wa Vatican.
2. Kuwe na uwiano wa kidini kwenye ajira. Nusu kwa nusu. Kama kuna Wakristo 50 basi waajiriwe Waislam 50.
3. Mihadhara ya "Yesu si Mungu" iruhusiwe.
4. Ujenzi wa bucha za nguruwe kwenye makazi ya watu upigwe marufuku.
5. Ijumaa iwe siku ya mapumziko kama Jumamosi na Jumapili. Na Idi na Maulid zisheherekewe kwa siku mbili mfululizo kama Pasaka na Christmas.
6. Mavazi yasiyo na staha yapigwe marufuku. Na hijabu na kanzu ziruhusiwe kila mahali.
7. Iwe marufuku kwa watumishi wa umma kusikiliza nyimbo za injili ofisini.
8. Tanzania ijiunge na OIC (Organisation of the Islamic Conference)
9. Matangazo ya pombe yapigwe marufuku.

No comments:

Post a Comment