9/1/2011 Waziri Mambo ya Ndani adanganywa Magereza (Habari Leo) tanzania
MRADI wa OMIS uliozinduliwa Desemba 17, mwaka jana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha katika Ofisi ya Makao Makuu ya Jeshi la Magereza umetajwa kuwa ulilenga kufunika utaratibu mbaya uliotumika katika utekelezaji wa mradi huo na kuisababishia hasara Serikali. Mradi wa OMIS (Offenders Management Information System), ulibuniwa na Jeshi la Magereza ukiwa na lengo la kuunganisha idara zote zinazohusika na masuala ya uhalifu ambazo ni Magereza, Polisi, Mahakama, Parole na Huduma za Jamii. Lengo la mradi huo ni kuboresha shughuli za wafungwa kwa kuzifanya idara husika ziweze kutekeleza shughuli zao kwa haraka na ufanisi kwa kutumia teknolojia ya kompyuta. Taarifa ya kurasa tisa iliyowasilishwa kwa Waziri Nahodha ambayo gazeti hili limefanikiwa kuipata nakala yake inayoelezea uhalisia wa mradi huo imefafanua upungufu mkubwa wa kiutendaji, jambo ambalo waziri huyo hakuelezwa awali.
Ndani ya taarifa hiyo, ilielezwa kuwa ni aibu kwa Waziri kukaribishwa kuzindua mradi huo huku uongozi wa Magereza ukifahamu wazi kuwa utekelezaji wake ulikwenda kinyume na nyaraka ya zabuni ya mradi wa OMIS-Software kumbukumbu namba 12/2006/2007 iliyoandaliwa Julai 23, 2007. Waraka huo ambao imeelezwa kuwa maelekezo yake hayakufuatwa, uliandaliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ndio ulipaswa kutumika kumpata mzabuni aliyepaswa kusimika mfumo huo katika eneo la majaribio, upande wa Jeshi la Magereza, lakini hilo halikufanyika, kwa mujibu wa waraka huo. Kwa mfano, taarifa hiyo ilieleza, mradi huo ulikwenda kinyume na waraka wa zabuni hiyo Omis-Software, uliosimikwa hauna uwezo wa kupanuliwa punde utakapohitajika kutumika sehemu nyingine za utekelezaji wa mradi huo ili kupeana taarifa katika maeneo yote yenye mfumo huo katika uendeshaji wa shughuli za wafungwa.Pia ilielezwa kuwa utekelezaji wa mradi huo umekwenda kinyume na kifungu namba 5 cha zabuni hiyo ambacho kilikuwa kikifafanua utekelezaji kwenye mahitaji ya mradi husika (OMIS-Software user requirements), jambo ambalo limezua sintofahamu kuhusu utekelezaji na ukamilikaji wa mradi huo. Kutokana na sababu hiyo, ilielezwa kuwa uzinduzi wa mradi huo umemdhalilisha Waziri kwa kuwa walitumia ugeni wake katika wizara hiyo kubariki mradi uliokwenda kinyume na maelekezo ya wizara husika. “Uzinduzi wa OMIS uliofanyika Desemba 17 mwaka jana, ulifanyika wakati mradi wa OMIS-Software ukiwa na kasoro nyingi zinazoashiria ubadhirifu wa fedha za Serikali, kupitia udanganyifu unaotengeneza mazingira yatakayodumisha ubadhirifu wa fedha za Serikali,” taarifa hiyo ilieleza. Pia taarifa hiyo ilieleza kuwa vielelezo vya malipo katika mradi huo vinaonesha wazi kwamba Kampuni ya GIVA ambayo inadaiwa kupata zabuni ya mradi huo kinyume na utaratibu, imetumika kama daraja la kuchotea fedha kupitia mradi huo ambapo hadi Oktoba 5, mwaka jana, ilikuwa imelipwa jumla ya Sh 1,936,541,550. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, malipo ya hivi karibuni yalifanyika kwa awamu sita ambapo Aprili 4, kupitia vocha namba 995592 ililipwa Sh 410, 884, 850; Juni 25, kwa vocha namba 996861, ililipwa Sh 89,115,150; Juni 24, kwa vocha namba 696977 ililipwa Sh 46,994,154.50. Malipo mengine yalifanyika Juni 27 vocha namba 694001, Sh 453,005,845.50; Septemba 9 kupitia akaunti namba 021240777055 ililipwa Sh 153,287,550; na Oktoba 5 kupitia akaunti namba hiyo hiyo ililipwa Sh 183,254,000. Pia ilielezwa kuwa katika mazingira ya utatanishi, kampuni hiyo iliiuzia Magereza ‘seva’ sita zenye kasi ya 2.2Ghz kwa Sh milioni 410 kwa kutumia zabuni ambayo ‘ilipikwa’ kwani ilikiuka taratibu. Gazeti hili lilielezwa kuwa wakati Jeshi la Magereza likinunua vifaa hivyo, tayari lilikuwa na vingine vitano vyenye uwezo mkubwa zaidi, kwani vina kasi ya 3.4 Ghz, hivyo vifaa vilivyonunuliwa kutoka GIVA vimepitwa na wakati kwa kuwa havitakidhi mahitaji ya mradi huo. Uongozi wa kampuni hiyo ulikiri kuwa Kampuni ya GIVA ilihusika katika mradi huo, lakini ulikataa kutoa taarifa zaidi kuhusu madai yaliyoandikwa kwenye ripoti hiyo. Ilielezwa kuwa Waziri Nahodha alidanganywa waziwazi, kwani katika hotuba ya uzinduzi wa mradi huo katika eneo la majaribio, aliambiwa kuwa mradi huo umekamilika kwa dola milioni moja za Marekani wakati si kweli. Ilielezwa pia kuwa hiyo ilitokana na ukweli kwamba wakati kauli hiyo ikitolewa hakupewa mchanganuo wa matumizi ya fedha katika mradi huo ambao inaonesha wazi matumizi zaidi ya fedha. Pia ilielezwa kuwa software (data au programu ya kompyuta) za alama za vidole na vifaa vingine vinavyotumika katika mradi huo, mpaka sasa havijulikani kinyume na maagizo ya zabuni hiyo, hivyo kujitokeza walakini katika matumizi ya fedha za ziada zilizolipwa kwa kampuni hiyo. Gazeti hili liliwasiliana na Ofisi ya Waziri Nahodha ili kupata ufafanuzi wa jambo hilo, ambapo Katibu wake aliyejitambulisha kwa jina la Nelson alisema kuwa Waziri bado mgeni katika wizara hiyo anahitaji muda wa maandalizi kabla ya kutoa kauli kuhusu jambo hilo. “Nitawasiliana naye kuhusu jambo hilo, nadhani na wewe unajua kwamba Waziri ndio kwanza ameanza kazi hivyo si rahisi akajua kila kitu kinachoendelea katika kila idara, nitumie namba yako ya simu tukishauriana nitakupigia,” alisema Nelson. Lakini hata baada ya kupita wiki mbili sasa, hakuna majibu yaliyotolewa, ilhali watendaji wakuu ndani ya Jeshi hilo wakionekana kukwepa kulizungumzia hilo kwa kile wanachodai kubanwa na majukumu ya kikazi.
No comments:
Post a Comment