Thursday, January 13, 2011

MWAKYEMBE ASEMA DOWANS KAMPUNI HEWA HAISTAHILI KULIPWA CHOCHOTE

Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe
Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amevunja ukimya kuhusu sakata la kutaka kulipwa fidia ya mabilioni ya Shilingi kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans Tanzania Limited, kwa kueleza kwamba itakuwa jambo la ajabu kama serikali itakubali kulipa fedha hizo, kwani kampuni hiyo awali ilibainika kuwa ya kitapeli, lakini sasa inaonekana kuwa ni halali.
“Tulishasema kuwa Richmond ni kampuni hewa ambapo Dowans wamerithi mkataba hewa, hivyo inakuwaje walipwe tena mabilioni ya fedha, tunasubiri kuona msingi uliotumika tapeli kulipwa fidia kwa kazi ya utapeli, nitaangalia amelipwa kwa sheria ipi,” alisema Dk. Mwakyembe jijini Dar es Salaam jana.
Dk. Mwakyembe ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza mchakato wa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura kwa Kampuni ya Richmond Development LLC, alitoa tamko hilo katika mahojiano maalum na NIPASHE ofisini kwake, baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu tangu itolewe hukumu hiyo ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC) na kulitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuamuriwa kuilipa Dowans Sh. bilioni 94..Alisema suala la kutaka kuilipa Dowans lina sura mbili, sura ya kisiasa na sura ya kitaalamu.
Alisema katika sura ya kitaalamu yeye kama mwanasheria ambaye amekuwa katika fani hiyo kwa zaidi ya miaka 20, anasubiri kwanza hukumu hiyo isajiliwe na itatoa fursa kila Mtanzania kuyasoma na kuyaelewa yaliyomo ndani.
Dk. Mwakyembe alisema kama mwanasheria, anatilia mashaka na kuzua maswali mengi hukumu hiyo kwa sababu haiwezekani kampuni iliyoonekana mwanzo kuwa ni ya kitapeli leo inaonekana halali.
“Mimi ni mwalimu wa sheria wa siku nyingi na nimekuwa kwenye fani hii kwa zaidi ya miaka 20, kwa hiyo nasubiri kwa hamu usajili wa hukumu hiyo ya ICC ili nione ni sheria ipi iliyotumiwa na wanasheria, tapeli kulipwa fidia kwa kazi yake ya utapeli,” alisema Waziri Mwakyembe.
Dk. Mwakyembe alisema baada ya kusajiliwa kwa hukumu hiyo, pia ana dukuduku la kutaka kujua ni vipi Tanzania imepoteza kesi rahisi kama hiyo ambayo hata mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Sheria angeweza kuiendesha na kushinda.
“Nina dukuduku kutaka kujua ni vipi tumepoteza kesi rahisi kama hii ambayo hata mwanafunzi wangu wa mwaka wa kwanza wa digrii ya sheria nina uhakika angeshinda kwa sababu Bunge lilishatafuna kila kitu,” alisema.
Alisema kama serikali itaingia mkenge kulipa mabilioni hayo ya fedha, ipo katika hatari ya kuingizwa katika kesi iliyofunguliwa Marekani ambayo Dowans wameshitakiana na Richmond kutokana na kung’ang’ania mtambo mmojawapo wa kuzalisha umeme.
Alisema kesi hiyo kati ya Dowans na Richmond ipo katika Mahakama ya Wilaya ya Kusini (The United State District Court for the Southern District of Texas Houstorn Division) ambapo zipo tetesi kuwa Tanzania itakapolipa fedha hizo itajumuishwa kwenye kesi hiyo ya kugombaniana mitambo.
“Dowans na Richmond wameshitakiana Marekani kwa kung’ang’ania mtambo GE TM2005 S/N 481-364,7LM 2005-PE-MDW GE UNIT ID.W/O 601178, sasa zipo tetesi kwamba Tanzania inasubiliwa kuingizwa katika kesi hiyo itakapokubali kulipa fedha hizo,” alisema.
Alisema hatua ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kueleza kwamba serikali imeamua kuilipa fedha Dowans, ameufanya haraka kwa sababu angesubiri kwanza hukumu hiyo isajiliwe.
Aliongeza kuwa kama serikali itakubali kulipa fidia hizo, kutakuwa kuna utata kwa sababu majina ya waliotajwa kuwa ni wamiliki wa Dowans Tanzania Limited, lakini wale wa Dowans Holding SA (Costa Rica) hawajulikani na wala hawana anuani ya posta wala simu nchini.
Alisema anayetajwa pekee kuwa mmiliki wa Dowans Holding SA ni Bernal Zamora Arase ambaye hata hivyo, ana makampuni 100 yanayoishia na SA.
“Huyu Bernal Zamora Arase anayetajwa kuwa mmiliki wa Dowans Holding SA hana simu, ofisi wala anuani ya posta, nyumba ya kuishi, gari wala pikipiki hapa nchini,” alisema Dk. Mwakyembe.
Aliongeza kuwa Watanzania wengi bado wanafahamu kuwa chini ya makubaliano, mali zote za Richmond bado hazijahamishiwa Dowans na hivyo wanalipwa pesa kinyemela na wameshitakiana Marekani.
Naibu Waziri huyo akizungumzia katika sura ya kisiasa kuhusiana na sakata la Dowans, alisema wasemaji wakuu ni Spika wa Bunge, ambaye Bunge lake lilipitisha maazimio 23 mwaka 2008 ambapo kati ya maazimio hayo ambayo yalihukumu Richmond kuwa ni kampuni hewa.
Alisema Bunge hilo pia lilienda mbele zaidi kwa kuagiza kutaka ifutwe kwenye orodha ya makampuni halali Tanzania ambapo Oktoba 2008 Richmond ilifutwa kama kampuni isiyo halali.
“Kimsingi, mwenye mamlaka ya kuelezea hatma ya maazimio 23 yaliyotolewa na Bunge ni Spika wa Bunge la Tanzania, kwa sababu hukumu ya ICC imegusa baadhi ya maadhimisho,” alisema.
Dk. Mwakyembe alisema pia Waziri Mkuu ambaye kikatiba ni msimamizi mkuu wa shughuli za Bunge na serikali hivyo ana imani baada ya kupokea ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali atakuwa na kauli yake ya mwisho.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment