Thursday, September 30, 2010

MAONI JUU YA UCHAGUZI MKUU TANZANIA 31/10/2010

IMECHANGIWA NA JAMII FORUMS

Hivi kweli hizi ni kampeni, au ni vita ya msalaba?

Mwaka 2005 maaskofu walijifunga vibwebwe na kufanya kile ambacho kisingetarajiwa kifanywe na viongozi wa dini. Bila kujali kuwa walichokuwa wanakifanya ni kinyume kabisa na maadili ya 'FAIR PLAY', yaani kutocheza rafu ya makusudi, walijitoa hadharani na kudai kuwa Taifa lilikuwa linahitaji kiongozi mwadilifu na mcha Mungu; na huyo hakuwa mwingine bali Jakaya Kikwete kwa kuwa huyo ndiye aliyekuwa 'CHAGUO LA MUNGU'!

Hakuna shaka yoyote kuwa kwa kitendo kile maaskofu walicheza rafu ya makusudi. Ni kwa nini nasema hivi? Nasema hivi kwa sababu kwa jinsi mfumo wa uendeshaji wa dini ya kikiristo ulivyo, na hasa kwa dhehebu la Roman Catholic, mlei, yaani muumini wa kawaida, mahusiano yake na muumba wake ni lazima yapitie kwa kiungo ambaye ni padri au askofu. Wabunifu wa utaratibu huu wameweka kanuni mbili muhimu ambazo zinawahakikishia utiifu wa waumini wao kwa muda wote.

Kwanza ni kanuni ya kujumuika kundini. Kwa mujibu wa kanuni hii utahesabiwa kuwa wewe ni muumini wa kweli na mwenye haki za kiroho sawa na waumini wengine, pale tu viongozi wa kanisa watakapojiridhisha kwamba umo 'kundini'; kwa maana ya kuwa unashiriki kikamilifu katika shughuli za kanisa lako chini ya miongozo ya padri wako. Kwa kutumia kanuni hii, wale wanaokwenda kinyume na miongozo ya mapadri na maaskofu wao hujikuta wakipewa adhabu ya kutengwa; na hii ni adhabu kubwa sana kwa sababu unatengwa ukiwa hai mpaka maiti yako!

Kanuni ya pili, ni ile ya mapadri na maaskofu kuwa na mamlaka ya kupokea toba za waumini wao. Kwa mujibu wa kanuni hii, waumini wakifanya dhambi, suala la toba siyo la binafsi kati ya mfanya dhambi na muumba wake, bali ni lazima toba ipitie kwa padri au askofu; ambaye baada ya kusikiliza ungamo lako ana mamlaka ya kutamka kuwa umesamehewa.

Mfumo huu unaozuia mawasiliano ya moja kwa moja kati ya muumini na muumba wake umeweza kujenga utii mkubwa sana wa waumini kwa mapadri na maaskofu wao na kusababisha kanisa kuwa na nguvu ya ajabu. Nguvu hii inatokana na ukweli kuwa kwa kutumia mfumo huu mapadri na maaskofu wamekuwa na mamlaka makubwa sana juu ya waumini wao kuhusu nini wafanye na nini wasifanye.

Maaskofu waliposema kuwa JK ni 'CHAGUO LA MUNGU' ilikuwa ni rafu ya makusudi kwa sababu walikuwa wanajua fika kuwa kwa mamlaka waliyonayo juu ya waumini wao tamko lao lilikuwa ni agizo kwa waumini wao kuhakikisha kuwa siku ya kupiga kura, kura zao zinaenda kwa JK.

Kwa mkristo mkereketwa kutotii agizo la askofu wake siyo tu kuwa ni dhambi, lakini pia ni kutafuta kufukuzwa kutoka 'kundini'. Sasa nani yuko tayari kufanya 'dhambi' ya waziwazi kabisa kama hiyo na kutengwa akiwa hai hadi maiti yake?

Tatizo la kanisa kuwachagulia waumini wao viongozi ni la kihistoria na wala halijajifunga katika mipaka ya kijiografia. Wakina Vladmir Lenin kule Urusi mwanzoni mwa karne ya ishirini walipokuwa wanafanya jitihada za kuwazindua wafanyakazi na wakulima wa huko kuupindua mfumo wa kibwenyenye uliokuwa unawatawala na kuwanyonya, kikwazo chao kikubwa kilikuwa ni viongozi wa kanisa.

Utiifu wa walalahoi hao wa kirusi kwa viongozi wao wa kanisa ulikuwa mkubwa kiasi cha kumlazimisha Lenin kutamka hadharani kwa uchungu kuwa 'DINI NI KASUMBA YA WATU'. Kasumba kama vilivyo vilevi vingine, kazi yake kubwa ni kumzuia mtu kujitambua na kuyatambua mazingira yake katika uhalisia wake.

Wakati vichwa vikiwauma wakina Lenin na Trosky kule Urusi jinsi ya kufuta kasumba ya ukristo kwenye akili za Warusi, kasumba hiyo pia ilikuwa imekamata akili za watu wengi katika mataifa mengine ya Ulaya. Kwa mfano, pamoja na kwamba kule nchini Uingereza hali ya wafanyakazi wengi ilikuwa ni duni sana, jitihada za chama chao cha Labor kushika madaraka ya dola ili kuboresha hali zao za maisha zilikuwa

zinakwamishwa na wafanyakazi wenyewe! Makada wa Labor walikuwa wakitukanwa, kubezwa na hata wakati mwingine kupigwa. Hali kwa makada wa Labor waliokuwa wanaendesha 'Operesheni Zinduka' hiyo iliendelea kuwa mbaya hadi mwaka 1914 pale kitabu cha hadithi cha mwandishi Robert Tressel, kinachoitwa 'The Ragged Trousered Philanthropists', yaani, 'Wasamaria wema waliovaa viraka', kwa tafsri isiyo rasmi, kilipochapishwa.

Kwa kifupi kitabu hiki kilikuwa kinawazungumzia wafanyakazi wa Uingereza ambao hali zao za kimaisha zilikuwa duni sana. Kilikuwa kinawaashangaa ni kiasi gani walikuwa HAWAJIONEI au KUWAONEA HURUMA WATOTO WAO kwa kuleta mabadiliko ya kisiasa, ukizingatia kuwa uwezo wa kufanya hivyo walikuwa nao kupitia kura zao.

Juu ya hali hiyo, mwandishi wa kitabu hicho, Robert Tressel, alielekeza lawama zote kwa kwa kanisa. Alilituhumu kuwa lilikuwa linatumiwa na watawala mabwenyenye na wakandamizaji waliokuwa wameshikilia mamlaka ya kisiasa kuwadanganya waumini wao - kuwa kuendelea kuwatii waliokuwa na mamlaka ya kisiasa juu yao ni KUMTII MUNGU - kwa sababu ati mamlaka zote za kisiasa zimewekwa na Mungu! Kupitia mhusika mkuu ndani ya hadithi hiyo, Tressel aliwaambia wafanyakazi kuwa njia nyepesi ya kuthibitisha kuwa makasisi wao walikuwa wanasema uwongo ni kuwapa changamoto ya kunywa sumu hadharani kwa sababu Bibilia inasema wazi kuwa muumini wa kweli kabisa hata akinywa sumu haitamdhuru!

Wachambuzi wa siasa za Uingereza za kipindi hicho cha mwanzoni mwa karne ya ishirini wanaamini kuwa kitabu hicho cha Tressel kilikuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa chama cha Labor pale chama hicho kiliposhinda kwa mara ya kwanza na kufanikiwa kuunda serikali mnamo mwaka 1924.

Mkakati wa watawala na mabwenyenye ya Ulaya kutumia ukristo kama 'kasumba' ya kuwaleweshea watu ili watawalike na kunyonywa kwa urahisi haukuishia kwenye mipaka ya bara hilo. Wakati tawala za Ulaya zilipokutana na kuamua kugawana bara la Afrika, wamishenari walitumiwa kama 'advance party', yaani wasafisha njia.

Kutokana na uzoefu ziliokuwa nao, tawala hizo zilijua fika kwamba itakuwa ni rahisi zaidi kwa wenyeji wa bara hili kuukubali ukoloni iwapo wenyeji hao tayari watakuwa wametiwa kwenye ukristo.

Afrika Mashariki ni mfano mzuri. Mnamo mwaka wa 1863, makasisi wa Holy Ghost Fathers walitua Zanzibar - nchi ya kiislamu – na kuomba waruhusiwe kufungua kituo chao. Tukio hili ambalo lilikuwa la kwanza la kurasimisha ukristo katika ukanda wa Afrika Mashariki lilitokea takriban miaka 20 kabla ya mkutano wa Berlin wa mwaka 1884. Mkutano huu ndio ulioigawa rasmi ardhi ya Afrika katika mapande mapande na kila tawala iliyohudhuria mkutano huo kukabidhiwa kipande au mapande yake ili kusimika ukoloni.

Baada ya vita kuu ya pili ya dunia, Marekani ilianza kuweka shinikizo kwa mataifa ya Ulaya ili yatoe uhuru wa bendera kwa makoloni yao; na kupisha njia ya kusimikwa kwa ukoloni mamboleo. Kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni mkongwe, ukristo ulitumiwa tena kama mbeleko ya kuubebea huo ukoloni mamboleo.

Zilitumika juhudi kubwa kuhakikisha kuwa takriban viongozi wote wa mwanzo wa zile nchi ambazo zilikuwa zimekabidhiwa uhuru wa bendera ni wakristo, ambao pamoja na mambo mengine, wana jukumu pia la kulinda maslahi ya ukristo dhidi ya yale ya Taifa.

Tanzania ni mfano mzuri. Pamoja na jitihada kubwa sana zinazoendelea usiku na mchana za kumtukuza Mwal. Julius Kambarage Nyerere, Nyerere alikuwa ni mmoja wa viongozi hao. Mwandishi Jan P van Bergen katika kitabu chake Development and religion in Tanzania, amefichua taarifa za kikao cha siri Ikulu ya Dar es Salaam mnamo Agosti 3, 1970 kati ya Rais Julius Nyerere, Padri Robert Rweyemamu na muwakilishi wa Papa, Giovanni Cerrano. Kwa mujibu wa van Bergen, katika kikao hicho Nyerere aliwaeleza viongozi wake wa dini kuwa ameunda idara ya elimu ya siasa katika TANU na amemuweka Padri aiongoze kwa sababu ya imani yake madhubuti. Aliwaeleza pia kuwa katika Kamati kuu ya chama ameweka Mapadri lengo likiwa kulipa Kanisa fursa na uwezo mkubwa hapa Tanzania.

Kutokana na matendo na kauli za maaskofu mbalimbali katika kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea hivi sasa inaonekana dhahiri kuwa rais Kikwete hatakiwi tena na maaskofu. Moja ya matendo ya dhahiri kabisa kufanywa na maaskofu yanayoonyesha msimamo wao ni lile tukio la kuukataa mwaliko wake wa kufuturu naye kule Mbeya wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani uliomalizika hivi karibuni.

Lakini ukitaka kujua kuwa kweli safari hii hawamtaki, rejea matamshi ya askofu Zakariah Kakobe wakati akitoa elimu ya mpiga kura kwa waumini wake, ambapo pia aliitumia fursa hiyo kufuta ibada katika makanisa yake yote siku ya Jumapili ya uchaguzi, ili tu awe na uhakika kuwa kila muumini wake hatakuwa na kisingizio cha kuacha kwenda kupiga kura.

Kakobe amenukuliwa akiwataka waumini wake wasitilie maanani tabia binafsi za wagombea zinazohusu mahusiano yao ya kingono, na badala yake waangalie kile ambacho amekiita, 'kipaji' cha mgombea. Pamoja na kwamba hakumtaja kwa jina, lakini kwa kuzingatia kuwa kati ya wagombea wote wanaowania nafasi ya uraisi kwa sasa, ni Dr. Slaa pekee ndiye aliyekumbwa na kashfa ya ngono, moja kwa moja inaonyesha kuwa Kakobe alikuwa anawapa maagizo waumini wake wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura na kumpigia Dr. Wilbrod Slaa.

Jambo la kushangaza sana kwa ndugu zangu maaskofu ni kwamba, ukiondoa mambo kadhaa yanayomwongezea sifa, 'Kikwete chaguo la Mungu' wa 2005, ndiye huyo huyo ambaye tunaye mwaka 2010. Hata hivyo tofauti na Kikwete wa 2005, hivi sasa Kikwete amekomaa zaidi, kwa maana ya kwamba ameongezeka umri na pia amepata uzoefu wa ziada. Katika tamaduni zetu za Kiafrika 'Mtu mzima ni dawa' , na katika taratibu za uendeshaji wa mambo 'uzoefu wa kina' ni jambo linalotukuzwa.

Aidha Kikwete na serikali yake wameweka mtandao mkubwa wa shule za sekondari za kata na kuongeza kwa kiwango kikubwa sana nafasi za masomo katika taasisi za elimu ya juu, hususan kupitia ujenzi wa chuo kikuu cha Dodoma kinachochukua zaidi ya wanafunzi 40,000 na kile ambacho kiko mbioni kujengwa mkoani Mara kitakachochukua idadi hiyo hiyo ya Wanafunzi. Ni wazi kabisa kuwa katika kipindi cha miaka kumi ijayo mtandao huu wa shule za sekondari na vyuo vikuu utakuwa umefuta kabisa pengo kubwa la kielimu lililopo siyo tu kijiografia, lakini pia kati ya jamii mbalimbali nchini.

Miaka kumi ijayo jamii ya Waislamu haitakuwa tena na sababu za kusema kuwa serikali inawapendelea Wakristo katika nyanja ya elimu; na viongozi wa serikali nao hawatakuwa tena na wakati mgumu wa kuwaambia Waislamu kuwa 'tatizo lao ni la kihistoria' kila wanapofikishiwa malalamiko ya Waislamu. Bila shaka hali hii siyo tu kuwa itaimaarisha mshikamano nchini, lakini pia itakuwa imeweka msingi mzuri kutuhakikishia kuwa amani tuliyonayo nchini inazidi kudumu.

Kikwete pia ametoa mchango mkubwa sana kwa demokrasia nchini kwa kitendo chake cha kubariki maridhiano baina ya vyama vya CCM na CUF kule Zanzibar. Tofauti na Watangulizi wake ambao walikuwa wakifanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa Zanzibar muda wote inaendelea kuwa chini ya genge la CCM wahafidhina, Kikwete kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu amejenga mazingira ya kuhamisha kitovu cha madaraka kutoka kwenye mikono ya wahafidhina hao, na kukiweka kwenye mikono ya Wananchi. Kama jina lake lilivyo, Serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar itakuwa ni serikali ya Wananchi kwa kila hali.

Aidha, tofauti na Mkapa ambaye aliunda tume ya Warioba kwa nia ya kutambua vyanzo na mianya ya rushwa na kisha baada ya kukabidhiwa ripoti akaifungia kabatini na kuisahau; Kikwete kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi amethubutu kuondoa kulindana na u-mwenzetu katika vita dhidi ya ufisadi.

Kitendo chake cha kuruhusu kesi kadhaa za vigogo wa serikali yake na ile ya mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, kufikikishwa mahakamani kujibu tuhuma mbalimbali za ufisadi; ni kielelezo cha wazi cha mabadiliko hayo ya msingi yanayolenga kuondoa dhana kuwa kuna watu 'wasioguswa' na sheria.

Thamani ya kitendo chake haimo kwenye utambulisho binafsi wa nani kafikishwa mahakamani na nani hajafikishwa, ila iko katika 'ujasiri wa kuvunja mwiko' ambao tumeuzoea kuwa siku zote wanaokamatwa na kufikishwa mahakani ni vidagaa tu wakati mapapa, masangara na manyangumi ya ufisadi yanaachiwa yaendelee 'kutesa'.

Aidha kitendo chake cha kuliachia bunge lichunguze kwa kina zabuni ya ukodishaji wa mitambo ya umeme iliyozaa kashfa ya Richmond na kupelekea aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowasa na mawaziri wenzake wawili kujiuzulu, ni moja ya vielelezo vya 'ujasiri huo wa kuvunja mwiko'.

Kashfa ya Richmond haina tofauti sana na kashfa ya ununuzi wa meli ya MV Bukoba enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere. Hata hivyo tofauti ni kwamba enzi ya Nyerere bunge halikuwa na uhuru wa kujadili lolote kwa kina; na kwa maana hiyo basi mjadala wa kina juu ya kashfa ya meli hiyo ukaepukwa.

Enzi ya Nyerere zilikuwepo pia kashfa za kukodi ndege mbovu, kashfa ya farasi wa makatibu kata, nakadhalika. Utawala wa Nyerere ulikwepa kashfa hizi kwa sababu tu vyombo huru vya habari havikuwepo; na pia kwa sababu Nyerere hakuona haya kutumia mamlaka ya kikatiba aliyokuwa nayo kutishia kuvunja bunge pale lilipoonekana kutaka kuchafua hali ya hewa. Tusisahau kuwa hadi leo raisi wa Tanzania bado ana mamlaka hayo kikatiba, na Kikwete angeweza kuyatumia kama angetaka.

Kama nia ni mabadiliko, huenda maaskofu wangehangaika kumpigia debe Prof. Lipumba kwa kigezo cha sifa huenda kidogo tungewaelewa; kwani hakuna mtu yeyote mkweli ambaye hatakiri kuwa Prof. Lipumba kawazidi sifa kwa kila hali wagombea wenzake wanaowania nafasi ya uraisi kwa sasa.

Lakini maaskofu hao wanapojifunga vibwebwe kujaribu kuwaghilibu wafuasi wao kuwa 'wasiangalie mambo binafsi ya wagombea' wakati wa kupiga kura, hata kama mambo hayo yanakiuka zile AMRI KUMI ZA MUNGU, hapo ni lazima tupate wasiwasi juu ya ajenda halisi ya maaskofu wetu. Ndiyo maana tunauliza: Hivi kweli hizi ni kampeni, au ni vita ya msalaba?

No comments:

Post a Comment