Monday, September 6, 2010

FREDERICK SUMAYE ASHITAKIWA KWA KIKWETE KILOSA

Imeandikwa na Mgaya Kingoba, Kilosa; Tarehe: 6th September 2010 Habari Leo

Image

Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye



WANANCHI wa vijiji vya Mvumi na Mvomero mkoani Morogoro, wamewashitaki mfanyabiashara Jeetu Patel na Waziri Mkuu wa Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye kwa Rais Jakaya Kikwete, kwa kuhodhi ardhi kubwa bila kuiendeleza na kutaka wanyang’anywe.

Kwa nyakati tofauti jana, wananchi hao walieleza masikitiko yao kwa Rais Kikwete wakati aliposimama kuwasalimia akiwa katika kampeni ya kuomba kura ili achaguliwe tena kuiongoza Tanzania baadaye mwaka huu.

Akiwa njiani kutoka Kilosa alikohutubia mkutano mkubwa wa kampeni, mgombea huyo wa CCM alisimama katika Kijiji cha Mvumi, ambako moja ya kero alizokumbana nazo ni ya Jeetu kuhodhi mashamba makubwa matatu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Jeetu ambaye ni mfanyabiashara maarufu wa Dar es Salaam, anamiliki mashamba hayo na hayamudu katika uwekezaji wake, na zaidi anayakodisha kwa wananchi kwa Sh 50,000.

“Jeetu Patel, amehodhi mashamba bila ya kuyamudu na anatoza shilingi elfu hamsini kwa ajili ya kulima. Suala hili limepelekwa kwa uongozi wa Wilaya na Mkoa, lakini hakuna utatuzi,” alisema na kushangiliwa na wananchi wenzake.

Mbali ya kero hiyo, Mwenyekiti huyo alizitaja kero nyingine ambazo serikali inapaswa kuzifanyia kazi ni maji, elimu na barabara.

Akijibu hoja ya suala la Jeetu Patel, Rais Kikwete alisema, “niacheni nihangaike nalo, halikuwahi kufika kwangu, ndio kwanza nalisikia kwenu, lakini hakuna lisilowezekana. Niachieni nitafute ukweli wake.”

Akiwa Kijiji cha Mvomero katika Wilaya ya Mvomero, kilio cha ardhi kilisikika tena, na safari hii, kilimgusa Waziri Mkuu wa kipindi chote cha miaka 10 ya Awamu ya Tatu, Sumaye anayemiliki ardhi kijijini hapo.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho hakuwepo wakati Rais Kikwete aliposimama na kusalimia wananchi, lakini mgombea wa udiwani wa CCM, Selemani Shomari maarufu Siri, alieleza wazi kero inayowasumbua ni shamba la Sumaye.

“Tunataka shamba la Mheshimiwa Sumaye lirudi katika Mamlaka ya Mji Mdogo kwa sababu lipo katikati ya mji,” alisema Shomari na kushangiliwa na maelfu ya wakazi wenzake wa mji huo wa Mvomero.

Kama ilivyokuwa katika majibu yake kwa wananchi wa Mvumi, Rais Kikwete alisema, “niachieni nihangaike nalo, nilijue vizuri na kupata majawabu stahili, kwa sababu ardhi ikishatolewa na serikali, kubadili ni lazima ufuate taratibu.”

Shamba la Sumaye alilolinunua akiwa madarakani, linadaiwa lilikuwa la Ushirika wa Wakulima wa Mvomero, uhamishaji wa miliki yake unadaiwa kwamba haukufuata utaratibu husika. Sakata lake lilivuma sana mwaka 2005.

Akiwa Dumila, alilalamikiwa na wananchi wa mji huo kuwa ekari zao 420 zimeporwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kilosa pamoja na maofisa ardhi, licha ya hati za kijiji kuonesha kuwa ni mali yao.

bali ya kuzungumzia suala la shamba la Sumaye lililoko katika barabara iendayo Kijiji cha Makuyu, Shomari alizitaja shida zao nyingine kuwa ni maji; kituo cha afya; kituo cha Polisi na gari lake na kujengewa barabara za mitaa.

Akijibu hoja hizo, Rais Kikwete alisema atawapigania wapate Mamlaka ya Mji Mdogo, hivyo kuweza kumudu kujenga barabara zao wenyewe na pia atasaidia kupatikana kwa kituo cha afya.

Akiwa njiani kutoka Kilosa alikoanza kampeni zake jana, Rais Kikwete alisimama katika vijiji vya Ilonga, Mvumi, Msowero, Kitete, Dumila, Mvomero na kuwasili Turiani ambako alihutubia mkutano mkubwa jioni.

No comments:

Post a Comment