Thursday, March 11, 2010

HABARI YA MAENDELEO YANGU KATIKA MASOMO YA UZAMIVU

Kwa kweli kila jambo hupangwa na Mungu.

1. Mimi nilijizatiti kutoa Andiko langu la kitaaluma la ["STARTING A LEGAL AID CLINIC AT MZUMBE UNIVERSIT (MULAC)]tarehe 9 Machi, 2010 kama nilivyotarajia mapema katika mkutano uliofanyika siku hiyo. Hata hivyo wajumbe wa Mkutano wa Faculty of Law Internal Examiners Board walikataa, kutokana na sababu kwamba Andiko hilo halijatolewa na kujadiliwa katika Idara ya Sheria za Utawala (Administrative Law Department) . Hivyo ikaamuliwa kwamba Andiko hilo likatolewe kwanza katika Mkutano wa Idara ya Sheria za Utawala (Department of Administrative Law).

2. Nilipomuona Mkuu wangu wa Idara Bw. Ignas Sethi Punge, na kumfahamisha jambo hilo mahsusi (alichelewa kufika kikaoni)akasema, itabidi jambo hili lipangiwe siku yoyote baada ya mkutano wa Bodi ya Kitivo cha Sheria tarehe 12/3/2010. Hivyo nimebaki nikisubiri kikao hicho kifanyike ili nikakumbushie tena Idarani kwangu kujua kama kikao cha kujadili Dondoo ya Andiko langu kitafanyika lini.

3. Tatizo ni kuwa pamebakia muda wa siku 10 tu kutoka siku ya Mkutano huo na kufunguliwa Chuo tarehe 22/3/2010. Kwa uzoefu tulionao, Chuo kikifunguliwa, inakuwa vigumu sana kuwapata walimu wa Idara wa kuhudhuria katika mikutano kwa kuwa idadi yao kubwa wanakuwa katika ratiba za kufundisha, hivyo kupanga mkutano wakati huo Kiidara inakuwa ni Mtihani mkubwa. Ndio maana naomba Mungu iwezekane mkutano huo ufanyike ndani ya siku hizo kumi(10) zitakazobaki baada ya Mkutano wa Bodi ya Kitivo cha Sheria.

4. Umuhimu wa Andiko hilo kupita na kufikia katika ngazi ya Bodi ya Kitivo cha Sheria, ngazi ya Seneti na ngazi ya Kanseli ya Chuo ni aina mbili:

(a) Kwanza hatima ya jambo zima hili itajulikana endapo Chuo kitakuwa tayari kuanzisha kituo kama hiki cha Kutoa Msaada wa Sheria kwa Wananchi kwa kutumia wanafunzi wake katika kufanya kazi mbalimbali za kisheria Ki tuoni hapo; jambo ambalo litakuwa ni faida kubwa sana kwa chuo, kwa wanafunzi wetu, kwa majirani na taifa kwa jumla. Pia kitapandisha sana hadhi ya chuo chetu kwamba ndio cha kwanza nchini kufanikiwa kuanzisha kituo kama hiki.

(b) Jambo la pili ambalo ni la kibinafsi zaidi ni kwamba Andiko hilo likishapita kote linakotakiwa kupita kiutaratibu, nimedhamiria kulichapisha Andiko hilo ili linisaidie katika kupandisha Chati yangu ya Kitaaluma Chuoni Mzumbe. Kama mfahamuvyo, katika Vyuo Vikuu vya Taaluma duniani kote kuna ile sera isemayo "EITHER YOU PUBLISH OR YOU PERISH" (Chapisha au Potea). Kwa kuwa sina nia ya kupotea, ni heri nichapishe, inshaallah.

No comments:

Post a Comment