Tuesday, August 11, 2015

TAMKO LA UMOJA WA WANAZUONI WA KIISLAM TANZANIA KUHUSU UCHAGUZI MKUU 2015 TANZANIA



Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehma, Mwenye Kurehemu
UMOJA WA WANAWAZUONI WA KIISLAMU TANZANIA
(HAY-ATUL ULAMAA)
TAMKO LA WANAWAZUONI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2015 NA HATMA YA AMANI YA NCHI YETU

Ndugu wanahabari na watanzania kwa ujumla,
Nchi yetu inapita katika kipindi kigumu na hatari, kipindi cha uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge, wawakilishi na Raisi mwaka 2015.

Katika hali ya kawaida,  mchakato wa uchaguzi haupaswi kutia watu wasiwasi wala hofu ya uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi. Lakini barani Afrika, harakati za uchaguzi zimekuwa chanzo kikubwa cha migogoro ya kisiasa, uvunjifu wa amani na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokana na uchu wa madaraka na kutokutendeka haki kwa wasimamizi wa uchaguzi.

Tumeshuhudia matokeo ya chaguzi hizi za kidemokrasia yakileta maafa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi za DR Congo, Ivory Coast, Kenya, Sierra Leone na hivi karibuni Burundi.

Tumelazimika kutoa tamko hili kutokana na hali inayojitokeza ambapo malalamiko ya wagombea kutokutendewa haki, matumizi ya rushwa kama kishawishi cha kuchaguliwa na kauli zinazoashiria hatari vimeanza kusikika wazi wazi.

Kauli kama ile iliyotolewa na kiongozi mmoja wa chama tawala (CCM) na kunukuliwa na vyombo vya habari likiwemo gazeti la Mwananchi la tarehe 23 Juni kwamba “CCM itashinda tu hata kwa goli la mkono” ni kauli ya kukemewa kwani inaashiria kujiandaa kwa wizi wa kura jambo ambalo ni hatari kwa amani na utulivu wa nchi yetu.

Tunampongeza Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva, kwa kuikataa kauli hiyo na kuahidi kwamba tume haitaruhusu jambo kama hilo kutokea.

Kauli za kuashiria hatari kutoka upande wa upinzani ni pamoja na ile iliyonukuliwa na vyombo vya habari kwamba kiongozi mmoja wa UKAWA akihutubia jijini Mwanza aliliambia jeshi la polisi nchini kwamba “Hatutapiga magoti na kuomba, kama ushindi utapatikana kwa njia halali hatuna tatizo, lakini tukiona mambo yanakwenda ndivyo sivyo tunasema polisi mtatusamehe, mabomu hayatatosha”.

Ndugu wanahabari na wananchi, katika mazingira haya, sisi viongozi wa dini ya kiislamu tumetafakari kwa kina na tunaiona hatari iliyo mbele yetu kama taifa. Tunaiona hatari hii kutokana na mambo yafuatayo:-

i)                  Chama tawala hivi sasa kinauguza majeraha ya mpasuko wa ndani kwa ndani uliojitokeza kule Dodoma, mpasuko ambao unaweza kuliathiri taifa.

ii)                Vyama vya upinzani vinaona ni LAZIMA safari hii vitashinda na kuingia Ikulu.

iii)             Vituo vya polisi vinavamiwa, polisi kuuawa na silaha kuibiwa na watu wasiojulikana.

iv)              Chama tawala kinajiandaa kuhakikisha kinashinda hata kwa “goli la mkono”.

v)                Matumizi ya rushwa na vurugu katika kampeni za uchaguzi kuanza kujitokeza.

vi)              Matukio yanayozidi kila uchao ya wananchi kukosa ustahamilivu na kujichukulia hatua mikononi.

Katika mazingira haya, hekma busara, na kuweka mbele maslahi ya taifa ni lazima vitawale katika kipindi chote cha kampeni, uchaguzi na hata baada ya matokeo ya uchaguzi kutolewa vinginevyo amani na utulivu ulioshamiri kwa miongo kadhaa nchini vinaweza kutoweka mwaka huu.

Ndugu wanahabari na wananchi,
Ili kuhakikisha uchaguzi huu unamalizika kwa amani na usalama, wadau wa mchakato huu ambao ni vyama vyote vya siasa, tume ya taifa ya uchaguzi, Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, vyombo vya ulinzi na usalama, serikali za mitaa, vyombo vya habari, viongozi wa dini zote, asasi za kiraia na wananchi kwa ujumla TUNAPASWA KUTANGULIZA MBELE MASLAHI YA TAIFA KULIKO KITU CHOCHOTE KILE NA KUTUMIA NJIA ZA AMANI KUTATUA MIGOGORO ITAKAYOJITOKEZA.

Tumeitisha mkutano huu na wanahabari ili tutoe tamko letu kwa wadau hawa mbali mbali kama ifuatavyo huku tukiamini kwamba viongozi wa dini hawapaswi kusubiri mpaka mambo yaharibike ndio watoe matamko;

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
Tume ya taifa ya uchaguzi ndiyo mshika dau mkubwa na ni kama baruti inayoweza kulipua bomu kwa sababu ndiyo inayosimamia zoezi zima la uchaguzi kuanzia uandikishaji wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura, kugawa vifaa vya kupigia kura, kuhesabu kura na kutoa matokeo.

Iwapo tume ya taifa ya uchaguzi itafanya kazi yake kwa haki na uadilifu bila upendeleo, kila upande ukaona haki siyo tu imetendeka bali imeonekana kutendeka wazi wazi, vyama vya siasa na wananchi watakubali matokeo na hapo hakutakuwa na sababu ya hofu ya uvunjifu wa amani.

Swali linabaki, katika mazingira haya ya tume kuteuliwa na mmoja wa washindani katika kinyang’anyiro hiki cha madaraka (serikali ya CCM) inaweza kusimamia uadilifu kwa vyama vyote? Jibu ni kwamba tume inaweza kabisa kutenda haki lakini inategemea dhamira za viongozi wa tume hiyo na kuweka kwao mbele maslahi ya taifa badala ya kuegemea upande fulani.

SERIKALI ZA MITAA
Sambamba na hili la tume ya taifa ya uchaguzi ni kwa serikali za mitaa kuanzia chini hadi wakurugenzi wa wilaya, miji na majiji. Huko ndiko vifaa kura hupelekwa, kura kupigwa, kuhesabiwa na matokeo kutolewa kwa kila kata au jimbo kabla ya kuwafikia watu wa tume ya taifa ya uchaguzi.

Uadilifu mkubwa unahitajika sana kipindi hiki ili kulivusha salama taifa letu. Kumekuwa na malalamiko ya kila mara kutoka kwa vyama vya upinzani kwamba baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa wanafanya kazi kama mawakala wa chama tawala badala ya mawakala wa tume ya taifa ya uchaguzi. 

Nasaha zetu kwa tume ya taifa ya uchaguzi na serikali za mitaa, wekeni mbele maslahi ya nchi yetu na vizazi vijavyo. Kutokutenda kwenu haki ndiyo sababu kubwa ya kupelekea uvunjifu wa amani kwa sababu mtu aliyenyimwa haki kuizuia nafsi asikasirike si rahisi. Kwa hiyo msiwatie majaribuni wengine kwa vitendo vyenu mkapendelea upande wowote au mgombea yeyote yule katika uchaguzi.

VYAMA VYA SIASA
Kwa vyama vya siasa hasa CCM na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) nasaha zetu kwao ni hizi zifuatazo. 

Kwa UKAWA; ni wazi kutokana na malalamiko ya uonevu katika chaguzi zilizopita na hakukuwa na mabadiliko kwa tume ya taifa ya uchaguzi, mtakuwa mnaingia katika uchaguzi huu huku tayari mioyo yenu ikiwa haina imani sana na tume ya taifa ya uchaguzi.

Hili ni jambo hatari sana kwa sababu kukosa kwenu imani na tume ya taifa ya uchaguzi kunaweza kuwasukuma kuyakataa matokeo ya uchaguzi hata kama mkishindwa kihalali. Nasaha zetu za dhati kwa UKAWA pamoja na maandalizi yenu makini na imani ya kushinda mwaka huu ni busara pia kujiandaa kisaikolojia kukubali kushindwa kwani hili linaweza kutokea. 

Viongozi wa UKAWA wamekuwa wakisema “CCM ijiandae kisaikolojia kuachia madaraka”. Lakini pia ni muhimu zaidi kwa vyama vya upinzani kujiandaa kisaikolojia kukosa madaraka. Kufanya hivyo kutasaidia kujiandaa kuyapokea matokeo yoyote yale hasa iwapo tume ya taifa ya uchaguzi itatenda haki. 

Kwa Chama Tawala CCM
Tunajua kupoteza madaraka ni jambo lisilowapendeza hata kidogo na bila shaka hampendi hata kulifikiria. Lakini lolote linaweza kutokea kama alivyosema hivi karibuni mwana CCM ndugu Salim Ahmed Salim kuwa “Chama chochote kinaweza kushinda”. Katika hili CCM inafanana kabisa na mtoto aliyezoea kunyonya jinsi ambavyo inakuwa vigumu kukubali kuachishwa ziwa.

Nasaha zetu kwa CCM ni kujiandaa tu kisaikolojia kwa lolote linaloweza kutokea kwani hiyo ndiyo siasa. Kujaribu kung’ang’ania madaraka haitakuwa jambo la maslahi kwa CCM yenyewe wala taifa. Ikitokea kushindwa waamini kuwa inawezekana kuishi nje ya madaraka kama ilivyotokea kwa UNIP ya Zambia, KANU  ya Kenya na MCP ya Malawi. 

Somo pekee CCM inapaswa kujifunza kwa kushindwa vyama hivyo vikongwe ni wao kujiandaa kimkakati jinsi ya kuwa chama cha upinzani mahiri. Kwa hali ilivyo, UKAWA haitarajiwi kushinda majimbo mengi ya uchaguzi na madiwani kuliko CCM. Kwa hiyo inaweza tu kuwa chama madhubuti cha upinzani kwa kuwa na bunge lenye idadi kubwa ya wabunge wake na se

Ikitokea UKAWA wakashinda, hali hii itawapa wakati mgumu sana kutawala nchi hata kama wakishinda uraisi na kuunda serikali. Huwezi kutawala nchi ipasavyo ukiwa na bunge linalodhibitiwa na chama cha upinzani tena kikongwe kama CCM. Hili ndilo ambalo vyama vilivyoondolewa madarakani katika nchi jirani havikujiandaa nalo -jinsi ya kuwa chama cha upinzani makini baada ya kutoka madarakani.

Kwa vyama vyote vya siasa, tunawanasihi kudhibiti hamasa, jazba na hasira za wanachama wao na malalamiko yoyote yale ya kutokutendewa haki katika uchaguzi yapelekwe mahakamani badala ya kuhamasisha vurugu, fujo na uvunjifu wa amani.

VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA
Kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, ninyi ndio washika dau wakubwa wa kulinda amani yetu kwa sababu askari na silaha ziko mikononi mwenu. Kama vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vitajiepusha na ushabiki wa kisiasa kwa kupendelea upande fulani tangu wakati wa kampeni hadi kutangazwa matokeo ya uchaguzi, bila shaka nchi yetu itavuka salama. 

Nasaha zetu ni kwa vyombo hivi kubakia bila upande (neutral) kama viapo vyenu vinavyowaelekeza kulinda Tanzania, watanzania na mali zao.

VIONGOZI WA DINI ZOTE
Kwa viongozi wa dini zote nchini, huu ndio wakati muhimu zaidi wa kuzidisha kuwachunga na kuongoza waumini wetu kwa kuwajenga zaidi kiimani, kuwapa hekima na busara na kuwahimiza kuwa wavumilivu na wasamehevu.

Tukumbuke kuwa nje ya majumba ya ibada utakuta wana-CCM, UKAWA, ACT-wazalendo, TLP, TADEA na kadhalika. Lakini wote hawa wakiingia katika majumba ya ibada anuani yao ni moja tu-WAUMINI ima waislamu, wa

Viongozi wa dini tusikubali uchaguzi huu kutawaliwa na upendeleo wowote ule kidini, jinsia, kabila, rangi, hadhi wala tofauti za kiuchumi kwa sisi wenyewe kushiriki kufanya hivyo au kuwavumilia wale wanaofanay hivyo. Kuruhusu hili ni sawa na kuingia na moto katika chumba chenye petrol. Ni wazi nyumba yetu, taifa letu litaungua. 

OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA
Msajili wa vyama vya siasa anao wajibu mkubwa kuangalia mwenendo mzima wa vyama vya siasa ili visivunje masharti ya kusajiliwa kwao kwa maslahi ya taifa.
Huko nyuma, ofisi hii imekuwa ikilalamikiwa kwa kukipendelea chama tawala kama inavyotuhumiwa tume ya taifa ya uchaguzi. Safari hii mazingira ni tete hivyo watendaji wa Ofisi ya Msajili wa Vyama waweke maslahi ya taifa mbele.

VYOMBO VYA HABARI
Vyombo vya habari vinao mchango mkubwa kuhatarisha amani au kuilinda. Ushawishi wenu kwa wananchi kwa kutengeneza mitazamo katika jamii (public opinion) kupitia habari zenu utumike vizuri katika uchaguzi mwaka huu.

Vyombo vya habari viripoti kuhusu mchakato huu kwa uadilifu pasina kupendelea wala kupokea rushwa. Mkimjenga mgombea mbovu wananchi wakamchagua au mkishabikia vitendo vinavyohatarisha amani mjue kuwa mtakuwa mmetumia tasnia yenu kuhatarisha amani ya taifa letu na vizazi vijavyo vitawahukumu.

ASASI ZA KIRAIA NA ZA KIDINI (AZAKI)
Asasi za kiraia na za kidini ni wadau muhimu katika uchaguzi huu. Nasaha zetu kwao ni kuhakikisha kwamba kunakuwa na haki sawa (fair play) katika uchaguzi na si kuchochea mitazamo ya kuwagawa wananchi kwa misingi ya kibaguzi.

MAHAKAMA ZA KISHERIA
Mahakama ndiyo kimbilio la wale wote watakaohisi kuonewa. Tungependa kutoa wito kwa wagombea wote, vyama vyote vya siasa na wananchi kwa ujumla kujenga tabia ya kupeleka malalamiko yao mahakamani ili wapate ufumbuzi wa kisheria.

Kama matokeo ya uchaguzi yanaweza kupingwa mahakamani, kwa nini chama au wananchi wajichukulie hatua mikononi mwao? Wito wetu kwa mahakimu na majaji wajiandae kutenda haki kuhusu kesi za uchaguzi.

Hili ni muhimu sana kwa sababu wananchi wakikosa imani ya kupata haki zao mahakamani bila shaka watashawishika kufanya fujo na vurugu ambazo zitapelekea uvunjifu wa amani.

WANANCHI WOTE
Mwisho kabisa kwa wananchi wote, wanasiasa mbali na madai yao ya kutaka kuwatumikia wananchi pia wanacho  kitu wanachokipigania. Kitu hicho ndicho kinachowapelekea kutoa au kupokea rushwa, kufanyiana fitna, majungu, siasa za kuchafuana na hata wako tayari amani ya nchi yetu iharibike iwapo watakikosa kitu hicho. Kitu hicho ni MADARAKA.

Lakini wanasiasa wanahitaji kuungwa mkono na wananchi ili wayafikie malengo yao hayo. Iwapo sisi wananchi tutakuwa wakomavu na kuweka mbele maslahi ya nchi yetu kwanza kwa kuhakikisha chochote kinachoashiria au kuhatarisha amani hakipewi nafasi, tutakuwa tumeliepusha taifa letu na uvunjifu wa amani.

Ndugu wanahabari na watanzania,
Nchi hii ni yetu sote. Kila mmoja wetu ajiulize maslahi gani mazito kwake; maslahi ya mtu mmoja mmoja au maslahi yetu sote kama taifa? Ni kweli madaraka kuwa mikononi mwa watu waadilifu ni jambo la muhimu, lakini tukumbuke nchi kuwa katika hali ya amani na utulivu ni jambo muhimu zaidi.
Asanteni sana.





No comments:

Post a Comment