Friday, February 27, 2015

MAZITO YA ANDREW CHENGE YAIBUKA SECRETARIATI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

Mazito ya Chenge yaibuka

      
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Alhamisi,Februari 26,  2015  saa 9:13 AM
KWA UFUPI
Mbunge huyo wa Bariadi Magharibi aliibua mvutano wa kisheria akipinga kujadiliwa.
Dar es Salaam. Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge ameibuliwa tuhuma nzito kwenye Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma baada ya kudaiwa kuwa aliishawishi kampuni ya Independent Power Solution Limited (IPTL) kuingia mkataba na Tanesco na baadaye kuwa mshauri wa kampuni hiyo binafsi iliyomuingizia Sh1.6 bilioni zinazohusishwa na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo, Chenge, ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Umahiri wa Sheria kwenye Chuo Kikuu cha Harvard cha Marekani, aliwasilisha amri ya zuio ya Mahakama Kuu inayokataza chombo chochote cha Serikali kujadili sakata la escrow hadi hapo shauri lililopo mahakamani litakapotolewa uamuzi, jambo lililozua mjadala wa kisheria na kusababisha mwenyekiti wa Baraza la Sekretarieti ya Maadili, Jaji Hamisi Msumi, kuahirisha hadi leo.
Chenge ni mmoja wa watu kadhaa wanaotarajiwa kuhojiwa na kamati hiyo kutokana na kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh306 bilioni kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa Benki Kuu kwa makubaliano kati ya Tanesco (shirika la umeme la umma) na IPTL baada ya pande hizo mbili kutofautiana kuhusu tozo za malipo ya umeme unaozalishwa na kampuni hiyo binafsi.
Mwingine ni mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Anna Tibaijuka, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na ambaye pia aliingiziwa kwenye akaunti yake Sh1.6 bilioni zinazohusishwa na akaunti hiyo ya escrow.
Wote wawili waliingiziwa fedha hizo na James Rugemarila, mkurugenzi wa VIP Engineering iliyokuwa ikimiliki asilimia 30 ya hisa za kampuni ya IPTL.
Tuhuma dhidi ya Chenge
Tangu sakata la escrow lianze, haikuwahi kuelezwa kuhusika kwa Chenge kwenye sakata hilo.
Lakini jana, akisoma hati ya malalamiko dhidi ya mbunge huyo wa Bariadi, mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili, Hassan Mayunga alisema mlalamikiwa, akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) mwaka 1995, aliishauri Serikali kuingia mkataba wa miaka 20 na IPTL wa kuongeza uzalishaji wa umme.
“Mlalamikiwa baada ya kustaafu wadhifa wa AG, Desemba 24 mwaka 2005, mwaka 2006 aliingia mkataba wa kuwa mshauri mwelekezi wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited iliyokuwa inamiliki asilimia 30 ya hisa za IPTL,” alisema Mayunga akikariri hati hiyo ya malalamiko.
“Kitendo cha mlalamikiwa kuingia mkataba na VIP Engineering and Marketing Limited iliyokuwa na asilimia 30 ya hisa kwenye kampuni ya IPTL ni ukiukwaji wa fungu la 6 (j) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambalo linamzuia kiongozi wa umma kujinufaisha na utumishi wake uliopita kwa kutumia taarifa alizozipata alipokuwa anatekeleza majukumu yake kwa manufaa binafsi.
“Kitendo cha mlalamikiwa kuendelea kuwa mshauri mwelekezi wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited akiwa na wadhifa wa ubunge ni ukiukwaji wa fungu la 6(e) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambalo linamzuia kiongozi wa umma kujiingiza katika mgongano wa maslahi.”
Mwanasheria huyo aliendelea kusema kuwa mkataba ambao mlalamikiwa aliingia na kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited ulimpatia manufaa ya kifedha ya Sh1.617 bilioni kinyume na fungu la 12(1)(e) la Sheria ya maadili ya viongozi wa umma. Aliongeza kuwa mlalamikiwa hakutamka maslahi aliyokuwa nayo katika mkataba wa Tanesco na IPTL kinyume na fungu 14 la sheria ya Maadili.
Aliongeza kuwa mlalamikiwa hakutamka madeni yake aliyokuwa anaidai kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited kwa Kamishna wa Maadili kinyume na matakwa ya fungu la 9(6)(b) la sheria hiyo.
“Malalamiko dhidi ya Chenge yanawasilishwa mbele ya Baraza la maadili lenye mamlaka ya kisheria ya kufanya uchunguzi wa kina na kumtaka mlalamikiwa kutoa maelezo bayana kuhusu mwenendo wake kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria,” aliongeza.
Baada ya kusoma tuhuma hizo, Chenge alitoa amri hiyo ya zuio la Mahakama Kuu ambayo pia iliwasilishwa kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano kulizuia kujadili ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu sakata hilo la escrow, lakini ikagonga mwamba baada ya wabunge na spika kulinda muhimili wao.
“Kwa kuwa amri hii ya mahakama nilikuwa sijaipata na ninyi (wanasheria wa sekretarieti) mlikuwa mmeipata mapema ngoja nikaisome na wenzangu,” alisema Jaji Msumi ambaye alikuwa akisaidiana na wajumbe wawili, Selina Wambura na Hilda Gondwe.
“Kama kweli mahakama imezuia vyombo vyote, suala hapa ni kuangalia amri hiyo. Tupeni muda tukaangalie na kesho (leo) tutatoa uamuzi kama tutaendelea au la.”
Mvutano ulivyokuwa
Kabla ya kuahirisha shauri hilo ulizuka mvutano mkubwa wa kisheria kuhusu amri hiyo ya zuio la mahakama.
“Suala hili ninavyofahamu mimi liko mbele ya Mahakama Kuu, hivyo tusubiri uamuzi wa mahakama kwani amri ya mahakama ilizuia vyombo vyote vya Serikali na hiki (Baraza la Maadili) ni chombo cha serikali. Mwenyekiti, mimi nataka kupata mwongozo wa suala hili, tukiendelea bila kupata mwongozo na mimi kama mwanasheria litanisumbua sana,” alisema Chenge ambaye alikuwa Mwanasheria wa Serikali kati ya mwaka 1972 na 1973.
Lakini Mayunga alisimama na kusema: “Mheshimiwa mwenyekiti, hii amri ya mahakama ambayo mlalamikaji (Chenge) ameitoa hapa, si Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inayohusika kama mlalamikiwa alivyotaja.
“Tuhuma ambazo zimeletwa hapa ni tuhuma za uvunjifu wa maadili ya viongozi wa umma na wala siyo suala lililoonyeshwa katika hii amri... ni tofauti kabisa.”
Mayunga, katika kujenga hoja, alisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara 132 (1) ya inayosema kuwa “kutakuwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo itakuwa na mamlaka ya kuchunguza tabia na mwenendo wa kiongozi wa umma yeyote kwa madhumuni ya kuhakikisha kwamba masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma yanazingatiwa ipasavyo”.
Pia alisoma fungu la 18 (2) (c) la sheria hiyo linaloipa Sekretarieti ya Maadili mamlaka ya kuchunguza tuhuma yoyote ya kuvunjwa kwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na viongozi wote wa umma, wanaopaswa kuwajibika chini ya sheria hiyo.
Kutokana na sheria hii, Sekretarieti haizuiwi kuendelea na shauri hili. Madai dhidi ya mlalamikiwa ni ya jinai na rushwa. Hapa tunajikita katika maadili wala sisi hatuzungumzii escrow, hapa ni maadili kuwa amepokea fedha kutoka VIP Engineering,” alisema Mayunga
Jaji Msumi alisema hati hiyo aliipitia haraka haraka na akahoji kama ina amri inayozuia suala hilo kujadiliwa.
Chenge alijibu, “mheshimiwa mwenyekiti, hoja ambayo nimeileta mbele yako ni zuio la mahakama. Kueleza kwamba chombo hiki kiko juu ya mahakama bila...”
Kabla ya kumalizia sentensi hiyo alisimama mwanasheria wa Sekretarieti hiyo, Filotheus Manula na kusema: “Kauli anayoisema mlalamikakiwa kuwa chombo hiki kiko juu ya mahakama siyo sahihi. awali Mayunga alishaelezea. Katiba na Sheria ya Maadili na iko wazi.”
Lakini Chenge akasema: “Ni vizuri vijana wakajifunza... amri hii ya mahakama siyo maoni yangu, hivyo ni vyema ikaheshimika. Itanisumbua mimi, mamlaka ya chombo hiki isitishwe siyo kwamba haina mamlaka, mnaweza kuendelea sawa, lakini hili ni ombi langu.
“Utawala wa sheria ni bora ukaheshimiwa na masuala ya siasa tuache tukapige siasa majukwaani.”
Mayunga alisimama na kusema: “Mheshimiwa mwenyekiti ukiruhusu hiki anachokisema au uhalisia wa kuzuia kinachoendelea, siyo sahihi.”
Chenge alijibu, “mheshimiwa mwenyekiti amri ya mahakama ni (inahusu) taarifa ya ukaguzi wa miamala ya akaunti ya Tegeta Escrow ya (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) CAG, na malalamiko yanayoletwa dhidi yangu ndiyo ambayo yamezuiwa... mimi ninachoomba ni ufafanuzi au mwongozo kwa hili.”
Lakini Manula alipinga akisema: “Penal Code (Sheria ya Kanuni ya Adhabu) haitumiki hapa. Mlalamikiwa ndiye aliyekuwa AG, alisimamia kuitunga... madai, jinai na rushwa, lakini hapa tunajadili maadili na siyo escrow.”
Chenge, aliyekuwa amesimama wakati wote, aliendelea na msimamo wake wa kuomba mwongozo, hali iliyomfanya mwanasheria mwingine wa sekretarieti hiyo, Getiruda Cyriacus kusimama na kunukuu fungu la 18 (4) la sheria hiyo linalosema sekretarieti itakuwa na mamlaka ya kuanzisha na kufanya uchunguzi wowote kuhusu ukiukwaji wa maadili yaliyotajwa katika sheria hiyo.
Vituko vya Chenge
Chenge aliingia kwenye viwanja vya Ukumbi wa Karimjee saa 3:02 asubuhi akiwa katika gari aina ya Toyota Land Cruizer akiongea na simu na aliposhuka, aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa wakimpiga picha akisema: “Nendeni mkauze magazeti na sura ya Chenge.”
Alipotaka kuingia ukumbini, aliambiwa asubiri kwenye viti, lakini aligoma na badala yake alishuka chini na kuanza kuzungumza na simu huku akizungukazunguka takribani dakika 10 kabla ya kutakiwa kuingia ukumbini saa 3:13 asubuhi.
Mara baada ya Jaji Hamis kuahirisha baraza hilo saa 3:55, waandishi walianza tena kumpiga picha na kama kawaida alisema: “Nendeni mkaandike mnavyoona... mnataka na mgongo muupige picha?”
Waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari walipotaka kufanya naye mahojiano ya suala hilo alijibu, “siwezi kuzungumzia chochote kuhusu yaliyopo katika maadili” na kupanda gari, kisha akaondoka


No comments:

Post a Comment