Monday, January 5, 2015

JUMBE ZA SMS KUCHUJWA WAKATI WA UCHAGUZI MKUU TZ - 2015 !!!

 KUTOKA  HABARI LEO, TANZANIA, 5/12/2014.


Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame :


KATIKA kuhakikisha uchochezi unaoweza kuvuruga amani ya nchi unadhibitiwa wakati wa uchaguzi, Serikali imeiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuja na mwongozo wa kampuni za simu katika kudhibiti ujumbe mfupi kwa njia ya simu.

Aidha, ameitaka sekta ya utangazaji nchini kutumia fursa ya Mkongo wa Taifa katika utangazaji.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa alipokuwa akifungua maadhimisho ya Siku ya Teknolojia ya Mawasiliano (ICT) Afrika.
Katika ujumbe wake kwa siku hiyo, alisema ujumbe mfupi wa kwenye simu usipodhibitiwa unaweza kuleta madhara makubwa wakati wa uchaguzi.

“TCRA mje na mwongozo wa makampuni ya simu hasa kuhusu ujumbe, maana kama utaachwa hivi hivi wakati wa uchaguzi itakuwa ni hatari, Kenya ilifanya hili na walifanikiwa,” alisema.

Tayari TCRA imeshatengeneza miongozo ya namna ya kuripoti na kuandaa vipindi wakati wa uchaguzi kwa upande wa sekta ya utangazaji na wamiliki wa mitandao ya kijamii, yaani ‘blogers’.

Mbarawa alitumia nafasi hiyo kuvitaka vyombo vya utangazaji kutumia miongozo waliyopewa katika kutangaza habari na zisizo na ushabiki na kutotumiwa vibaya na baadhi ya watu.

Kuhusu Mkongo wa Taifa, Mbarawa aliitaka sekta ya utangazaji kutumia ipasavyo fursa ya kuwapo kwa Mkongo wa Taifa katika matangazo yao.

Alisema Serikali imewekeza dola za Kimarekani milioni 200 (Sh bilioni 340) katika teknolojia hiyo na kuwa sekta ya simu ndiyo pekee inayotumia na kunufaika na teknolojia hiyo.

Mbarawa alisema ili kuhakikisha taasisi za utangazaji zinatumia Mkongo wa Taifa, amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake kuunda timu ya wadau itakayoangalia suala hilo.

Awali, Mkurugenzi wa TCRA, Profesa John Nkoma alisema teknolojia ya mawasiliano nchini imekuwa na manufaa na kuchagiza maendeleo ya wananchi.

Nkoma alitolea mfano kuwa hadi sasa kuna laini za simu milioni 28 na laini za intaneti milioni tisa na kuwa matumizi ya simu katika kufanya miamala ya kibenki imeongezeka.

Naye Mratibu wa Ufundi wa Umoja wa Mawasiliano Afrika (ATU) “African Telecommunications Union), Kezias Mwale aliipongeza Tanzania kwa kuwa miongoni mwa nchi tatu za Afrika ambazo zimeshahamia kwenye dijitali na kuwa baadhi ya nchi zimeahidi kufikia lengo hilo kabla ya muda uliowekwa kupita.

Tanzania inatarajiwa kuingia katika mwaka wa uchaguzi mwaka kesho, kwani mbali ya kutarajiwa kupata Rais wa Awamu ya Tano atakayechukua nafasi ya Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake, wananchi wanatarajiwa pia kupiga kura za kuwapata wawakilishi wapya katika ngazi za majimbo na kata.

Aidha, kama sehemu ya mchakato wa uchaguzi mkuu ujao, mwishoni mwa wiki ijayo Watanzania watafanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaowaweka madarakani viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa.

No comments:

Post a Comment