Imetundikwa hapa leo hii tarehe 16/4/2013.
TAMKO LA HAKIELIMU KUHUSU
BAJETI YA SEKTA YA ELIMU MWAKA WA FEDHA 2013/2014
UTANGULIZI
Yanayotokea sasa katika sekta ya elimu yanaleta aibu kusimulia na yanaumiza kutafakari. Uwezo duni wa vijana wanaohitimu shule za msingi na sekondari, wanafunzi kufaulu bila kujua kusoma na kuandika, kuporomoka kwa ufaulu na kuongezeka kwa kiwango cha kutojua kusoma na kuandika ; haya ni baadhi tu ya mambo ambayo yanapaswa sasa kutufumbua macho na kutufanya tutambue ukweli kuwa tunapoteza mwelekeo na kama hatua za makusudi za kunusuru elimu zisipochukuliwa, basi tujue tunajenga taifa la watanzania wasio na ujuzi na maarifa ya kutatua changamoto za kiuchumi, kisiasa na kijamii zinazoendelea kutukabili.
Hali hii imeshaanza kuathiri upatikanaji wa maendeleo ya mtu binafsi, familia na hata taifa kwa ujumla. Tumepuuza kwa muda mrefu hali ya kushuka kwa ubora wa elimu, leo hii tunashuhudia matunda yake na kama tutaendelea “kufunika kombe mwanaharamu apite” tutajifariji na uwepo wa wanafunzi shuleni lakini wasio jifunza kikamilifu wala kuelimika ipasavyo, hatimaye kuwa na taifa mbumbumbu ambalo litashindwa kujiongoza.
Matokeo ya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne mwaka 2012 yanaakisi kiwango cha juu cha kudorora kwa elimu nchini na matokeo ya kuipuuza elimu. Tumeshuhudia watahiniwa
240,903 sawa na asilimia 60.6 wakipata daraja
SIFURI katika matokeo hayo;
103,327 sawa na asilimia 26.02 wakipata daraja la nne huku wanafunzi
23,520 tu, ambao ni sawa na asilimia 5.16 (waliopata kati ya daraja la kwanza, la pili na la tatu) ndiyo wakihesabiwa kufaulu vizuri.
Matokeo ya mtihani wa kitaifa wa darasa la saba mwaka 2012 hali kadhalika, sehemu kubwa ya waliochaguliwa (zaidi ya wanafunzi
294,833) wamepata ufaulu wa daraja “D”. Aidha, zaidi ya watahiniwa
139,923 sawa na asilimia 35.45 ya waliofanya mtihani wa kitaifa wa kidato cha pili 2012, hawakufaulu. Kiwango cha kutojua kusoma na kuandika kinazidi kuongezeka na sasa kimefikia asilimia 30 tofauti na ilivyokuwa miaka ya 1980 ambapo ilikuwa asilimia 9 tu. Wanafunzi wengi wanamaliza darasa la saba hawajui kusoma na kuandika.
Takwimu za elimu hadi mwaka 2012 zinaonesha hali ya mazingira ya kujifunzia katika shule zetu kuanzia elimu ya awali mpaka sekondari kutokuwa ya kuvutia. Uwiano wa mwalimu mwenye sifa kwa mwanafunzi kwa elimu ya awali umebaki kuwa 1:124 badala ya 1:25; uwiano wa matundu ya vyoo kwa wanafunzi msingi unakadiriwa kuwa 1:56 badala ya 1:25 kwa wavulana na 1:55 badala ya 1:20 kwa wasichana. Mrundikano wa wanafunzi darasani ni mkubwa mno, wastani kwa nchi nzima ni 1:70 badala ya 1:40, uhaba wa madawati unafikia asilimia 49.1 kwa sasa ikiwa ni upungufu wa takribani madawati
1,879,806 kati ya
3,893,338 yanayohitajika.
Shule za sekondari pia zinaathiriwa na changamoto za namna hii ikiwa ni pamoja na tatizo la uhaba wa mabweni, maabara, vitabu na walimu wa masomo ya sayansi. Pia hamasa ya mioyo ya walimu kujitolea na kuridhika na ualimu iko chini sana(HakE, 2011). Changamoto hizi zinatupa ishara kuwa shule zetu za umma (msingi na sekondari) si shule ambazo zina viwango vya kuridhisha na hata kumsaidia mwanafunzi afundishwe na ajifunze ipasavyo.
Siyo siri kuwa changamoto hizi zina uhusiano wa moja kwa moja na upangaji wa vipaumbele vyetu na maamuzi ya matumizi ya rasilimali za taifa. Ikiwa tunataka kutoka hapa tulipo kwenda mahali bora zaidi ni lazima upangaji wa bajeti katika sekta ya elimu uangaliwe kwa makini sana kwa kuwashirikisha wadau wote wa sekta ya elimu ili kutatua changamoto za sekta ya elimu. HakiElimu inaishauri serikali sasa kuacha visingizio vya uhaba wa bajeti na wahisani kukwamisha utekelezaji wa mipango ya kuikwamua elimu. Kwa kutambua mchango wa ushiriki wa wadau na HakiElimu tukiwa wadau tunaosononeshwa na hali mbaya ya elimu inayoendela kwa sasa, yafuatayo ni maoni au mapendekezo ya HakiElimu katika upangaji wa bajeti ijayo ya sekta ya elimu 2013/2014. Na haya tungependa yatiliwe mkazo sana;-
TATIZO LA WANAFUNZI KUTOJUA KUSOMA NA KUANDIKA
Hili bado ni tatizo kubwa na hadi sasa serikali haijawa na mkakati maalumu wa kuondoa tatizo hili. Shule za msingi kwa madarasa yote bado zina wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika. Hali hii imejitokeza pia katika baadhi ya shule za sekondari licha ya serikali kudai itawabaini na kuwaondoa. Tatizo hili lazima lianze kufanyiwa kazi kwa kuwa na mpango maalumu wa kutathmini idadi kamili ya wanafunzi hao na kupanga mkakati wa makusudi wa kutokomeza tatizo la kuwa na wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika sekondari. Mpango huu lazima uwashirikishe wadau wote wa sekta ya elimu hasa wazazi na kamati za shule ili watambue majukumu yao katika kuondoa tatizo hili.
Kwa kuwa elimu ya awali ni msingi wa mwanafunzi katika kujifunza kusoma na kuandika, tunataka kuona bajeti hii inatia mkazo katika uwekezaji katika elimu ya awali hasa kuwa na walimu bora na vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Uwekezaji katika elimu ya awali utachangia sana kupunguza tatizo sugu la kuwa na wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika katika shule za msingi. Tunatambua kuwa katika Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM III), Serikali imeazimia kuanzisha fungu maalumu katika bajeti ya elimu (separate budget line) kwa ajili ya elimu ya awali na kutenga asilimia 20 ya matumizi yake ya kawaida kwa ajili ya sekta ya elimu huku asilimia 60 ya fedha zitakazotengwa kwa ajili ya sekta kuelekezwa katika elimu ya awali na msingi. HakiElimu ingependa kuona mpango huu ukianza kutekelezwa kikamilifu katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2013/14.
UHABA WA FEDHA NA WATAALAMU IDARA YA UKAGUZI WA SHULE
Ripoti ya tathmini ya Mpango wa pili wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM II) inaonesha kutofikiwa kwa malengo ya ukaguzi wa shule hivyo kuziacha shule nyingi bila kukaguliwa. Sababu kubwa ya kutofikiwa kwa malengo ya ukaguzi ni uhaba wa fedha unaosababisha uhaba wa vitendea kazi na wataalamu wa ukaguzi. Mwaka 2011/12 shule za msingi zilizokaguliwa ni 3,061 tu kati ya 7,200 zilizopangwa kukaguliwa (sawa na asilimia 42.5). Aidha, sekondari 935 (43.3%) zilikaguliwa kati ya 2,100 zilizopangwa kukaguliwa. Hii ni kusema ni asilimia 19.1 pekee kati ya shule za msingi nchini hukaguliwa na asilimia 21.4 tu ya sekondari hukaguliwa kwa mwaka. Tafsiri hapa ni kuwa uwezo wa fungu la ukaguzi katika bajeti ni kukagua asilimia 20 tu ya shule zake zote, asilimia 80 ya shule hazipati fursa ya kukaguliwa kutokana na uhaba wa bajeti.
Athari za shule kutokaguliwa ni nyingi, kwa mfano utendaji wa walimu kutopimwa, utekelezaji wa mitaala, maendeleo ya shule na wanafunzi kutopimwa. Kama ukaguzi haufanyiki kwa nini tunashangaa wanafunzi kufeli au kumaliza elimu ya msingi na kufaulu mitihani ilihali hawajui kusoma na kuandika? HakiElimu inatoa rai katika bajeti ya 2013/14 kutoa kipaumbele katika kuimarisha ukaguzi wa shule. Serikali itenge fungu la kutosha kwa ajili ya ukaguzi, tumeona athari ya shule kutokaguliwa katika matokeo mabaya ya wahitimu wa darasa la saba, kidato cha pili na cha nne 2012 na tusingependa kuona haya yakijirudia.
SERA YA ELIMU NA MAFUNZO NA SERA YA ELIMU YA AWALI
Serikali imeendelea kupanga bajeti zake kwa kuzingatia “Sera ya Elimu na Mafunzo iliyopitwa na wakati” (ETP 1995). HakiElimu inajiuliza Mpango wa III wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM III) ambao serikali imeanza kuutekeleza umetokana na sera gani? Pia Mabadiliko ya mtaala wa elimu kutoka kuwa Mtaala unaoangalia maudhui kwenda katika Mtaala unaomjengea mwanafunzi ujuzi ulifanywa kwa kutumia sera gani? Je imetumia sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 au rasimu ya sera mpya ambayo bado haijapitishwa?
Tunahoji sera gani kwa kuwa sera ya 1995 inayopigiwa kelele kutokidhi mahitaji na kupitwa na wakati haijapatiwa mbadala na ni wazi kuwa kuendelea kupanga bajeti kwa kutumia sera iliyopitwa na wakati kunaweza kusitupe matokeo mazuri yanayokusudiwa katika elimu kama ambavyo tumeshuhudia katika matokeo ya kidato cha nne 2012. Wakati umefika sasa waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi aje na majibu juu ya lini sera hii itakuwa tayari na itaanza kutumika ili kutoa dira katika mipango na utelekelezaji wake ikiwemo bajeti.
UHABA WA FEDHA ZA RUZUKU SHULENI
Ili kuinua ubora wa elimu, serikali iliazimia kutoa ruzuku kwa kila mwanafunzi kupitia MMEM na MMES Shilingi 10,000 kwa kila mwanafunzi wa shule ya msingi na 20,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kila mwaka. Hata hivyo, takwimu za elimu 2012 zinaonesha wastani wa sh. 6,025 tu ndizo hufika shuleni badala ya 10,000/= kwa shule za msingi na wastani wa shilingi 14,178/= pekee badala ya shilingi 20,000/= zilizoahidiwa kwa kila mwanafunzi wa Sekondari.
Hali hii imekwamisha shughuli nyingi za maendeleo ya wanafunzi shuleni, vitabu havinunuliwi kwa wakati, nyenzo za kufundishia na fedha za uendeshaji wa shule hazitoshi. HakiElimu inaishauri serikali kutenga kiwango kamili cha 10,000/= na 20,000/= kama mipango inavyoonesha. Na tena ni muhimu upangaji uzingatie mfumuko wa bei ambao umekuwa ukiathiri pia uwezo wa shilingi katika kufanya manunuzi, itakumbukwa kuwa upangaji wa kiwango hiki cha ruzuku ulifanyika 2002-2006 wakati mfumuko wa bei ukiwa katika wastani wa 4.4% wakati leo wastani wa mfumuko wa bei ni asilimia 14.9% , hii ni mara tatu zaidi ya kiwango cha awali.
UPANGAJI NA USIMAMIZI WA FEDHA ZA UMMA
Serikali imekuwa ikitoa ahadi juu ya kupunguza bajeti ya matumizi ya kawaida kwa muda sasa, (Hotuba ya Waziri wa Fedha Juni 9, 2011). Hata hivyo bado Wizara ya Elimu imeendelea kutenga fedha nyingi katika matumizi ya kawaida huku eneo la “matumizi mengineyo” likiendelea kutengewa fedha nyingi zaidi. Takwimu zinaonesha bajeti ya matumizi ya kawaida ya wizara imeongezeka kutoka bilioni 523.8 mwaka 2011/12 hadi bilioni 631.9 mwaka 2012/13, sawa na ongezeko la asilimia 20; wakati fedha za matumizi mengineyo (posho, mafuta, safari, samani na ukarimu) ikiongezeka kutoka bilioni 207 mwaka 2011/12 hadi bilioni 386 mwaka 2012/13 sawa na ongezeko la asilimia 86. Hii ina maanisha bado agizo na ahadi ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima halizingatiwi katika bajeti zetu.
Pia utekelezaji wa bajeti ya sekta ya elimu umekuwa si mzuri. Licha ya serikali kudai haina fedha za kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu, bado kumekuwa na usimamizi mbaya wa hata zile fedha kidogo zinazopangwa. Ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2010/2011 imebainisha fedha zilizotolewa kwa miradi ya MMEM na MMES kushindwa kutumiwa na Halmashauri katika kutekeleza miradi hiyo. Hata fedha zinazotolewa kwa ajili ya mfuko wa jimbo ambazo zingesaidia kuboresha shule zetu nazo hazitumiki.
Rai yetu ni kuwa bajeti hii ya mwaka wa fedha 2013/14 iachane na matumizi ya kawaida yasiyokuwa ya lazima, badala yake fedha hizo zitumike kutatua changamoto muhimu kama vile urekebishaji wa maslahi ya walimu kama mishahara, posho za mazingira magumu, nyumba katika maeneo yasiyokuwa na nyumba za kupanga na kuboresha mazingira yao ya kufundishia shuleni. Hatua hii itasaidia kurudisha morali wa ufundishaji na kupunguza matatizo ya ufaulu nchini. Upangaji wa fedha na matumizi yake katika elimu kamwe hauwezi kuwa na mafanikio iwapo kutaendelea kuwepo kwa kutoelewana kati ya walimu na serikali. Mwalimu ni mtekelezaji mkuu wa bajeti na mipango shuleni, hivyo hakuna budi kukawa na maelewano kati ya wadau hawa muhimu ili utekelezaji wa mipango uwe na ufanisi na uwekezaji ulete tija.
Pia, tufike mahala sasa tupange bajeti kwa kuwa na vipaumbele vichache ili tuvitekeleze. Ni dhahiri kuwa, Serikali haiwezi kutatua matatizo yote kwa wakati mmoja, hivyo lazima tujenge utamaduni wa kuwa na kipaumbele au vipaumbele vichache katika bajeti kwa kila mwaka wa fedha ili kutatua changamoto za sekta ya elimu. Bajeti hii lazima ieleze bayana mikakati ya Wizara ya kuboresha usimamizi na ufanisi wa fedha za umma hasa katika kuhakikisha fedha zinafika kwa walengwa kwa wakati, zinatumika kama zilivyopangwa na zinatumika ipasavyo kwa mantiki ya kuleta ufanisi wa fedha.
Elizabeth Missokia
Mkurugenzi Mtendaji
HakiElimu