Thursday, January 24, 2013

TAMKO LA WILLIAM BENJAMIN MKAPA [RAIS MSTAAFU WA TANZANIA] KUHUSU RASILIMALI TANZANIA

IMETUNDIKWA HAPA LEO HII  24/1/2013.

 TAMKO HILI LILIKUJA BAADA YA WANA-MTWARA KUANDAMANA KUDAI HAKI YA KUTUMIA WAO GESI YA  MTWARA KABLA YA KUNUFAISHA MIKOA MINGINE  TANZANIA.

TAMKO LA NDUGU BENJAMIN WILLIAM MKAPA


 Katika wiki za hapa karibuni kumekuwa na mijadala na mazungumzo mengi
  kuhusu mikakati ya maendeleo ya mikoa ya Kusini hususan Mkoa wa Mtwara.

  Mazungumzo hayo yamekuwa na lugha kali na yameambatana, hatimaye, na
  maandamano na mikutano ya hadhara.  Kiini chake ni matumizi ya gesi
  iliyogunduliwa mkoani kwa ajili ya miradi au mipango ya maendeleo ya mkoa
  huo, mipango iliyopo mbioni kutekelezwa au inayotarajia kutekelezwa.

  Mwenendo wa mazungumzo, maandamano na mikutano ya hadhara imeelekea
  kuashiria shari na kuvunjika kwa amani.

Aidha vituko na kauli hizo zimekaribia kujenga kutokuelewana kati ya
  Viongozi wa Vyama vya Siasa na Serikali, kati ya wanachama wa vyama vya
  siasa na viongozi wao, kati ya wananchi na viongozi wa Serikali.  Mtafaruku
  huu haufai kuachwa uendeleee na kutishia usalama.  Mipango ya maendeleo
  siyo Siri.  Mikakati na mbinu za Utekelezaji wake siyo Siri.  Maelezo yake
  mazuri yanaweza kutolewa yakadhihirisha namna na kasi ambayo raslimali
  zitawanufaisha wananchi wa eneo zilizomo na Taifa zima.  Utekelezaji wa
  miradi unategemea masharti kadhaa, k.m. Uwapo wa mitaji na teknolojia.
  Lakini pia mwekezaji, awe Serikali au Sekta binafsi, atataka iwepo hali ya
  utulivu na usalama wa watu, hali na mali.  Hayo yatadaiwa na wawekezaji wa
  ndani na wa nje.  Vurugu, fujo, vitisho havivutii uwekezaji.

  Nikiwa Mwana Mtwara na raia mwema mpenda nchi, nimefadhaishwa sana na
  matukio haya ya siku za karibuni Mtwara.  Kwa sababu hiyo natoa wito kwa
  wadau wote wa maendeleo ya Mtwara kusitisha harakati hizi na maandamano na
 mihadhara na badala yake wajipange *KUKAA PAMOJA* katika meza moja, kupitia
 historia, kutathmini mipango, kuchambua kwa kina mikakati ya utekelezaji
  wake, na hatimaye kufikia muafaka wa Ujia wa maendeleo. Fujo, vitisho,
  kupimana nguvu na malumbano kamwe si masharti ya maendeleo.  Mazungumzo
  yataboresha sera, ya uwekezaji ya mkoa na nchi.

  Linalowezekana leo lisingoje kesho.

  Benjamin William Mkapa
 *Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania*

No comments:

Post a Comment