Wanachama 1,550 wa CCM watimkia CHADEMA
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana kikiadhimisha miaka 34 tangu kianzishwe, zaidi ya wanachama wake 1,550 wamekihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Katibu wa CHADEMA wa Wilaya ya Maswa, Luhende Mipawa, alisema kuwa wanachama hao wamerudisha kadi hizo kwa wakati tofauti siku tatu tangu CCM ilipozindua maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa chama hicho.
“Tangu CCM walipozindua sherehe zao za kutimiza miaka 34, tumepokea wanachama wapatao 1,550 kutoka matawi mbalimbali ya CCM katika Wilaya ya Maswa ambao wamejiunga na chama chetu,” alisema.
Alisema kuwa dalili hizo zinaonyesha wazi wananchi wa wilaya hiyo walivyo na imani kwa CHADEMA wanachokiamini ndicho chama kikuu cha upinzani hapa nchini.
“Hizi ni dalili njema kuwa wananchi wanakikubali chama chetu ndiyo maana unaona kwa muda wa siku tatu tumevuna wanachama 1,550, tuna kazi kubwa ya kutimiza kiu kubwa ya wananchi wetu,” alisema.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, mmoja wa wanachama wa CCM aliyehamia CHADEMA, Geni Jilala, alisema kuwa kwa sasa chama hicho kimekosa mwelekeo na kupoteza misingi iliyowekwa na Mwalimu Nyerere na matokeo yake kimekuwa ni cha kuwatumikia wenye fedha huku wanyonge wakiachwa, hivyo CHADEMA ndiyo chama mbadala.
“CCM ya leo inawakumbatia wenye fedha, kwani ndiyo wana sauti ndani ya chama, sisi wanyonge tumeachwa, hivyo tumeona heri tukimbilie CHADEMA ambacho ndicho chama cha wanyonge,” alisema Jilala.
Aliongeza kwamba kutokana na mgawanyiko na makundi yanayokitafuna chama hicho wilayani humo, kuna hatari ya kusambaratika na kubaki na jengo la ofisi. Hivi karibuni Katibu wa Uenezi wa CCM Taifa, Kapteni John Chiligati, alishindwa kuhutubia mkutano wa hadhara mjini Maswa katika viwanja wa MADECO, baada ya wananchi kutojitokeza kwa madai kuwa chama hicho hakina jipya la kuwaeleza wakazi wa mji huo.
No comments:
Post a Comment