Kwanini Rais Kikwete ameanguka tena? Habari hii imehifadhiwa humu 22/8/2010
Ansbert Ngurumo
NATOA pole kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye ameanguka tena jukwaani jana (21/8/2-2010).
Namuombea apone haraka, aweze kuendelea na majukumu yake, na kutafakari upya uzito wa ujumbe wa makala za safu hii ya Maswali Magumu.
Aamini kwamba safu hii inalenga kumsaidia kwa kumfikishia ujumbe mzito ambao wasaidizi wake wanaogopa kumpatia.
Ajue pia kwamba tunapomuonya yeye au wasaidizi wake, dhidi ya mambo fulani, hatusukumwi na chuki binafsi, bali uzalendo; mapenzi yetu kwa nchi yetu. Na baada ya tukio la jana, la rais kuanguka tena (mara ya nne), jukwaani akiwa anahutubia kwenye viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, imenilazimu kuwahoji tena madaktari wake, kwa kuwakumbusha hoja niliyoitoa katika makala ya Oktoba 11, mwaka jana.
Nilitilia shaka taarifa ya daktari; nikahisi imetolewa kisiasa, si kitabibu. Nikahoji, Rais Kikwete akianguka tena, daktari wake atatuambia nini? Nairudia. Isome.
Naandika kwa uangalifu mkubwa kwa sababu mada yenyewe ni nyeti, kuhusu mjadala uliotawala wiki hii juu ya afya ya Rais Jakaya Kikwete, hata baada ya ofisi yake kujitetea na daktari wake kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari. Wananchi wamekataa kunyamaza. Kwa nini?
Ni vigumu kuwanyamazisha watu na si vema kuwanyamazisha, wanapojadili suala gumu na zito kama hili. Na hapa si tu kwamba wanajadili, bali wanamjali rais wao; na wanaipenda nchi yao.
Na katika hili hatugombani na rais hata kidogo. Tunamfariji. Rais ni mgonjwa kwa daktari wake; ni kiongozi kwa wananchi wake. Ingawa ugonjwa wa rais ndiyo ajira ya daktari wake, naamini kwamba sote, na daktari akiwamo, tunaguswa sana na msukosuko wa kiafya unaomgusa rais kwa namna yoyote ile.
Na inapofika mahali ofisi ya kiongozi mkuu wa nchi ikatoa idhini kwamba daktari wake azungumze hadharani kuhusu afya ya mgonjwa wake, ujue kuna tatizo kubwa.
Lakini kubwa ninaloliona hapa ni kwamba kisaikolojia rais amefedheheshwa na matukio ya kuzidiwa na kudondoka hadharani pamoja na lile la kuishiwa nguvu hivi karibuni jijini Mwanza, na njia mojawapo ya kuyakabili na kupunguza porojo juu ya afya yake ni kufanya hiki walichofanya wiki hii.
Binadamu yeyote mwenye akili timamu na moyo wa utu, atamuonea huruma rais wetu, atamtakia mema na hata kumwombea apone (hata kama wanatuambia hana tatizo). Ndivyo tunavyofanya sasa. Lakini kuna jambo la ziada.
Tuna ugomvi na wasaidizi wa rais. Hatuwezi kuwaacha wamdhalilishe na kumfedhehesha kiongozi mkuu wa nchi, halafu wakatoa taarifa za kujisafisha. Wakitaka kutoa maelezo rasmi wajiandae vizuri zaidi.
Katika blogu yangu ya Kiingereza (www.ngurumo.wordpress.com) nimelijadili suala hili kwa kifupi, nikisisitiza kwamba kiongozi wa nchi hapaswi kuzidiwa na kuanguka hadharani; na nikatoa mifano ya wachache waliovunja kanuni hii, Rais Kikwete akiwamo.
Nimedokeza pia kwamba kuzidiwa kwa Rais Kikwete akiwa anahutubia umati wa waamini wa Kanisa la African Inland (AIC), Mwanza, lilikuwa tukio la tatu ninalokumbuka kumpata hadharani ndani ya miaka 12.
Alipokuwa waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, aliwahi kuzidiwa ghafla mwaka 1997 katika Uwanja wa Ndege wa Brussels, Ubelgiji, akiwa njiani kuelekea Cuba. Ilibidi alazwe kwa saa nane kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari.
Tunakumbuka pia kilichomtokea mwaka 2005, siku moja kabla ya Uchaguzi Mkuu; alipozidiwa ghafla na kudondoka kutoka jukwaani, akakatiza hotuba yake katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam. Viongozi waandamizi waliokuwapo, wanausalama, wanahabari na wananchi waliokuwa uwanjani na hata waliokuwa wanafuatilia katika redio na runinga, walipata mshtuko mkubwa.
Baada ya ‘mgonjwa’ kupewa huduma hospitalini, aliweza kuzungumza na vyombo vya habari akiwa nyumbani kwake, akasema alianguka kwa sababu ya uchovu wa kampeni, na kwa kuwa siku hiyo alikuwa amefunga. Naamini tukio hilo lilimpatia pia ‘kura za huruma.’
Sijui tukio jingine la kuanguka kwake hadharani au faragha, lakini hili la Mwanza la juzi, lilikuwa la tatu. Kwa serikali iliyo makini, na kwa wahudumu wanaotaka tuwaamini kwamba wanatimiza wajibu wao katika kumhudumia kiongozi mkuu wa nchi, tukio la Mwanza lilipaswa kuepukwa.
Wanaofanya kazi kwa karibu na rais wamekuwa wakisimulia jinsi ambavyo katika miezi yake ya awali ya utawala wake, alikuwa akipatwa na hisia mbaya kila alipokumbuka anguko la Jangwani.
Fedheha ya kuanguka hadharani ilimnyima imani ya kujiamini mbele ya umma, kiasi kwamba alikuwa akizungumzia mara kwa mara kwa utani ili kuliondoa kwenye hisia chafu.
Miaka minne baadaye, linapomtokea tukio jingine linalofanana na hili katika mazingira ya jukwaani mbele ya umma, linamtonesha vidonda na kumdhuru kisaikolojia. Kujiamini kunatoweka tena.
Hawezi kusema hadharani, lakini sasa hivi rais anapaswa asaidiwe kuondokana na hofu ya kusimama hadharani.
Baada ya yote yaliyotokea, haitoshi kauli ya daktari wa rais kwamba “tumejifunza, na tunaahidi kuwa waangalifu zaidi”, inaeleza kwamba anatambua kosa lake na wenzake, lakini haitoshi.
Wanapaswa wafanye jambo la ziada la kumuimarisha rais mwenyewe kimwili na kisaikolojia. Bila hivyo, ataanguka tena, na tutaambiwa “hana tatizo la kiafya.”
Haitoshi kabisa kusema kwamba rais hana tatizo lolote la kiafya, bali uchovu pekee ndio umesababisha matukio yote hayo.
Tunavyojua, kwa kawaida, watawala na wanajeshi hawaanguki hovyo hovyo - tena hadharani. Si kawaida, ni aibu, na haitarajiwi kwa watawala na wanajeshi kuzidiwa na kuanguka hadharani.
Inakuwaje Amiri Jeshi Mkuu, mtawala na mwanajeshi kitaaluma azidiwe na kudondoka mara kadhaa, halafu wasaidizi wake wanacheka cheka na kusema hakuna tatizo? Wanamdanganya yeye au wanatudanganya sisi?
Si tu rais ni mwanajeshi, bali anatunzwa kama mtoto - anakula vizuri, anapimwa afya kila mara, analala pazuri, anasafiri kwa raha katika daraja la juu kwenye ndege, anafunguliwa hata mlango wa gari, anapangiwa ratiba ya kazi, anapangiwa hata muda wa kulala.
Ndiyo, anafanya kazi zinazoweza kumchosha akili lakini hayuko peke yake.
Rais wetu si dhaifu kama wananchi wake ambao wengi wanalala au kushinda njaa; wanapata mlo mara moja moja (na wenyewe haujakamilika virutubisho); wanafanya kazi nzito na ngumu zinazokula nguvu ya mwili na akili; wana pato duni sana (chini ya shilingi 1,000 kwa siku); wanakabiliwa na magonjwa hatari na hawana huduma ya matibabu inayoeleweka na inayoaminika; wanaishi katika mazingira hatari; wanakabiliwa na magonjwa sugu kwa miaka mingi; wanatembea kwa miguu au baiskeli, Bajaj au wanasafiri kwa malori na mabasi mabovu; hata kwa wanaosafiri kwa ndege, wanatumia madaraja ya chini yanayochosha; wanalala kwa saa mbili au tatu kila siku; wanasumbuliwa na umaskini wa kutisha kiasi kwamba kila wanapolala hawana tumaini kama wataiona kesho.
Watanzania hawa hawazimii, hawaishiwi nguvu wala hawaanguki, aanguke rais mwenye afya isiyotetereka (kama tulivyoelezwa) na mwenye matunzo ya viwango vya juu? Hapa ndipo kuna swali kuu ambalo daktari wa rais, Dk. Peter Mfisi, hajalijibu.
Na ingawa tunajua kuwa afya ya mgonjwa ni siri yake na daktari wake, kwa kuwa Dk. Mfisi amepewa ruhusa na mteja wake (rais) kutangaza taarifa hiyo, alipaswa kujua kwamba ripoti yake ingeibua maswali mengine yaliyofichika.
Kwanza, wapo wanaosema amekwenda mbali kuliko alikopaswa; kwamba ingetosha tu yeye kutoa tamko kwamba rais anaumwa nini, au kwamba haumwi bali amezidiwa kutokana na uchovu tu.
Kauli hiyo pekee kutoka kwa daktari wa rais ingekuwa na uzito wa kutosha, na labda ingeibua maswali machache zaidi.
Pili, uungwana wa kawaida unatulazimisha kukubaliana na daktari, maana sisi hatuna taarifa za ziada.
Lakini kwa kuwa daktari na mteja wake wamewasiliana na sisi kwa kutumia taarifa ya kisiasa kupitia vyombo vya habari; wala hakuna mwanahabari au mwana taaluma mwingine aliyeonyeshwa faili la afya ya rais, wananchi wana haki ya kuendelea kujadili suala hili na kuhoji maswali zaidi, hata yanayoudhi. Tusiwachukie. Tuwavumilie.
Hili la kuchoka na kuzidiwa si kosa binafsi la rais, bali ni la wasaidizi wake, ingawa naye ana uamuzi wa kufanya au kuacha jambo lolote analopangiwa. Washauri wa rais katika fani mbalimbali lazima walinde heshima yao kwa kuzingatia kwamba wao ni wataalamu wa maeneo husika.
Rais anapaswa awasikilize wao wanapomshauri kwa kuwa ndio wataalamu aliowateua au aliokabidhiwa. Ni makosa makubwa rais kudhani kwamba wataalamu waliomzunguka ni matarishi wa kumbebea mafaili na kuimba vibwagizo vyake kwa madhumuni ya kisiasa.
Yeye mwenyewe amekiri kwamba walimshauri akawagomea. Tungetarajia mambo mawili: kwanza, wataalamu hao wangelinda heshima ya taaluma zao kwa kujiuzulu kazi, kwa sababu hawana sababu ya kufanya kazi ya kumshauri kiongozi asiyeshaurika. Hawana kazi ya kufanya Ikulu.
Pili, baada ya tukio la Mwanza, rais alipaswa awawajibishe, kwamba wameshindwa kummudu na kumlindia afya na heshima mbele ya umma.
Bahati mbaya, kama ilivyo kawaida yake, badala ya kuwawajibisha kwa kumfedhehesha, amewatetea!
Wamepata bahati ile ile wanayofaidi mafisadi wanaocheka vizuri na wakubwa - kulindwa.
Matarajio yetu ni kwamba wasaidizi wamejifunza, lakini wajue bado wananchi wanahoji: Kama rais ni mzima kiasi tulichoelezwa, mbona anazidiwa na kuanguka? Kama ni uchovu tu, na kama wanasema wamejifunza, watatuambia nini iwapo rais atazidiwa tena hadharani kwa mara ya nne?
Imetokea. Sasa wana majibu? Bado wasaidizi wako Ikulu wanakula kuku?
No comments:
Post a Comment