Sunday, February 28, 2010

K U Z E E K A

KUZEEKA - imechangiwa na dr. Wilbert Bunini Manyilizu wa Chuo Kikuu, Mzumbe, Tanzania.

* Kila mmoja anazeeka/ataazeeka

* Kuna tabia za kimwili na kiakili zinazoambatana na mchakato huu usioepukika wa kuzeeka

* Kasi ya kuzeeka hutofautiana kutoka mtu hadi mtu kutokana na sababu mbalimbali za kimaisha, mazingira, tabia, vyakula na kadhalika.


MABADILIKO YA KIMWILI WAKATI WA MKCHAKTO WA KUZEEKA

Tabia za kuzeeka Mwili huonekana mapema zaidi kuliko zile za kisaikolojia.
Uzee huanza lini?
Unapozaliwa tu unaanza kuzeeka. Japo kuzeeka halisi ni pale kukua kunapokoma.
Mchakato wa kuzeeka haraka au taratibu hutegemea mtu binafsi.
Uzee huja kwa kasi tofauti kati ya mtu na mtu na kwa viwango tofauti kati ya kiungo na kiungo katika mtu huyo huyo.
Kwa nini mtu anazeeka?
Nadharia za sayansi za mchakato wa kuzeeka zinaeleza kuwa:

1. Kadiri siku zinavyopita kuna upotevu wa chembe chembe zinazotengeneza mwili hasa mtu anapokuwa ametoka kwenye utoto au ujana na anaposimama kukua. Hii ni hali ya kurithi ambayo kila mtu ameumbwa nayo.

2. Baadhi ya chembe chembe kama vile zile za damu za ngozi, ubongo nakadhalika hazigawanyiki tena ili kuongezeka (yaani hakuna kukua tena).Kukua maana yake ni kuongezeka wingi wa chembe chembe za mwili na ubongo kunakotokana na kugawinyika kwake.

3. Chembe chembe kama za neva za fahamu, misuli nakadhalika zinapopotea kwa kuzeeka na kufa kunakotokana na kushindwa kugawanyika, hupotea milele.

4. Viunganishi ( ni kama jointi za matofali ya nyumba= matofali ni chembe chembe) vya chembe chembe za mwili katika viungo vyote kama vile kwenye ngozi, misuli, ubongo nakadhalika. Tishu hizi ambazo ni viunganishi vya chembe chembe hukakamaa na kupoteza uwezo wake wa asili na kukatika kwa kukomaa, hivyo kubakia jointi dhaifu kwa kuunganisha chEmbe chembe. Hii huonekana wazi sana kwenye ngozi inapozeeka na kubakia tepetepe.

Pia tukumbuke kuwa takataka au makapi yanayotokana na michakato mbalimbali ndani ya mwili huharakisha kuzeeka kwa chembe chembe kwa kuwa na sumu na kemikali ambazo hazikutolewa kwa wakati na hivyo huchangia kuzeesha na kuchosha chembe chembe na kuzifanya zife kwa kukosa huduma bora zikilinganishwa na zile chembe chembe zisizozeeka.

MABADILIKO YA KAWAIDA YA MCHAKATO WA KUZEEKA

MACHO

1. Macho huanza kuonesha dalili za kushindwa kuona vizuri kati ya umri wa miaka 30 mwishoni na 40 mwanzoni. Macho huendelea kupungua nguvu zaidi na zaidi kadiri mtu anavyoendelea kuzeeka. Mtu hulazimika kukunja uso au kuweka ukurasa wa maandishi mbali akijitahidi kuona vizuri.

2. Kadiri mtu anavyozeeka lensi ya jicho hupoteza uwezo wake wa kulengesha mwanga unaotoka nje ya jicho kwenda kwenye retina ambako ndiko kuliko mlango unaoenda kwenye ubongo kunakotoa tafsiri ya kitu kilichopo mbele ya macho kama ni mtu, gari, mti na kadhalika.

3. Ukubwa wa tundu dogo linaloonekana jeusi kwenye jicho (pupil) hupungua kwa kukakamaa sababu hupoteza mnyambuliko (flexibility) kadiri mtu anavyozeeka hivyo kuruhusu mwanga kidogo sana kupitia lensi kwenda kwenye retina. Hivyo mtu hujaribu kukodoa macho na kukunja uso ili kuruhusu mwanga mwingi bila mafanikio kwani uzee ndio ulioleta matatizo hayo. Tatizo hili mtu huliona zaidi anapokuwa akiangalia kwenye mazingira ya mwanga mdogo sana kama vile anapoendesha gari usiku. Macho huchoka sana na uso huanza kuzoea kukaa katika mkazo huo na hatimae huanza kubadilika uso na kuwa na makunyanzi tofauti na wakati wa ujana wakati hapakuwa na ulazimishaji wa kuona.

4. Ulengaji wa kuona na kulenga (focusing) hupungua mtu anapozeeka na usahihi wa kuona kitu kwa mipaka, rangi na sura kwa uzuri hupungua. Uwezo wa kuona vitu vya pembeni vya jicho pia hupungua na kumlazimisha mtu huyu kugeuza shingo ili kuona kitu ambacho angeona bila kugeuza shingo, hasa wakati wa giza.

5. Uwezo wa kuona rangi pia hupotea kidogo kidogo kadiri ya umri unavyosonga mbele.

MASIKIO

1. Hupoteza uwezo wa kusikia sauti kali bali nafuu huwepo kama sauti zikiwa kubwa lakini za pichi ya chini.

2. Sauti ambayo wazee husikia vizuri wakati mwingine huonekana kero kwa vijana walio na masikio yanayosikia vizuri.

3. Maneno yakichanganywa na muziki na sauti zingine kidogo husababisha tatizo la kutokuelewa ujumbe kwa kadiri mtu anavyozeeka. Huwapo nafuu ya kuelewa na kufuata maongezi kama vyombo vya sauti zingine tofauti na maongezi vitazimwa kwa ajili ya mzee. Vyombo hivyo ni kama redio, runinga, ngoma au maongezi pembeni.

4. Vitu hivi kama vitaendelea kusikika huleta ghadhabu ya haraka na tafsiri tofauti kwa mzee kama vile huonesha kumdharau, kutokumheshimu na kadhalika.

5. Matokeo yanayojitokeza kwa mzee kwa kutokuzingatia haya ni pamoja na mzee huyo kutofurahia maongezi, kuzira (Kususa), malalamiko, kujitenga na kujenga dunia ya upweke. Hamu ya chakula hupotea na afya hudhoofu zaidi. Mzee huyu huendelea kuumia ndani kwa ndani na hivyo kinga yake dhidi ya maradhi huporomoka kwa kasi kutokana na msongo wa mawazo ambayo ni matatizo ya akili. Vyote hivi huongeza kasi ya kuzeeka na hatimaye kupoteza maisha.


LADHA YA CHAKULA NA HARUFU

1. Milango ya kupokea Ladha ya chakula hudhoofika na kushindwa kupeleka taarifa za ladha ya chakula kwenye ubongo kwa kadri mtu anavyozeeka. Hii hujitokeza mtu anapofikia miaka ya hamsini, hii huendelea hivyo hadi miaka sabini ambapo wazee wengi hupoteza sehemu kubwa ya milango hii na hivyo kuwa na matatizo ya kula.

2. Tatizo kubwa la wakati wa uzee ni ulaji wa tabu ambao husababisha afya kudhoofika sana hasa wasipokuwa na wasimamizi wa utaratibu wa chakula na aina za vyakula wapendavyo wazee wenyewe.

3. Matatizo ya ulaji yanaweza kuwa makubwa sana kama kuna tatizo la upendo na huduma hafifu anazoona mzee. Wazee huzira kwa urahisi wanapoona hawathaminiwi na kujiona hawana faida na kuona heri wafe badala ya kuendelea kusumbua watu. Hulalamika, hukata tamaa na kupoteza hamu ya kula. Hali hii pia huathiri milango ya ladha ya chakula.

4. Uwezo wa (kunusa) milango ya kupokea harufu nzuri na mbaya ya chakula kudhoofika na kushindwa kugundua chakula kizuri cha kutia hamu ya chakula.

No comments:

Post a Comment