Imechangiwa na Mwalimu Bashiru Ally wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 17/10/2009.
Wanambongi, salaamNaomba nami kuchangia kidogo mjadala kuhusu swala la mpasuko katika Tanzania. Kwa maoni yangu mpasuko katika jamii yetu upo. Mpasuko huu unajibainisha katika sura nyingi kama vile pengo kubwa katika kipato cha chini na wenye kipato cha juu. Katika lugha ya kisasa mpasuko huu unajibainisha zaidi kwa jina la umaskini. Kwa mda mrefu tumekuwa tukipambana na umaskini, ingawa umaskini unaongezeka. Mbinu za kila namna zimetumika ikiwa ni pamoja na kuweka vigenzo na viwango vya umaskini. Hivi sasa wapo maskini wakubwa na wadogo, maskini wa kike na kiume, maskini wa mjini na wa vijijini, maskini mwenye njaa na masikini wa kipato, maskini anayeishi katika mazingira hatarishi na kadhalika.Mifuko ya uwezeshaji imeanzishwa, taasisi za fedha za kukopesha maskini zimeanzishwa, mafunzo ya ujasiriamali yameendeshwa hadi vyuo vikuu. Yote haya hayapunguza kiwango cha umaskini Katika kutafuta majibu ya kwanini umaskini unaongezeka ingawa vita dhidi ya tatizo hili inapamba moto, UFISADI ukaonekana kuwa ndio chanzo kikuu cha kuongezeka kwa umaskini nchini. Wakajitokeza wannchi kutoka katika kada mbalimbali kupambana na ufisadi. Kadri mapambano hayo yanavyozidi kupamba moto ufisadi kama ulivyo umaskini unaongezeka na hivyo kuongeza zaidi umaskini. Tatizo ninalolipata katika vita dhidi ya ufisadi ni kwamba mapambano dhidi yake hayalengi kukabiliana na vyanzo vikuu vya ufisadi pamoja na vikwazo vya mapambano ya ufisadi. Hata mapambano ya umaskini nayo yanakabiliwa na tatizo kama hili.Kama alivyosema Kweka, hakuna mkakati wa kuwaunganisha wananchi ambao ni waathirika na umaskini na ufisadi ili washiriki katika mapambano dhidi ya maadui wa maendeleo yao. Mikakati iliyopo inawagawa zaidi wananchi na kuwakatisha tamaa. Ninaamini kwamba bila ya ushiriki wa wananchi wengi, ushindi dhidi ya umaskini na ufisadi hautapatikana. Umoja unaotakiwa hauwezi kejengwa misikitini wala makanisani kupitia matamko na miongozo au Ilani za kidini. Hata kama nia ya viongozi wa dini ni njema, miongozo yao haiwezi kupata uhalali wa kisiasa kwa kiwango cha kuvuka mipaka ya nchi au kukabiliana na upinzani kutoka katika makundi yanayonufaika na kushamiri kwa ufisadi na umaskini. Ni vyema tukatambua kwamba matatizo ya umaskini na ufisadi ni dalili ya ukosefu wa mfumo mbadala wa kisiasa na kiuchumi. Hili sio Tatizo la Tanzania peke yake bali ni tatizo la nchi zote za dunia ya tatu.Kwa hiyo mapambano dhidi ya mfumo huu yanapaswa kuwa na sura ya kisiasa katikangazi ya kitaifa na kimataifa. Ingefaa sana tukapanua mjadala wetu na kuupa sura ya kisiasa ambayo itayasambaza mapambano haya nchi nzima na pia kuyaunganisha na mapambano yanayoendelea kwingineko.Hivi ndivyo mifumo ya ukoloni na ukaburu ilivyosambaratishwa. Kila mtu bila kujali dini, rangi, jinsia,tabaka au kabila alishiriki kupambana na ukoloni na ukaburu. Ikiwa tutashindwa kufanya hivyo, mda sio mrefu mapambano haya yatakuwa na sura ya ukabila na udini. Swali kuu hapa la kujiuliza ni kwa vipi mshikamano wa kitaifa na kimataifa dhidhi ya mifumo ya kifisadi itajengwaje? Mkakati wa kwanza ni kuendeleza mijadala KUHUSU MBINU MUAFAKA ZA KUJENGA MSHIKAMANO miongoni mwa wanachi kitaifa na kimataifa na kuiieneza mijadala hii zaidi kadri iwezekanavyo. Mkakati wa pili ni kuunda vikundi huru vya kiraia vyenye malengo ya kisiasa ya kupambana na mifumo ya kifisadi popote pale ufisadi ulipo. Vikundi hivi viendeleze mapambano dhidi ya ufisadi wa kiuchumi (wizi wa kimataifa wa raslimali zetu kama ardhi na madini); Ufisadi wa kidini( kuzifanya huduma za kiroho na kijamii kuwa biashara); ufisadi wa kijamii(makuadi wa soko huria, unyanyasaji wa wanawake na watoto): Ufisadi wa kisiasa(Wizi wa kura, uroho wa madaraka,rushwa,udini, ukabila); Ufisadi wa kisomi (Woga na unafiki wawasomi). Ili tuweze kufika huko uongozi wa kisiasa, kisomi, kidini na kijamii utahitajika. Hata hivyo mshikamano wa wananchi ndioutakaotuwezesha kupata uongozi mzuri ambao wengi wanaona haupo. Viongozi wazuri wanazaliwa na kutayarishwa. Pengine tuanze pia kujadili namna ya kuwapata viongozi wazuri. Ila mjadala huo uwe mpana na uwe wazi.Mikakati ya kidini kuhusu hatima ya nchi maskini haiwezi kupata uhalali wa kisiasa na haitekelezeki.
No comments:
Post a Comment