Tuesday, November 8, 2011

ATI? WATANZANIA WANATAMANI KUWA WAMAREKANI !!! WATUULIZE TULIOFIKA NA KUISHI HUKO !!!

Watanzania wanatamani kuwa Wamarekani
Saturday, 05 November 2011 21:31


Na Assumpta Nalitolela, Gazeti la Mwananchi, Tanzania.

KUIGA kutoka kwa mtu aliyefanikiwa ni jambo jema, tena linakubalika pale ambapo mbinu safi zilizomfanya mhusika afanikiwe, ndizo zinazoigwa. Hivyo hata katika biashara, mtu anatakiwa ailinganishe biashara yake na ile yenye mafanikio na aangalie ni kipi anaweza kuiga na kukiingiza kwake ili naye apate mafanikio.

Vijana wanaaswa waige kutoka kwa watu wazima ambao wamekuwa na mafanikio ili nao wafuate nyayo. Hivyo kuiga kupo na ni jambo jema. Kwa kulikazia hilo kuna msemo kwamba ‘‘kwanini uhangaike kuunda gurudumu wakati tayari kuna mtu aliyekwisha liunda?’’ Huko ni kupoteza raslimali muda ambayo inahitajika sana kwa mambo mengine ambayo katika dunia hii yapo mengi.

Hivyo kuiga kwa ajili ya maendeleo mimi hakunisumbui, kinachosumbua moyo wangu ni kuiga kulikopitiliza kiasi kwamba mtu anatamani sio tu kuiga bali awe nakala ya huyo mtu anayemuiga. Kama ni suala la mtu moja moja tunaweza kusema mtu anaiga kwa kiasi ambacho anatamani kuwa nakala ya mtu mwingine, hiyo ni kumkosoa Mungu kwa kukuumba kama ulivyo.

Sijui tusemeje kama ni taifa ndilo linalotamani kuwa taifa jingine katika nchi yake yenyewe. Hapa ndipo tulipofikia Watanzania. Tunapenda kuwa Wamarekani tukiwa ndani ya Tanzania. Hali hii ipo toka kwa wasomi mpaka wasioingia darasani, taasisi binafsi mpaka zile za umma, wasanii mpaka wale wa fani zingine. Tulitafakari hili.

Sarafu ni alama moja wapo inayotambulisha taifa. Matumizi ya sarafu katika biashara kwa wakazi wa mahali fulani yanamuongoza mtu kusema kwa uhakikia kwamba, yupo kati ya watu wa taifa fulani.

Hivyo kama ni Shilingi ya Kenya, anajua kwamba yuko ndani ya mipaka ya Kenya. Kama ataigundua kuwa ni Shilingi ya Tanzania basi atajua yuko ndani ya mipaka ya Tanzania.

Umezuka mtindo ambao unakera kweli kweli; na nashukuru umma wa Watanzania umeanza kuupigia kelele, nao ni baadhi ya watu au taasisi kudai malipo kwa Dola ya Marekani badala ya shilingi kwa bidhaa na huduma wanazotoa. Hivi bila aibu mtu au taasisi inamdai Mtanzania kulipia bidhaa au huduma kwa dola katika nchi ya Tanzania, azitoe wapi na yuko kwenye uchumi wa shilingi?

Cha ajabu, haya yanafanywa hata na vitengo vya vyuo na shule ambako ulitegemea kuna wasomi wenye kuelewa vizuri kwamba sarafu ya nchi hii ni shilingi na kwamba ni shilingi ndio inayotakiwa kulindwa kwa sababu ndio yetu.

Shilingi ndio inayotutambulisha utaifa wetu. Sasa hata wasomi wanapokataa kuipokea maana yake nini? Kwamba tuingie kwenye mchakato wa kubadilisha sarafu ili tutumie Dola ya Marekani na Benki Kuu yetu iwe hiyo ya Marekani? Wasomi hawa wanatambua kwamba kudai kwao malipo kwa dola kunazidi kuizorotesha shilingi, cha ajabu hili haliwasumbui.

Natambua uimara wa dola na utamu wake katika biashara kwa mtu anayeipokea lakini hiyo sio yetu. Tutafute mbinu za kuimarisha ya kwetu. Kuibeza pesa yetu kwa kuwa ni hafifu, ni sawa na mtoto kumbeza baba yake kwa kuwa hali yake hailingani na baba wa nyumba jirani.

Jambo lingine linaloonesha matamanio yetu ya kuwa Wamarekani ni mahangaiko ya vijana wetu ya kuwa na lafudhi ya Kimarekani na kuikataa ya makabila ya Kitanzania. Lafudhi hujengeka katika matamshi ya mtu kwa muda mrefu sana. Mtu hujengeka kwa lafudhi ya jamii inayomzunguka kipindi anachokua. Hivyo akikuzwa katika mazingira ambayo watu wanazungumza kwa lafudhi ya Kihaya ya kwake pia itakuwa ya Kihaya, vivyo hivyo Kinyakyusa, Kingoni nk. Baada ya kujengeka sio rahisi kutoka.

Lafudhi sio kitu kibaya, hiki ni kitambulisho cha jamii aliyotoka mtu. Kuikataa lafudhi ni kuikana jamii iliyomkuza. Vijana wanahangaika kutumia lafudhi ya Kimarekani wakati wanapoongea Kiingereza kiasi kwamba wanaishia kumung’unya maneno, yasiyoeleweka.

Hawaeleweki kwa sababu wanajaribu kuzungumza kwa namna ambayo sio wao. Lafudhi ya mtu ipo palepale haijalishi kama mtu huyo anaongea Kiswahili, Kingereza, Kichaga nk. Hivyo mtu anapojaribu kuibadilisha kwa kuwa tu anaongea lugha ya mtu mwingine, lazima itampa shida, na ataishia kuchekesha watu.

Uigizwaji wa lafudhi tunawaachia wasanii katika michezo ya kuigiza kwani lengo lao ni kutuchekesha. Kwa lafudhi yako mtu unajulikana unatokea upande upi wa dunia, kwa lafudhi yako unapendeza, kwa lafudhi yako mtu unajiamini zaidi unapoongea, lakini kwa lafudhi ya mtu mwingine unachekesha na hueleweki. Yanini mtu uishie kuwa kichekesho wakati hiyo haikuwa nia yako?

Tunatamani kuwa Wamarekani mpaka tunapeperusha bendera yao katika nchi yetu. Kama ilivyo kwa sarafu, bendera pia ni alama ya taifa. Tanzania tunapeperusha bendera ya Marekani kwa kubandika kwenye mikokoteni, kuvaa kama vilemba, kuibandika kwenye daladala, kuitangaza kwenye fulana tunazovaa.

Hiyo ni kutamani kuwa Wamarekani , hiyo ni kasoro kubwa sana kwenye taifa letu ambalo tunasherehekea miaka 50 ya kuwa huru. Miaka 50 ya kuwa na bendera yetu wenyewe ambayo sasa tunaikana na kutamani kupeperusha ile ya Marekani.

Haya ni machache tu yanayoashiria kulikana taifa letu la Tanzania. Ukweli nchi yetu ni maskini na ni ukweli tuna kasoro nyingi za hapa na pale zinazorudisha maendeleo ya nchi nyuma, lakini kusahihisha kwake sio kwa kuikana kwa kuendelea kuzorotesha uchumi kwa kutumia sarafu isiyo yetu, au kwa kutumia lafudhi isiyo yetu au kwa kuukana uhuru wetu kwa kupeperusha bendera isiyo yetu.

Tuchangie kwa kuhakikisha nasi tunakuwa taifa ambalo wengi wa watu wake wanaishi maisha yenye neema. Tukosoane, tuwajibike na tuige mambo ambayo mataifa mengine wameyatekeleza na kuwafanya waneemeke. Lakini tubaki kama Watanzania. Kwa wale wanaoukana Utanzania wao basi wahame wakaishi na jamii za taifa hilo wanalolipenda .

Tukutane Jumapili ijayo panapo majaliwa.


CHANZO: MWANANCHI