Sunday, July 12, 2015

WALIOWEKEZA KATIKA MASHAMBA NA VIWANDA WAHIMIZWA KUVIENDELEZA !!!


WALIOWEKEZA KATIKA MASHAMBA NA VIWANDA WAHIMIZWA KUVIENDELEZA  !!!
Je,  haya yaliyoandikwa hapa yalitekelezwa ?
Angela Semaya, Dodoma
Daily News; Saturday,August 02, 2008 @00:03


Serikali  [ya Tanzania]  imetoa miezi miwili kwa watu waliopewa mashamba na viwanda vya mifugo vilivyobinafsishwa kuhakikisha wamewekeza na kuviendeleza kama ilivyoainishwa katika makubaliano ya mkataba wa uwekezaji. Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, John Magufuli alitoa mwito huo jana wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya matumizi ya fedha kwa mwaka 2008/09.

Magufuli alisema wale wote waliopewa mashamba na viwanda hivyo ambavyo havijaendelezwa au wanafanyia shughuli nyingine tofauti na makubaliano ya mkataba kuhakikisha wanawekeza katika kipindi cha miezi miwili ama sivyo watanyang'anywa na kupatiwa wawekezaji mwingine.

"Napenda kutoa mwito kwa wote waliopewa mashamba na viwanda hivyo ambavyo havijaendelezwa au wanafanya shughuli nyingine tofauti na makubaliano ya mkataba kuhakikisha wanawekeza katika kipindi cha miezi miwili ama sivyo watanyang'anywa na kupatiwa wawekezaji wengine wenye nia ya kuviendeleza," alisema.

Magufuli alisema ili kuhakikisha mashamba, miundombinu na huduma zilizokuwa chini ya wizara na kubinafsishwa zinaendelezwa na kufanya yaliyokusudiwa ilifanyika tathmini ya mashamba 58 na viwanda viwili. Alisema katika tathmini hiyo ilionyesha kuwa baadhi ya mashamba na viwanda havijaendelezwa kama ilivyotarajiwa na kwamba wizara inaendelea kufuatilia na kutoa ushauri unaohitajika.

Magufuli
alisema wizara imekuwa ikifanya kila juhudi kuendeleza zao la nyama wakiwemo ng'ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe, kuku na kwamba kwa mwaka 2007/2008 uzalishaji wa nyama uliongezeka kutoka tani 370,566 mwaka 2006/2007 na kufikia tani 410,706 sawa na ongezeko la asilimia 10.8.

Akizungumzia uvuvi, alisema bado kuna tatizo la uvuvi haramu uliokithiri katika Ziwa Victoria na kwamba kasi ya uvuaji wa samaki aina ya sangara ni mkubwa kiasi cha kutishia uvuvi endelevu wa samaki hao. Magufuli alisema pia wizara imepiga marufuku wavuvi wakubwa kuvua samaki aina ya kambamti kwa kipindi cha mwaka mmoja katika maji ya kitaifa kutokana na kupungua kwa rasilimali hiyo.

Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2008/2009, Mwadini Abbas Jecha, katika hotuba yake alisema wafugaji wadogo hawajapewa kipaumbele cha kutosha kwani hakuna mkakati wa kuhakikisha wanapewa mikopo, mafunzo, kutafutiwa masoko, miundombinu na nyenzo nyingine.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Gideon Cheyo, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na mjumbe wa kamati hiyo, Kaika Telele, alisema uwekezaji mdogo katika sekta ya mifugo na uvuvi umesababisha ukuaji mdogo wa sekta hizo kuliko inavyotarajiwa. Cheyo alisema pia uhaba wa viwanda vya kusindika mazao ya mifugo na uhifadhi wa samaki na mazao ya uvuvi, uzalishaji duni na ukosefu wa masoko ya uhakika kumepunguza mchango wa sekta hizo katika pato la taifa.

No comments:

Post a Comment