Friday, April 17, 2015

HOTUBA YA RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE DAR ES SALAAM, TAREHE 28 MACHI, 2015

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, WAKATI WA MAZUNGUMZO NA KAMATI YA HAKI NA AMANI YA VIONGOZI WA DINI MKOA WA DAR ES SALAAM, UKUMBI WA MIKUTANO WA JULIUS NYERERE, DAR ES SALAAM, TAREHE 28 MACHI, 2015

Posted by Sebastian Gabriel On April 01, 2015

Chanzo :Ikulu
Sheikh Alhadi M. Salum, Mwenyekiti wa Kamati ya Haki na Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es Salaam;
Mhasham Askofu Valentino Mokiwa, Kaimu Makamu Mwenyekiti,;
Fadha John Solomon, Katibu wa Kamati ya Haki na Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es Salaam;
Wajumbe wa Kamati ya Haki na Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es Salaam;
Viongozi wa Dini;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Shukrani

Nianze kwa kuungana na walionitangulia kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyetuwezesha kukutana siku hii ya leo tukiwa na afya njema. Nawashukuru Mwenyekiti na Katibu wa Kamati ya Haki na Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es Salaam kwa kunialika kushiriki nanyi katika mkutano huu maalum wa kutafakari afya ya jamii katika taifa letu. Hili ni jambo muhimu hasa wakati huu taifa letu linapopitia kwenye hali isiyokuwa ya kawaida.

Nawapongeza viongozi na wanakamati wote kwa juhudi kubwa mnazozifanya katika kuhakikisha kwamba taifa letu linabakia kuwa kisiwa cha amani. Hii si kazi ndogo hata kidogo. Ni kazi kubwa yenye vikwazo vingi. Inahitaji moyo wa ujasiri uvumilivu na wenye kuweka maslahi ya taifa mbele. Unahitaji uongozi wenye kuona mbali na wenye kujali maslahi mapana ya taifa letu na watu wake. Naamini ni kazi ambayo inampendeza Mwenyezi Mungu hivyo ina Baraka zake zote. 

Ndugu Viongozi wa Dini;
Kwenye mwaliko wenu mmenitaka nizungumzie mambo makubwa matatu; amani ya nchi, Katiba Inayopendekezwa na Mahakama ya Kadhi. Suala la usalama na amani ya nchi yetu nimekuwa nalizungumza mara kadhaa na mara ya mwisho nililizungumzia kwa kirefu kwenye hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa Februari, 2015. Leo nitalizungumzia suala la amani kwa kulihusisha na wakati tulionao na hasa mwelekeo wa mambo yanayotokea hivi sasa nchini. Huhitaji kuwa bingwa wa unajimu kuweza kujua kuwa hali ilivyo sasa hairidhishi na kama hatutachukua hatua thabiti kuubadili mwelekeo huu nchi yetu itaingia kwenye mfarakano mkubwa kati ya Wakristo na Waislamu. Hatari ya kuvunjika kwa amani ni kubwa.

Kama sote tujuavyo mchakato wa kutunga Katiba Mpya unakaribia ukingoni baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa Rasimu ya Katiba na Bunge Maalumu la Katiba kutunga Katiba Inayopendekezwa. Tunasubiri kupiga Kura ya Maoni ya kuamua juu ya hatma ya Katiba hiyo. Upigaji kura huo utaendeshwa kwa kutumia Daftari la Wapiga Kura lililoboreshwa na siyo la zamani. Kwa kuwa daftari linaboreshwa kwa kutumia teknolojia mpya kila mtu anapatiwa kitambulisho kipya cha mpiga kura. Kinachoendelea sasa ni zoezi la uandikishaji wa wapiga kura na litakapokamilika ndipo Kura ya Maoni itakapofanyika. 

Kwa sasa wengi wetu tunasubiri zamu yetu ya kujiandikisha ili tupate vitambulisho vyetu vya Mpiga Kura, ili kuwa tayari kutimiza haki yetu ya Kisheria na Kikatiba ya kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa na baadae kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani. Bahati mbaya kasi ya uandikishaji haijaenda kama tulivyotangaziwa awali na Tume ya Uchaguzi. Naamini wakati mwafaka Tume itatueleza na kutuelekeza kuhusu uandikishaji na mchakato mzima mpaka upigaji wa Kura ya Maoni. 

Waheshimiwa Viongozi wa Dini;
Katika kipindi cha kusubiri kujiandikisha katika Daftari la Mpiga Kura, kumetokea matamko ya baadhi ya viongozi wa dini ya kuwataka waumini wajiandikishe kwa wingi ambalo ni jambo jema sana. Lakini, pia wamewataka waipigie kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa. Kauli hii imenisikitisha na kunihuzunisha kwa sababu sikutegemea viongozi wetu hawa tunaowaheshimu sana wangeweza kufanya hivyo na kwa namna ile waliyofanya. Ninaposema hivyo sipendi nieleweke kuwa nahoji haki yao kama raia kutoa maoni ya kuunga mkono au kutokuunga mkono Katiba Inayopendekezwa. Hiyo ni haki yao ya msingi kama ilivyo kwa raia ye yote. Kinachonisumbua ni kutaka kulipa suala la Katiba Inayopendekezwa ambalo ni la raia wote, sura, mtazamo na msimamo wa kidini. Kama ingekuwa Katiba Inayopendekezwa inakinzana na uhuru wa kuabudu hapo wangekuwa na haki ya kuikataa na mimi ningeungana nao kuipinga.

Ukweli ni kwamba Katiba Inayopendekezwa inatambua haki na uhuru wa watu kuabudu dini wanayoipenda. Niruhusuni ninukuu Ibara ya 41 ya Katiba Inayopendekezwa ambayo ina vifungu saba lakini ninanukuu vichache (1, 2, 3, 5 na 6) inasema kwamba: 

(1) Kila mtu ana uhuru wa mawazo, dhamiri, imani na uchaguzi katika mambo ya imani ya dini na anao uhuru pia wa kubadilisha dini, imani yake au kutokuwa na imani na dini.

(2) Kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari kwa mtu binafsi ili mradi hakiuki sheria za nchi.

(3) Shughuli ya uendeshaji wa jumuiya za dini itakuwa nje ya shughuli za mamlaka za Serikali.

(5) Ni marufuku kwa mtu, kikundi, au taasisi ya dini kutumia uhuru wa kutangaza dini kwa namna ambayo italeta uvunjifu wa amani, kujenga chuki au kuchochea vurugu na ghasia kwa madai ya kutetea imani au dini hiyo.

(6) Dini na imani ya dini haitatumika kwa namna yoyote iakayowagawa wananchi, kuleta uhasama au uvunjifu wa amani miongoni mwa wananchi.

Kwa kweli kulipa jambo la Katiba Inayopendekezwa sura, mtazamo na msimamo wa kidini linanipa taabu sana kuelewa. Nasumbuliwa na ule ukweli kwamba haijakiuka misingi yoyote ya dini, labda dini ya shetani kama ipo. Isitoshe mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya umekuwa na ushirikishwaji mkubwa na mpana wa watu katika hatua zote. Viongozi wa dini na waumini wao walishiriki katika hatua zote za mchakato. Haijapata kutokea mambo ya dini kupuuzwa au watu wa dini ye yote kubaguliwa. Katiba Inayopendekezwa imezingatia, imeimarisha, kudumisha na kuendeleza misingi muhimu ya taifa letu. Misingi hiyo ni pamoja na:

(i) Nchi yetu kutokuwa na ubaguzi wa aina yoyote, ubaguzi wa dini, rangi, kabila, jinsia au eneo mtu atokako.

(ii) Serikali yetu kutokuwa na dini ingawa wananchi wake wanaruhusiwa kuwa na dini.

(iii) Uhuru wa kuabudu. Kila Mtanzania anao uhuru wa kufuata na kuabudu dini atakayo bila kubughudhiwa. Uhuru huu umezingatiwa katika Katiba Inayopendekezwa.

(iv) Utoaji wa fursa sawa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wote bila upendeleo wala ubaguzi.

(v) Haki za msingi za makundi yote zimeainishwa.

Ndugu Viongozi wa Dini;
Ndugu Wageni Waalikwa;
Kwa ajili hiyo sioni sababu kwa nini viongozi wa dini wawaelekeze waumini wao kuipigia Kura ya Hapana, Katiba Inayopendekezwa. Kuna lipi la kidini au linalokwenda kinyume na haki na uhuru wa kuabudu? Nimeisoma na kuirudia sijaliona linalokwenda kinyume na dini yo yote. Kwa ajili hiyo nawasihi viongozi wa dini wawaache waumini wao kuamua wenyewe wanavyoona inafaa, bila ya kushinikizwa na mtu yeyote. Katiba Inayopendekezwa ni ya taifa letu na ya Watanzania wote. Tena walikuwa ni wawakilishi wazito, bora na makini kwa kila hali. Lipi tena lililoharibika hadi tufikie hapa?

Nilifuatilia kwa undani nini kilichowafanya viongozi wetu wa dini kutoa matamko ya kuwataka waumini wao kuikataa Katiba Inayopendekezwa na kutokuipigia kura CCM. Nimeona kuwa labda ni hasira kwa uamuzi wa Serikali kupeleka Bungeni Muswada unaohusu Mahakama ya Kadhi. Pia wana hasira kuwa Katiba Inayopendekezwa imeyaacha baadhi ya mambo wanayoyaona kuwa ni muhimu. Nitajaribu kuyazungumzia yote mawili, na namuomba Mwenyezi Mungu anijaalie kauli njema ili maelezo yangu yatosheleze kujibu hoja hizo.

Waheshimiwa Viongozi wa Dini;
Niruhusuni nianze na hili la pili la baadhi ya mambo waliyoyaona kuwa ya msingi kutokuwemo katika Katiba Inayopendekezwa. Niseme kwa jumla tu kwamba si kila alichokitaka kila mtu kimejumuishwa au kingejumuishwa. Isingekuwa rahisi kufanya hivyo. Tungekuwa na Katiba ya ukubwa gani na ingeandikwaje na nani angeiandika! Mchakato huu unaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kila taasisi au chombo kilichotakiwa kuundwa kwa mujibu wa Sheria hiyo kiliundwa na kutimiza ipasavyo wajibu wake. Wapo waliohoji Mahakamani mamlaka ya Bunge Maalumu la Katiba kuhusu Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Walipata majibu stahiki kuwa Sheria ilizingatiwa na Bunge maalum lina mamlaka hayo.

Sioni ubaya wa mtu kuyasikitikia yale ambayo yamemkereketa sana, lakini kuyapa sura, mtazamo na msimamo wa kidini inanipa taabu. Mambo ya dunia yanayotungwa na wanadamu hubadilika na nyakati, tofauti na maandiko matakatifu. Linaloonekana linafaa leo kesho siyo na linaloonekana silo leo kesho litaonekana ndilo lenyewe. Niliwahi kusema wakati mmoja kuwa kama jambo halipo sasa ipo siku litakuwepo. 

Mfano mzuri ni Orodha ya Mambo ya Muungano katika Katiba yetu ya sasa. Yalipoingizwa yalionekana yanafaa na yanahitajika sana, leo baadhi yameonekana hayajitajiki na ni kikwazo. Kwa mambo kama hayo kwa viongozi wa dini kuyawekea msimamo wa dini ni kwenda mbali mno. Waachieni wanasiasa walumbane na waumini wenu waamue wanavyoona inafaa. Mtawakwaza isivyostahiki.

Waheshimiwa Viongozi wa Dini;
Pengine niyasemee kidogo haya madai yahusuyo maadili. Napenda kuwahakikishia kuwa maadili ya taifa pamoja na miiko ya uongozi vimezingatiwa. Katiba Inayopendekezwa imeyaainisha vizuri maadili ya viongozi tena kwa namna inayotekelezeka na kuunda mifumo na vyombo vya kusimamia. Miongoni mwa vyombo hivyo ni pamoja na Tume ya Maadili tofauti na ilivyo sasa ambapo ni Baraza la Maadili. Katiba Inayopendekezwa inaitambua Sheria ya Maadili na TAKUKURU ambayo haikutajwa kabisa katika Rasimu ya Katiba ya Tume nayo imeingizwa. 

Kumekuwa na madai kwamba maadili ya viongozi na watendaji wa umma yameondolewa kwenye Katiba Inayopendekezwa. Hiyo siyo kweli. Ibara za 28 na 29 zinazungumzia maadili ya viongozi wa umma na Ibara ya 30 na 31 zinazungumzia maadili ya watendaji wa umma. Ibara ya 228 inaunda Tume ya Maadili ya Umma na Ibara ya 249 inaunda Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU). Kilichofanyika ni kuyaondoa maadili kutoka kwenye sehemu yaliyopendekezwa kuwekwa na kupelekewa sehemu nyingine ambako yanaweza kutekelezwa kwa mujibu wa sheria. Tume iliandika maadili kama Tunu tu ambazo kimsingi hazipaswi kutekelezwa bali kuzingatiwa tu. Bunge Maalumu la Katiba likaona liyajengee Mifumo ya Utekelezaji na vyombo vya kusimamia.

Hivyo ndugu zangu, Katiba Inayopendekezwa ni bora kuliko Katiba ya sasa na Rasimu ya Katiba. Katiba Inayopendekezwa isipopita, tunarudi kwenye Katiba ya sasa na changamoto zake. Ni vizuri sana ikaeleweka kuwa, chaguo ni kati ya Katiba Inayopendekezwa ambayo imeboreshwa na kukidhi mahitaji na maslahi ya makundi mbalimbali nchini au kubaki kwenye Katiba ya Sasa. Pamoja na hayo, tutambue kwamba Katiba si Biblia au Msahafu vitabu ambavyo haviwezi kubadilishwa. Zitakuwepo fursa mbalimbali za kuifanyia marekebisho kadri mahitaji ya wakati yatakavyojitokeza.. Tumekuwa tukifanya hivyo siku zote, sioni sababu ya watu kuhamanika na kuwa na mashaka safari hii. Kile ambacho hakikupatikana leo kinaweza kupatikana kesho.

Mahakama ya Kadhi

Ndugu Viongozi wa Dini;
Ndugu Wageni Waalikwa;
Kuhusu Mahakama ya Kadhi, ni vizuri tukaelewa kwamba Serikali ilishafanya maamuzi kwamba Mahakama hiyo haitaanzishwa na Serikali bali na Waislamu wenyewe wakiona inafaa. Tulielewana pia kwamba Serikali haitaingia gharama za kuiendesha. Hayo yote yamezingatiwa na Mahakama hizo zimekwishaanzishwa na BAKWATA, Makadhi wamekwishateuliwa na zinaendeshwa na Waislamu wenyewe. 

Tunachotaka kufanya sasa Bungeni ni kuwezesha maamuzi yanayofanywa na Kadhi yatambuliwe kisheria. Kwa mujibu wa Sheria zetu hilo siyo jambo geni na wala halikinzani na Katiba wala Sheria za nchi. Sheria zetu zinatambua Sheria tulizozirithi kutoka kwa Wakoloni, Sheria zilizotungwa na Bunge, Sheria za Kimila pamoja na Sheria za Kiislamu. Hii ni kwa mujibu wa Sheria iitwayo Judicature and Application of Laws Act, 1961 (JALA) hususan kifungu cha 11(c)(ii) kinachoelekeza kwamba: “Nothing in this Section shall prelude any Court from applying the rules of Islamic Law in matters of marriage, divorce, guardianship, inheritance, wakf and similar matters in relations to members of a Community which follows that law”.

Ndugu Viongozi wa Dini;


Kufuatia kuunganishwa kwa mifumo yetu ya Mahakama za wenyeji na Mahakama za wazungu na kuwa mfumo mmoja, mwaka 1963, kazi ya kusimamia sheria hizi ilikuwa chini ya Mahakama za Mwanzo.
Mwaka 1964 ilitungwa Sheria iitwayo “The Islamic Law Restatement Act (Sura ya 378) ambayo ilimpa Waziri wa Sheria majukumu ya kutambua na kutangaza matamko mbalimbali ya sheria za kiislamu kwa mujibu wa madhehebu tofauti ya Kiislamu. Sheria zote mbili (JALA) na Islamic Law Restatement Act, zilipiga marufuku matumizi ya Sheria za jinai za Kiislamu na Kimila. 

Mwaka 1971 kufuatia Tume ya Jaji Spry iliyoundwa mwaka 1968, ilitungwa Sheria mpya ya ndoa. Sheria hii ya ndoa inatambua mifumo ya sheria na taratibu za kufunga ndoa zinazotumika na dini mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya Wakristo na Waislamu. Ndoa za Kikristo zinasajiliwa na Wakristo wenyewe Makanisani na kwa Waislamu, Makadhi wanatakiwa kuhudhuria, kufungisha na kusajili ndoa za Kiislamu. Hii ni kwa mujibu wa fungu la 43 la Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, Sura ya 29 ya Sheria zetu ambayo inasema:

(2) When a marriage is celebrated by a minister of religion according to the rites of a specified religion, it shall be his duty forthwith to register it.

(3) When a marriage is contracted in Islamic form in the presence of a Kadhi, it shall be his duty forthwith to register it.

(4) When a marriage is contracted in the presence of a registration officer in Islamic form (no kadhi being present) or according to customary law rites, it shall be the duty of the registration officer to take necessary steps to register the marriage with the district registrar or a kadhi.

Taratibu za kuvunja ndoa kwa mujibu wa fungu la 101 la Sheria hiyo, linawataka wahusika kwanza kupata suluhu ya Mabaraza ya Ndoa, ikiwa ni pamoja na yale ya Makanisa na ya Misikiti. Kama mabaraza haya yakishindwa ndipo mtu anaweza kuomba talaka. Ingawa utaratibu huu umewekwa kwenye Sheria ya Ndoa, talaka ni utaratibu unaotumbulika na Waislamu, Wakristo hawana. Kwao ndoa inayofungwa Kanisani haivunjiki. Hivyo, usuluhishi wa Kiislamu ni tofauti sana na wa Kikristo.

Hivyo basi, kinachotafutwa kwenye muswada uliopo Bungeni siyo kitu kigeni, kipo kwenye Sheria ya JALA, Islamic Law Restatement Act na Sheria ya Ndoa. Kwa kweli kinachotafutwa ni kidogo tu, kama Kadhi anafungisha ndoa kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa, kwa kutumia Sheria ya Kiislamu, inayotambulika kwa mujibu wa Sheria ya Islamic Law Restatement Act na JALA, basi mamlaka itambue maamuzi yake hayo na katika masuala ya mirathi na wakfu. Ilivyo sasa, ni vigumu kwa Waislamu waliopitia kwenye Mahakama ya Kadhi, kupata haki zao kutoka kwenye Mamlaka mbalimbali za nchi kwa sababu maamuzi ya Mahakama hizo hayana nguvu ya kisheria. Jamani ndugu zangu hili nalo lina ubaya gani mpaka tufike mahali pa kutaka kupata uhasama na kuhatarisha amani, usalama na utulivu wa nchi zetu? 

Sioni sababu ya kupandikiza chuki baina ya Wakristo na Serikali yao, au baina ya Wakristo na Chama cha Mapinduzi chenye hiyo Serikali. Sioni sababu ya kuleta mfarakano baina ya Wakristo na Waislamu. Haipo kabisa kwani sheria zetu zinatambua na kujali haki za msingi za dini zote. Zipo Sheria zinazotambua mambo ya Wakristo kuhusu ndoa (Sheria ya Ndoa ya 1971 Sura 29), urithi Cap 345 ya 2002, Sheria ya Viapo na Matamko na kadhalika. 

Zipo sheria zinazowahusu Waislamu, sura 28 ya 2002 inayozungumzia mirathi ya muumini asiyekuwa mkristo au mwenye asili ya Kiasia (Non Christian – Non Asiatic Act, the Islamic Law (Restatement) Act. Na Wahindu nao wanasheria yao kuhusu mirathi na kuendeleza mali za marehemu (Hindu Law Succession Act of 1870.

Kila dini mambo yake yanatambuliwa kisheria tena kwa mujibu wa taratibu za dini hizo zinavyotaka iwe. Na, yote yanahusu ndoa, talaka, mirathi na wakfu. Katu hairuhusu masuala ya jinai. Na, Mahakama ya Kadhi inahusu mambo hayo. Kama inavyofanywa kwa dini zote nyingine kama Waislamu wameamua Kadhi ndiyo wasimamie shughuli hizo iweje tuwakatalie? Tutazua chuki isiyo kuwa na sababu.

Mwisho
Ndugu zangu, tunapoelekea kwenye uchaguzi kuna mambo mengi yatakayofanywa na mengi yanayosemwa. Mengine kwa nia njema, na mengine kwa hila za kujitafutia ushindi katika chaguzi, na mengine kwa hila ya kuitakia nchi yetu mabaya. 

Tusikubali kuruhusu watu wenye nia mbaya na nchi yetu kutugawa kwa misingi ya dini zetu. Daima tukumbuke kuwa yale yanayotuunganisha ni muhimu zaidi kuliko yale yanayotugawa. Viongozi wa dini hamna budi kutambua kwamba nafasi na mamlaka yenu katika kujenga au kubomoa umoja na mshikamano wa kitaifa ni mkubwa. Huko nyuma nilikwisha watahadharisha juu ya watu wenye dhamira ya kutaka kutufarakanisha kwa misingi ya dini. Wako watu wanaojiuliza kwa nini Tanzania ni tulivu kwa nia ya kutafuta mbinu za kuwagawa na hata kuwasambaratisha kama ilivyo kwa baadhi ya nchi za Afrika. Kwa historia yetu si rahisi kutumia kabila, rangi na mengineyo. Wameamua kutumia imani zao za kidini. Ninyi ndio viongozi wetu naomba muwe wepesi kutambua hila hizo na kuzizuia. Narudia kuwatahadharisha muwe macho na watu hao. Hatutegemei viongozi wa dini wakatufikisha huko.

Kama viongozi wa kitaifa, tunao wajibu wa kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa. Na si vinginevyo.

Mungu Ibariki Tanzania!

Asanteni kwa Kunisikiliza!


No comments:

Post a Comment