Na Fidelis
Butahe, Mwananchi
Alhamisi, Februari 26, 2015 saa 9:1 AM
Kazi ya
uandikishaji wapigakura ambayo ni muhimu katika mchakato wa Kura ya Maoni ya
kupitisha au kukataa Katiba Inayopendekezwa, imekuwa na changamoto nyingi
kutokana na kutumia teknolojia ya ‘Biometric Voters Registration’ [BVR] ambayo
hukusanya taarifa za mpigakura, ikiwa ni pamoja na alama za vidole.
Dar es
Salaam. Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umetaja mambo nane
yatakayosababisha Kura ya Maoni isipigwe Aprili 30, 2015 kama ilivyotangazwa na Rais
Jakaya Kikwete, licha ya kazi ya kuandikisha wananchi kwenye Daftari la
Wapigakura kuendelea mkoani Njombe.
Kazi hiyo
ya uandikishaji wapigakura ambayo ni muhimu katika mchakato wa Kura ya Maoni ya
kupitisha au kukataa Katiba Inayopendekezwa, imekuwa na changamoto nyingi
kutokana na kutumia teknolojia ya ‘Biometric Voters Registration [BVR] ambayo
hukusanya taarifa za mpigakura, ikiwa ni pamoja na alama za vidole.
Ukawa,
ambayo inaundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD, pia imetaka
fedha ambazo zimetengwa na Serikali kwa ajili ya Kura ya Maoni, kupelekwa
kwenye uboreshaji wa Daftari la Wapigakura kwa maelezo kuwa uboreshaji
unaondelea mkoani Njombe unakabiliwa na changamoto nyingi na kutaka kura ya
Maoni kuahirishwa hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Kauli hiyo
imekuja siku tatu baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuanza kuandikisha
wakazi wa mji mdogo wa Makambako, ambapo kwa kasoro hizo wakazi wake
wamelazimika kuiomba Nec kuongeza maofisa na vitendea kazi ili kuwezesha
shughuli hiyo kukamilika ndani ya muda uliopangwa.
Viongozi
wa Ukawa, Freeman Mbowe (Chadema), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Dk Emmanuel
Makaidi (NLD) na Mosena Nyambabe (NCCR-Mageuzi), walitoa kauli hiyo jana wakati
wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wakisisitiza kuwa
Serikali inalazimisha mambo isiyoyaweza.
Akitaja
sababu hizo, Profesa Lipumba alisema: “Kwanza, Nec haina watumishi wa kufanya
kazi ya uandikishaji. Mshauri mwelekezi kutoka Marekani aliishauri tume kuwa
inahitaji kuwa na watumishi 10,000 ili kufanikisha uandikishaji nchi nzima na
wapewe mafunzo ya kina ya kutumia mashine hizo.”
Alisema
watumishi waliopo Makambako ni wachache na wamepewa mafunzo ya siku moja tu,
kabla ya kuanza kwa uandikishaji, na wengi wao hawajui kutumia kompyuta wala
kamera ambazo ndiyo zinazotumika kuchukua taarifa muhimu.
Alitaja
sababu ya pili kuwa ni Nec kukabiliwa na uhaba wa fedha kwa maelezo kuwa
ilipewa jukumu la kuboresha Daftari la Wapigakura bila kutengewa fedha za
kutosha za kununulia vifaa, kuajiri na kuwapa mafunzo wafanyakazi husika
sambamba na kutoa elimu kwa wananchi.
“Tatu,
Tume haisemi ukweli juu ya suala zima la uandikishaji. Wamesema watakamilisha
kazi Aprili 28 na 30 itafanyika Kura ya Maoni. Nchi ina watu milioni 24 wenye
haki ya kupiga kura na haiwezekani wakaandikishwa kwa muda uliobaki,” alisema.
Alisema
sababu ya nne ni mashine za BVR kuwa na kasoro nyingi, ikiwamo ya kutotambua
alama za vidole gumba vya wananchi ambao wanafanya kazi ngumu, hivyo vidole
vyao kuwa na sugu ambao wengi wao ni wakulima, wafugaji na wachimbaji wa
madini.
“Sababu ya
tano, ni Nec kupuuza ushauri wa mshauri mwelekezi ambaye aliitahadharisha tume
hiyo kwamba haiwezekani kutumia mfumo wa BVR kukamilisha kazi kwa wakati
kutokana na changamoto zinazoikabili tume hiyo, ikiwamo ya ukosefu wa fedha,
uchache wa watumishi, ” alisema.
Akizungumza
na Mwananchi mapema wiki hii, mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva alisema
ushauri wa mtaalamu huyo ni wa siku nyingi na kwamba alitaka utumike mfumo wa
zamani, lakini tume yake imekataa.
Mchumi
huyo, Lipumba alitaja sababu ya sita kuwa ni Nec kutoweza kuandikisha
wapigakura wote katika jimbo moja kwa siku saba na kueleza kuwa ni aibu kwa
tume hiyo kusema kuwa imeandikisha wapigakura 3,014 katika vituo 55, sawa na
wapigakura 54 tu kwa siku kwa kila kituo.
“Sababu ya
saba. Ili kuandikisha wananchi milioni 24 wenye haki ya kupiga kura,
itahitajika wastani wa siku 55 kila mashine kuandikisha kwenye vituo nchi
nzima, tena mashine zisiharibike. Kwa sasa Nec wana mashine 250 tu na nyingine
7,750 hazijulikani zitafika lini,” alisema.
Alitaja
sababu ya nane kuwa ni Nec kutotoa taarifa za kutosha kwa wadau wote kuhusu
teknolojia ya BVR, kutotoa taarifa ya nchi nzima ya vituo vya kuandikishia
wapiga kura vilivyopo kila kata, mpaka sasa hakuna mwananchi anayejua.
Profesa
Lipumba alisema kama hali ikiendelea hivyo, Ukawa watafungua kesi mahakamani
kutaka kusitishwa kwa kura ya maoni kwa sababu Nec haijatoa elimu kwa wananchi,
kukiukwa kwa Sheria ya Kura ya Maoni.
“Taifa
litaingia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa kama uandikishaji wapigakura
hautafanyika kwa ufanisi kabla ya kipindi cha kampeni ya Uchaguzi Mkuu.
Tunaitaka Nec ikae na wadau wa Tehama ili kueleza matatizo ya BVR na jinsi ya
kutoka hapa tulipo,” alisema.
Akizungumzia
kuhusu muda mfupi kabla ya tarehe ya Kura ya Maoni mapema wiki hii, Jaji Lubuva
alisema wanachoangalia sasa ni kazi ya uandikishaji wapigakura na kwamba kama
itashindikana, wataeleza.
Tayari
mchakato huo umekumbwa na utata kutokana na wadau kusema kuwa Sheria ya Kura ya
Maoni imekiukwa baada ya Rais Kikwete kutangaza tarehe ya kupiga kura.
Wanaeleza kuwa Sheria hiyo inaipa Nec mamlaka ya kutangaza siku ya kupiga kura,
wakati Rais anatakiwa atangaze kipindi cha Kura ya Maoni.
Mbowe
Akizungumza
mashine hizo Mbowe alisema kwa taarifa walizonazo, Makambako kuna mashine 82 na
siyo 250 kama Nec inavyodai na kwamba zilizobaki zinatumika kufundishia
watumishi wa tume hiyo watakaotumiwa kwenye mikoa mingine.”
“Tuna
taarifa pia kuwa hawa jamaa wanashinikiza Kura ya Maoni ipigwe Aprili 30, 2015 na
Katiba ianze kutumika kabla ya Uchaguzi Mkuu, tayari wameanza kubadili baadhi
ya sheria.”
Mbowe
alisema Rais Kikwete asilazimishe kupatikana kwa Katiba mpya ili aondoke katika
utawala wake akiiacha nchi ikiwa na amani kama ilivyo sasa.
Kwa upande
wake Dk Makaidi alisema tatizo ni Rais Kikwete kutaka Katiba Mpya ipatikane
kabla hajaondoka madarakani ilia ache sifa kwa watanzania, jambo ambalo alisema
litasababisha machafuko nchini.
No comments:
Post a Comment