Saturday, February 14, 2015

MADHILA NA MADHARA - NILITEMEWA MATE NA MPIGA DEBE WA DALADALA BUGURUNI 12/2/2015

TUKIO  LA KUTEMEWA  MATE  NDANI  YA  DALADALA  JIJINI  DAR ES SALAAM

Na.  Zainab M. Mwatawala

Jamani hili nimeona nilisimulie humu, ili tujionee jinsi jamii yetu inavyoendelea kuporomokewa maadili. 
Nikiwa katika Daladala la kutokea Mbagala kuelekea Ubungo kupitia njia ya  Kilwa Road, Mandela Access Road, tulifika kituo cha Buguruni wakati wa magharibi. 

Kosa langu lilikuwa kukaa kiti cha dirishani kushoto.  Akatokea  mpiga debe na kuanza kudai fedha kwa kondakta.  Baada ya kondakta kutomsikiliza [kumpotezea], yule mpiga debe akanigeukia mimi.  Akaniuliza endapo nilishalipa nauli kwa kondakta?  Na kama bado, ile nauli yangu nimpe yeye kama malipo yake hayo aliyokuwa anayadai kwa kondakta.  Nami nikawa  nimegeuza uso wangu pembeni kabisa kana kwamba sikusikia alichokisema.   Nalifahamu kwamba mimi mkataba wangu wa kulipana fedha ni kwa kondakta wa basi na sio mpiga debe hivyo sikuona cha kumjibu wala sikuona sababu ya kubishana na mpiga debe. 

Baada ya kuona kuwa kondakta na mimi wote hatumtimizii hitajio lake na baada ya dereva kuonyesha dalili ya kutaka kuliondoa basi kituoni,  mpiga debe aliyekuwa anaonekana dhahiri kwamba ana ugonjwa mkubwa akaamua kunitemea mate kwa kuwa dirisha lilikuwa wazi.  Akamwaga mate yake yakeniangukia mimi pamoja na niliyekaa naye pembeni yangu.

 Jambo hili limenisikitisha na kunisononesha sana kuona jinsi jamii yetu inavyozidi kuporomoka kimaadili.  Kama kweli mpiga debe alikuwa na ugomvi wa kudaiana fedha  na kondakta,  nilihusikaje kuadhibiwa kwa kutemewa mate?   Siku hiyo sikuwa na jazba hasa kutokana na hali ya huyo mhalifu mpiga debe kwa sababu kwa kweli alionekana kuwa ni dhaifu aidha ana TB au ana zaidi ya TB.   Maana alikuwa dhaifu mno.  Pamoja na hayo, udhaifu ule haikuwa ndio ruhusu kwake kufanya uhalifu ule wa kunitemea mate mimi kwa kosa nisilolifahamu.  Na hata kama nilikuwa nimemkosea,  alichofanya hakikuwa kitendo sahihi kwa shitaka lake. 

Hivyo natoa tahadhari sana kwa wasafiri wenzangu hasa wakaao viti vya madirishani, wawe macho sana na wahalifu kama hao.   Kwa upande wangu,  mavazi yangu yalimkwaza yule mhalifu kuninyang'anya chochote nilichokuwa nacho mkononi, lakini nahofia huenda angepata fursa hiyo, huenda angeitumia kunikwapulia nilichonacho kisha aseme tudaiyane na kondakta!  Jamani jamii yetu inakwenda wapi?

No comments:

Post a Comment