Mazito ya Chenge yaibuka
Na Ibrahim
Yamola, Mwananchi
Alhamisi,Februari 26, 2015 saa 9:13 AM
Alhamisi,Februari 26, 2015 saa 9:13 AM
KWA
UFUPI
Mbunge huyo wa Bariadi
Magharibi aliibua mvutano wa kisheria akipinga kujadiliwa.
Dar es Salaam. Mbunge
wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge ameibuliwa tuhuma nzito kwenye Baraza
la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma baada ya kudaiwa kuwa
aliishawishi kampuni ya Independent Power Solution Limited (IPTL) kuingia
mkataba na Tanesco na baadaye kuwa mshauri wa kampuni hiyo binafsi
iliyomuingizia Sh1.6 bilioni zinazohusishwa na sakata la Akaunti ya Tegeta
Escrow.
Hata hivyo, Chenge,
ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Umahiri wa Sheria kwenye Chuo Kikuu cha Harvard
cha Marekani, aliwasilisha amri ya zuio ya Mahakama Kuu inayokataza chombo
chochote cha Serikali kujadili sakata la escrow hadi hapo shauri lililopo
mahakamani litakapotolewa uamuzi, jambo lililozua mjadala wa kisheria na
kusababisha mwenyekiti wa Baraza la Sekretarieti ya Maadili, Jaji Hamisi Msumi,
kuahirisha hadi leo.
Chenge ni mmoja wa
watu kadhaa wanaotarajiwa kuhojiwa na kamati hiyo kutokana na kuhusishwa na
kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh306 bilioni kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta
Escrow iliyofunguliwa Benki Kuu kwa makubaliano kati ya Tanesco (shirika la
umeme la umma) na IPTL baada ya pande hizo mbili kutofautiana kuhusu tozo za
malipo ya umeme unaozalishwa na kampuni hiyo binafsi.
Mwingine ni mbunge wa
Muleba Kusini (CCM), Anna Tibaijuka, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi na ambaye pia aliingiziwa kwenye akaunti yake Sh1.6 bilioni
zinazohusishwa na akaunti hiyo ya escrow.
Wote wawili
waliingiziwa fedha hizo na James Rugemarila, mkurugenzi wa VIP Engineering
iliyokuwa ikimiliki asilimia 30 ya hisa za kampuni ya IPTL.
Tuhuma dhidi ya Chenge
Tangu sakata la escrow
lianze, haikuwahi kuelezwa kuhusika kwa Chenge kwenye sakata hilo.
Lakini jana, akisoma
hati ya malalamiko dhidi ya mbunge huyo wa Bariadi, mwanasheria wa Sekretarieti
ya Maadili, Hassan Mayunga alisema mlalamikiwa, akiwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG) mwaka 1995, aliishauri Serikali kuingia mkataba wa miaka 20 na
IPTL wa kuongeza uzalishaji wa umme.
“Mlalamikiwa baada ya
kustaafu wadhifa wa AG, Desemba 24 mwaka 2005, mwaka 2006 aliingia mkataba wa
kuwa mshauri mwelekezi wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited
iliyokuwa inamiliki asilimia 30 ya hisa za IPTL,” alisema Mayunga akikariri
hati hiyo ya malalamiko.
“Kitendo cha
mlalamikiwa kuingia mkataba na VIP Engineering and Marketing Limited iliyokuwa
na asilimia 30 ya hisa kwenye kampuni ya IPTL ni ukiukwaji wa fungu la 6 (j) la
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambalo linamzuia kiongozi wa umma
kujinufaisha na utumishi wake uliopita kwa kutumia taarifa alizozipata alipokuwa
anatekeleza majukumu yake kwa manufaa binafsi.
“Kitendo cha
mlalamikiwa kuendelea kuwa mshauri mwelekezi wa kampuni ya VIP Engineering and
Marketing Limited akiwa na wadhifa wa ubunge ni ukiukwaji wa fungu la 6(e) la
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambalo linamzuia kiongozi wa umma
kujiingiza katika mgongano wa maslahi.”
Mwanasheria huyo
aliendelea kusema kuwa mkataba ambao mlalamikiwa aliingia na kampuni ya VIP
Engineering and Marketing Limited ulimpatia manufaa ya kifedha ya Sh1.617
bilioni kinyume na fungu la 12(1)(e) la Sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Aliongeza kuwa mlalamikiwa hakutamka maslahi aliyokuwa nayo katika mkataba wa
Tanesco na IPTL kinyume na fungu 14 la sheria ya Maadili.
Aliongeza
kuwa mlalamikiwa hakutamka madeni yake aliyokuwa anaidai kampuni ya VIP
Engineering and Marketing Limited kwa Kamishna wa Maadili kinyume na matakwa ya
fungu la 9(6)(b) la sheria hiyo.
“Malalamiko
dhidi ya Chenge yanawasilishwa mbele ya Baraza la maadili lenye mamlaka ya
kisheria ya kufanya uchunguzi wa kina na kumtaka mlalamikiwa kutoa maelezo
bayana kuhusu mwenendo wake kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa kwa mujibu wa
sheria,” aliongeza.
Baada ya
kusoma tuhuma hizo, Chenge alitoa amri hiyo ya zuio la Mahakama Kuu ambayo pia
iliwasilishwa kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano kulizuia kujadili ripoti ya
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu sakata hilo la escrow,
lakini ikagonga mwamba baada ya wabunge na spika kulinda muhimili wao.
“Kwa kuwa
amri hii ya mahakama nilikuwa sijaipata na ninyi (wanasheria wa sekretarieti)
mlikuwa mmeipata mapema ngoja nikaisome na wenzangu,” alisema Jaji Msumi ambaye
alikuwa akisaidiana na wajumbe wawili, Selina Wambura na Hilda Gondwe.
“Kama
kweli mahakama imezuia vyombo vyote, suala hapa ni kuangalia amri hiyo. Tupeni
muda tukaangalie na kesho (leo) tutatoa uamuzi kama tutaendelea au la.”
Mvutano ulivyokuwa
Kabla ya
kuahirisha shauri hilo ulizuka mvutano mkubwa wa kisheria kuhusu amri hiyo ya
zuio la mahakama.
“Suala
hili ninavyofahamu mimi liko mbele ya Mahakama Kuu, hivyo tusubiri uamuzi wa
mahakama kwani amri ya mahakama ilizuia vyombo vyote vya Serikali na hiki
(Baraza la Maadili) ni chombo cha serikali. Mwenyekiti, mimi nataka kupata
mwongozo wa suala hili, tukiendelea bila kupata mwongozo na mimi kama
mwanasheria litanisumbua sana,” alisema Chenge ambaye alikuwa Mwanasheria wa
Serikali kati ya mwaka 1972 na 1973.
Lakini
Mayunga alisimama na kusema: “Mheshimiwa mwenyekiti, hii amri ya mahakama
ambayo mlalamikaji (Chenge) ameitoa hapa, si Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma inayohusika kama mlalamikiwa alivyotaja.
“Tuhuma
ambazo zimeletwa hapa ni tuhuma za uvunjifu wa maadili ya viongozi wa umma na
wala siyo suala lililoonyeshwa katika hii amri... ni tofauti kabisa.”
Mayunga,
katika kujenga hoja, alisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka
1977 Ibara 132 (1) ya inayosema kuwa “kutakuwa na Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma ambayo itakuwa na mamlaka ya kuchunguza tabia na mwenendo wa
kiongozi wa umma yeyote kwa madhumuni ya kuhakikisha kwamba masharti ya Sheria
ya Maadili ya Viongozi wa Umma yanazingatiwa ipasavyo”.
Pia
alisoma fungu la 18 (2) (c) la sheria hiyo linaloipa Sekretarieti ya Maadili
mamlaka ya kuchunguza tuhuma yoyote ya kuvunjwa kwa Sheria ya Maadili ya
Viongozi wa Umma na viongozi wote wa umma, wanaopaswa kuwajibika chini ya
sheria hiyo.
Kutokana
na sheria hii, Sekretarieti haizuiwi kuendelea na shauri hili. Madai dhidi ya
mlalamikiwa ni ya jinai na rushwa. Hapa tunajikita katika maadili wala sisi
hatuzungumzii escrow, hapa ni maadili kuwa amepokea fedha kutoka VIP
Engineering,” alisema Mayunga
Jaji Msumi
alisema hati hiyo aliipitia haraka haraka na akahoji kama ina amri inayozuia
suala hilo kujadiliwa.
Chenge
alijibu, “mheshimiwa mwenyekiti, hoja ambayo nimeileta mbele yako ni zuio la
mahakama. Kueleza kwamba chombo hiki kiko juu ya mahakama bila...”
Kabla ya
kumalizia sentensi hiyo alisimama mwanasheria wa Sekretarieti hiyo, Filotheus
Manula na kusema: “Kauli anayoisema mlalamikakiwa kuwa chombo hiki kiko juu ya
mahakama siyo sahihi. awali Mayunga alishaelezea. Katiba na Sheria ya Maadili
na iko wazi.”
Lakini
Chenge akasema: “Ni vizuri vijana wakajifunza... amri hii ya mahakama siyo
maoni yangu, hivyo ni vyema ikaheshimika. Itanisumbua mimi, mamlaka ya chombo
hiki isitishwe siyo kwamba haina mamlaka, mnaweza kuendelea sawa, lakini hili
ni ombi langu.
“Utawala
wa sheria ni bora ukaheshimiwa na masuala ya siasa tuache tukapige siasa
majukwaani.”
Mayunga
alisimama na kusema: “Mheshimiwa mwenyekiti ukiruhusu hiki anachokisema au
uhalisia wa kuzuia kinachoendelea, siyo sahihi.”
Chenge
alijibu, “mheshimiwa mwenyekiti amri ya mahakama ni (inahusu) taarifa ya
ukaguzi wa miamala ya akaunti ya Tegeta Escrow ya (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali) CAG, na malalamiko yanayoletwa dhidi yangu ndiyo ambayo
yamezuiwa... mimi ninachoomba ni ufafanuzi au mwongozo kwa hili.”
Lakini
Manula alipinga akisema: “Penal Code (Sheria ya Kanuni ya Adhabu) haitumiki
hapa. Mlalamikiwa ndiye aliyekuwa AG, alisimamia kuitunga... madai, jinai na
rushwa, lakini hapa tunajadili maadili na siyo escrow.”
Chenge,
aliyekuwa amesimama wakati wote, aliendelea na msimamo wake wa kuomba mwongozo,
hali iliyomfanya mwanasheria mwingine wa sekretarieti hiyo, Getiruda Cyriacus
kusimama na kunukuu fungu la 18 (4) la sheria hiyo linalosema sekretarieti
itakuwa na mamlaka ya kuanzisha na kufanya uchunguzi wowote kuhusu ukiukwaji wa
maadili yaliyotajwa katika sheria hiyo.
Vituko vya Chenge
Chenge
aliingia kwenye viwanja vya Ukumbi wa Karimjee saa 3:02 asubuhi akiwa katika
gari aina ya Toyota Land Cruizer akiongea na simu na aliposhuka, aliwaambia
waandishi wa habari waliokuwa wakimpiga picha akisema: “Nendeni mkauze magazeti
na sura ya Chenge.”
Alipotaka
kuingia ukumbini, aliambiwa asubiri kwenye viti, lakini aligoma na badala yake
alishuka chini na kuanza kuzungumza na simu huku akizungukazunguka takribani
dakika 10 kabla ya kutakiwa kuingia ukumbini saa 3:13 asubuhi.
Mara baada
ya Jaji Hamis kuahirisha baraza hilo saa 3:55, waandishi walianza tena kumpiga
picha na kama kawaida alisema: “Nendeni mkaandike mnavyoona... mnataka na
mgongo muupige picha?”
Waandishi
kutoka vyombo mbalimbali vya habari walipotaka kufanya naye mahojiano ya suala hilo
alijibu, “siwezi kuzungumzia chochote kuhusu yaliyopo katika maadili” na
kupanda gari, kisha akaondoka
No comments:
Post a Comment