KUTOKA HABARI LEO, TANZANIA, 5/12/2014.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame :
KATIKA kuhakikisha uchochezi unaoweza kuvuruga amani ya
nchi unadhibitiwa wakati wa uchaguzi, Serikali imeiagiza Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuja na mwongozo wa kampuni za simu katika
kudhibiti ujumbe mfupi kwa njia ya simu.
Aidha, ameitaka sekta ya utangazaji nchini kutumia fursa ya Mkongo wa Taifa katika utangazaji.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa alipokuwa akifungua
maadhimisho ya Siku ya Teknolojia ya Mawasiliano (ICT) Afrika.
Katika ujumbe wake kwa siku hiyo, alisema ujumbe mfupi wa
kwenye simu usipodhibitiwa unaweza kuleta madhara makubwa wakati wa
uchaguzi.
“TCRA mje na mwongozo wa makampuni ya simu hasa kuhusu
ujumbe, maana kama utaachwa hivi hivi wakati wa uchaguzi itakuwa ni
hatari, Kenya ilifanya hili na walifanikiwa,” alisema.
Tayari TCRA imeshatengeneza miongozo ya namna ya kuripoti
na kuandaa vipindi wakati wa uchaguzi kwa upande wa sekta ya utangazaji
na wamiliki wa mitandao ya kijamii, yaani ‘blogers’.
Mbarawa alitumia nafasi hiyo kuvitaka vyombo vya utangazaji
kutumia miongozo waliyopewa katika kutangaza habari na zisizo na
ushabiki na kutotumiwa vibaya na baadhi ya watu.
Kuhusu Mkongo wa Taifa, Mbarawa aliitaka sekta ya
utangazaji kutumia ipasavyo fursa ya kuwapo kwa Mkongo wa Taifa katika
matangazo yao.
Alisema Serikali imewekeza dola za Kimarekani milioni 200
(Sh bilioni 340) katika teknolojia hiyo na kuwa sekta ya simu ndiyo
pekee inayotumia na kunufaika na teknolojia hiyo.
Mbarawa alisema ili kuhakikisha taasisi za utangazaji
zinatumia Mkongo wa Taifa, amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake kuunda
timu ya wadau itakayoangalia suala hilo.
Awali, Mkurugenzi wa TCRA, Profesa John Nkoma alisema
teknolojia ya mawasiliano nchini imekuwa na manufaa na kuchagiza
maendeleo ya wananchi.
Nkoma alitolea mfano kuwa hadi sasa kuna laini za simu
milioni 28 na laini za intaneti milioni tisa na kuwa matumizi ya simu
katika kufanya miamala ya kibenki imeongezeka.
Naye Mratibu wa Ufundi wa Umoja wa Mawasiliano Afrika (ATU)
“African Telecommunications Union), Kezias Mwale aliipongeza Tanzania
kwa kuwa miongoni mwa nchi tatu za Afrika ambazo zimeshahamia kwenye
dijitali na kuwa baadhi ya nchi zimeahidi kufikia lengo hilo kabla ya
muda uliowekwa kupita.
Tanzania inatarajiwa kuingia katika mwaka wa uchaguzi mwaka
kesho, kwani mbali ya kutarajiwa kupata Rais wa Awamu ya Tano
atakayechukua nafasi ya Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake,
wananchi wanatarajiwa pia kupiga kura za kuwapata wawakilishi wapya
katika ngazi za majimbo na kata.
Aidha, kama sehemu ya mchakato wa uchaguzi mkuu ujao,
mwishoni mwa wiki ijayo Watanzania watafanya Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa utakaowaweka madarakani viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa.
No comments:
Post a Comment