Thursday, February 14, 2013

VURUGU ZA BUSERESERE, WILAYANI CHATO, MKOANI GEITA, TANZANIA

Imetundikwa hapa leo hii tarehe 15/2/2013

Chanzo:  TANZANIA DAIMA,  14 Februari, 2013.

Naomba kujua kama kuna sheria Tanzania inayoelekeza uchinjaji wa kitoweo. Naomba nielimishwe ni sheria gani hiyo?




MCHUNGAJI wa Kanisa la PAGT, Isaya Rutta (52), mkazi wa Kijiji cha Katoro, Wilaya ya Geita, mkoani Geita, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuchinja ng’ombe mmoja na mbuzi wawili kinyume cha sheria, hali iliyosababisha vurugu kati ya Waislamu na Wakristo.
Vurugu hizo zilitokea juzi na kusababisha kifo cha mtu mmoja ambaye ni mchungaji wa kanisa moja wilayani hapa huku watu wengine 10 wakijeruhiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Paulo Kasabango, alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi katika kijiji hicho ambapo inadaiwa kuwa alihusika kuchinja mifugo eneo la Kanisa la AIC bila ya kuhusisha daktari wa mifugo kwa lengo la kuthibitishwa kama nyama hiyo ni salama kuliwa na binadamu.

Kasabango alisema kuwa mbali na kukamatwa kwa kosa hilo, pia anadaiwa kufanya makosa ya kuchinja eneo ambalo si rasmi kwa mujibu wa sheria ya kifungu namba 17 ya mwaka 2003.

Alisema kuwa mtuhumiwa mwingine Ramadhani Pastory, ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, anadaiwa kumuua Mchungaji Mathayo Kachila wa Kanisa la PAGT Buseresere na kwamba atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo wakati wowote akipata nafuu.

Uchunguzi wa gazeti hili uliothibitishwa na polisi umebaini kuwa baadhi ya watu katika Kijiji cha Buseresere wametelekeza familia zao na kukimbilia kusikojulikana ili kukwepa mkono wa sheria, kwa hofu ya kukamatwa na kuhusishwa na vurugu hizo.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Magalula Saidi Magalula, alikemea vikali kitendo walichokifanya baadhi ya wananchi cha kujichukulia sheria mkononi, akisema kuwa kinahatarisha amani.

Naye Mganga Mfawidh wa Hospitali ya Mkoa wa Geita, John, alisema hali za majeruhi zinaendelea vizuri na kwamba hawajapokea majeruhi wengine isipokuwa kati ya waliopokewa jana Ramadhani Pastory (52) na Sadiki Yahaya (40), wamehamishiwa Bugando kutokana na hali zao kuwa mbaya.

No comments:

Post a Comment