HAKUNA kitu kibaya kama kumpa mtu au umma wa watu matumaini ambayo baadaye yanakuja kuonekana kuwa yalikuwa siyo na kama yapo si kwa kiwango kilichotarajiwa.
Kwenye siasa watu wanaweza kufanya mazingaombwe, kwa kuwaambia watu kuwa watajazwa mapesa mifukoni, kama ilivyowahi kutamkwa siku za nyuma na baadhi ya wanasiasa kumbe ni danganya toto. Ni namna tu ya kupeleka ujumbe wa kupata ridhaa ya uongozi mahali hapo.
Mapema mwezi Agosti mwaka jana, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison George Mwakyembe aliuondoa uongozi wote wa juu wa TPA, ikiwa ni pamoja na kuvunja bodi ya shirika hilo nyeti kwa kile alichokieleza ni kukithiri kwa uozo, uzembe na wizi uliosababisha wateja waikimbie Bandari ya Dar es Salaam.
Wengi walipongeza uamuzi wa waziri kiushabiki na wengine kadiri siku zinavyokwenda wamekuwa wakiukosoa na kuona kuwa hautaleta tija anayotegemea, hasa kwa kuwa TPA ni mshirika kati ya wadau wengine muhimu wanaoifanya bandari iwe na ufanisi unaotakiwa.
Kwa sisi wafanyakazi hasa kutoka Idara ya fedha tunakiri kuwa mapato ya TPA yamekuwa yakiongezeka kwa kiasi kikubwa mwaka hadi mwaka tangu 2006 hadi Juni 2012 na miradi (projects) nyingi kama mradi mkubwa wa bomba la kupokelea mafuta (spm), ujenzi wa one stop centre wa ghorofa 35 unaoendelea, gati ya Mafia, ujenzi wa Cfs (cargo freight station) pale ilipokuwapo Nasaco Depot--Kurasini, ujenzi wa magati kwenye bandari za maziwa, kupanua maeneo ya kuegesha makontena ndani ya Bandari ya Dar es Salaam, n.k. Yote yamefanyika katika kipindi hicho.
Ni vema watu wakakumbushwa historia kuwa TPA ilikuwa moja ya mashirika yaliyokuwa ‘lined up’ na PSRC katika kubinafsishwa na mwaka 2000 kitengo chake muhimu cha kuingizia mapato kilibinafsishwa ambacho ndiyo TICTS ya sasa.
Kutoka mwaka 2000 hadi 2006 TPA haikushughulika na chote chote katika kuendeleza shughuli zake kwenye vitengo vilivyobakia, kwa kuwa walikuwa wanangojea kubinafsishwa na kubaki tu kama mwenye nyumba (land lord).
Mwaka huo 2006 tena serikali ilibadilisha mawazo na kuruhusu TPA waendelee kuwekeza na kufanya tena biashara hadi hapo itakapoamuliwa tena.
Ni kipindi hiki pia utawala mpya wa Ephraem Mgawe ulipoingia chini ya
Mwenyekiti wa Bodi, Raphael Mollel na kuanza kulirudisha shirika kwenye mstari.
Sisi kama wahasibu tumeshangaa kumsikia waziri akiwaambia wanahabari kwamba tangu auondoe uongozi wa zamani na kuweka mpya mapato ya TPA yamepanda na kufikia sh bilioni 50 kwa mwezi, kitu ambacho hakina ukweli hata chembe.
Tunachofahamu, mapato ya juu kabisa kupatikana ni ya mwezi Desemba, 2012 ambayo yalikuwa sh bilioni 31 tu, na hii ni kutokana na msimu wa Sikukuu ya Krismasi, pia ni kipindi cha Ticts kulipa ‘rental and royalty fees’ zao kwa TPA kwa mwaka na kamwe haijawahi kufika sh bilioni 50 kwa mwezi.
Kwanza ieleweke kwamba kabla ya timuatimua hii ya waziri kitengo cha makontena (TPA) kilikuwa kimekwisha kufikia karibu 35% ya meli za makontena zinazotia nanga hapa na sasa kimeshuka hadi 15%.
Je, kwa ‘trend’ hii haya mapato ya sh bilioni 50 yangetoka wapi? Ni vema waziri au kaimu mkurugenzi mkuu wake, Kipande Madeni, auambie tena umma kwamba mapato ya mwezi Januari 2013 yalikuwa kiasi gani na ikifika Machi 31, 2013 atoe linganisho la mapato ya Januari - Machi 2012 na yatakayokuwa yamepatikana Januari - Machi 2013 ndipo itajulikana kama kweli kulikuwa na uzembe kwenye kusimamia mapato.
Tunavyoelewa biashara bandarini zinafuata misimu na mazingira mengi, yakiwamo ya kisiasa, hivyo mapato kupanda kwa mwezi mmoja si kuhalalisha kuwa yatakuwa hivyo kwa kipindi endelevu kama waziri alivyotaka kuuaminisha umma pamoja na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu aliyokutana nayo mapema mwaka huu.
TAARIFA HII HAIONDOI UKWELI KWAMBA WENGI WETU TULIOTUMIA BANDARI YA DAR ES SALAAM KUPITISHIA MIZIGO YETU TUMEPATA HASARA KUBWA YA KUIBIWA MIZIGO HIYO NA BILA KUJUA TUMSHITAKI NANI JUU YA JAMBO HILO.
Mimi binafsi nilisafirisha mizigo yangu mwaka 2010, kupitia kontena la ndugu zangu Amos na Stephen Cherehani, na Kenyatta Mayanga waliyofanya malipo. Kwa kuwa lilikuwa na nafasi, nami nikatia mizigo yangu humo kutoka Washington DC, U.S.A hadi Dar es Salaam.
Kilichotokea ni kwamba vitu vyote vipya nilivyonunua huko U.S.A. VILIIBIWA ndani ya kontena hilo na wakanibakishia mitumba ya vyombo vichache tu. Kwa mtindo huu, bado bandari yetu ya Dar es Salaam, Tanzania, ifanye kazi kubwa ya ziada ya kutatua matatizo haya ili kuirudishia hadhi yake ya stahili ya kupakua na kupakia mizigo itokayo na iendayo kokote ulimwenguni.
[paragrafu tatu za mwisho zimeandikwa na mwenye blogu akielezea uzoefu wake]
|
No comments:
Post a Comment