Imetundikwa hapa leo hii tarehe 18 Februari, 2013.
Pinda akwama mgogoro wa Geita
"Tanzania Daima", 18 Februari, 2013.
Imeandikwa na Victor Eliud, Geita
JUHUDI za Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda za kutaka kutanzua mgogoro wa kidini wilayani Geita mkoani Geita kati ya Waislamu na Wakristo, zimegonga mwamba baada ya Waislamu kugoma kuendelea na kikao wakitaka wenzao waliokamatwa na kushtakiwa waachiwe.
Pinda aliwasili mkoani hapa ili kumaliza mgogoro huo ambao uliibuka wiki iliyopita na kusababisha kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila (45) wa Kanisa la Tanzania Assemblies Of God katika eneo la Buseresere.
Mapema Mkuu wa Mkoa wa Geita, Said Magalula alimtambulisha Pinda na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye alikuwa akimwakilisha waziri wake, Dk. Emmanuel Nchimbi aliyelazimika kwenda Zanzibar kushughulikia tukio la kifo cha Padri Evarist Mushi.
Akizungumza kabla ya waandishi wa habari kutolewa nje ya kikao hicho, Pinda alisema kuwa tukio la Zanzibar linafanana na lile lililotokea Geita, na kwamba alikuwa hapo kutafuta suluhu.
Habari za ndani zilisema kuwa, wakati kikao hicho kikiendelea kati ya Pinda na viongozi hao wa dini zote mbili, mwakilishi kutoka upande wa Waislamu, Hamza Omar alisimama na kumweleza waziri mkuu kuwa yafaa wenzao waliokamatwa waachiwe kwanza, ili wawepo kwenye mazungumzo hayo.
Hata hivyo, Pinda hakukubaliana na wazo hilo kwa ufafanuzi kuwa suala hilo kwa vile liko kisheria, aliomba mahakama iachiwe ifanye kazi yake.
Waziri Mkuu alifafanua kuwa bado watuhumiwa hao hawajatiwa hatiani kwa vile bado uchunguzi unaendelea, hivyo si utaratibu kuingilia uhuru wa mahakama.
Msimamo huo ulipingwa vikali na wawakilishi wa Waislamu waliokuwa kikaoni hapo, na hivyo kunyanyuka na kuondoka ukumbini, hatua iliyomlazimu Pinda kuahirisha kikao hicho.
“Utaratibu unabaki ule ule wa kuchinja, mazungumzo yameshindikana hadi siku nyingine baada ya Waislamu kugomea mazungumzo mpaka wenzao waliokamatwa Buseresere waachiwe,” alisema Pinda.
Kabla ya Waislamu kutoka nje, Pinda alikuwa amekabirisha maoni kutoka pande zote mbili akianza na Wakristo, ambapo Askofu Musa Magwesela wa AICT alisimama na kumwomba kiongozi huyo atoe tamko kuhusu kuchinja.
“Sisi hapa hatuko tayari kula nyama iliyochinjwa na Waislamu kwa vile utaratibu huo hauko kisheria bali ni mazoea, hivyo tunakuomba Waziri Mkuu utoe tamko,” alisema askofu huyo.
Katika vurugu hizo, mali za wananchi ziliharibiwa vibaya, huku baadhi ya maduka na bidhaa zikiteketezwa kwa moto.
Miongoni mwa wananchi walioharibiwa mali zao ni pamoja na Mwenyekiti wa Bakwata Wilaya ya Chato na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Buseresere, Yusuf Idd Banana ambaye amezitaja mali zake zilizoharibiwa kuwa na thamani ya shilingi milioni 10.
No comments:
Post a Comment