AHADI TANO ZA KIKWETE ZISIZOTIMIA
BY THOBIAS MWANAKATWE
2nd October 2015
Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Wakati
zikiwa zimebaki siku 22 kuanzia leo kabla ya uchaguzi mkuu
utakaofanyika Oktoba 25, imebainika kuwa Rais ajaye atakuwa na mzigo
mzito wa kutekeleza ahadi kadhaa zilizowahi kutolewa na serikali ya Rais
Jakaya Kikwete anayetarajiwa kumaliza muda wake baada ya uchaguzi huo
utakaompata mrithi wake.
Uchunguzi
uliofanywa na Nipashe umebaini kuwa, licha ya mafanikio makubwa katika
sekta mbalimbali katika kipindi cha miaka 10 ya serikali iliyopo
madarakani, bado kuna ahadi tano kubwa ambazo ni miongoni mwa zile
zinazoonekana wazi kuwa utekelezaji wake utahitaji muujiza kutokana na
muda mfupi uliobaki kati ya sasa na siku ya kupiga kura.
Kwa
sababu hiyo, imebainika kuwa Rais ajaye atalazimika kufanya kazi ya
ziada kuhakikisha kuwa walau anatekeleza ahadi hizo na hivyo kufufua
matumaini waliyokuwa nayo wananchi kwa kipindi chote tangu wakati wa
kampeni za uchaguzi uliopita.
Hadi
sasa, wagombea wanaoonekana kuchuana vikali katika kampeni
zinazoendelea ni Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
anayewakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) vya NCCR-Mageuzi, NLD na Chama cha Wananchi (CUF).
Wagombea
wengine wanaotafuta ridhaa ya Watanzania katika uchaguzi mkuu wa tano
tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992 ni Fahmy Dovutwa
wa UPDP, Hashim Rungwe wa Chama cha Umma (Chaumma), Maximillian Lymo wa
TLP, Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo, Chifu Lutasola Yemba wa ADC na
Janken Kasambala wa NRA.
Kadhalika,
imebainika kuwa yeyote ayakayeshinda kati ya wagombea hao wa urais,
hasa Dk. Magufuli wa CCM na Lowassa wa Ukawa wanaoonekana kuchuana kwa
karibu kutokana na maelfu ya watu wanaojitokeza kwenye mikutano yao kila
uchao, atakabiliana na mtihani mzito wa kutekeleza ahadi hizo.
Uchunguzi
umebaini kuwa Rais ajaye kutoka miongoni mwa wagombea nane wanaoendelea
na kampeni hivi sasa, atakuwa na kazi ya kutekeleza ahadi zake binafsi
na zilizotolewa katika ilani za chama chake na pia atakuwa na kibarua
kizito cha kuangalia ni kwa namna gani atatekeleza ahadi zilizowahi
kutolewa na Rais Kikwete kwa nyakati tofauti kabla na baada ya chaguzi
zilizoiingiza serikali ya sasa madarakani.
Ahadi
tano kubwa kati ya zile zilizowahi kutolewa na serikali ya Rais Kikwete
ni pamoja na ununuzi wa meli katika maziwa ya Victoria, Tanganyika na
Nyasa; ununuzi wa bajaji maalum za kubebea wagonjwa katika hospitali;
kuimarishwa kwa mgodi wa makaa ya mawe Kiwira ili mwishowe usaidie
kuzalisha umeme; ujenzi wa reli mpya ya kati na pia kumalizwa tatizo la
maji katika maeneo kadhaa nchini ikiwamo katika Jimbo la Nzega mkoani
Tabora.
1. KIGOMA KUWA DUBAI YA AFRIKA
Serikali
ya Rais Kikwete iliahidi kuwa itaubadilisha Mkoa wa Kigoma na kuwa
Dubai ya Afrika kwa maana kuwa wa kibiashara kama ilivyo Dubai kwa
kujenga uwanja wa ndege, kupanua bandari na kuimarisha reli ili
kuhudumia nchi za maziwa makuu na za kusini mwa Afrika.
2. AFYA (BAJAJ KUBEBEA WAGONJWA)
Wakati
wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010, Rais Kikwete alitoa ahadi ya
kununua pikipiki za miguu mitatu (bajaj) 400 za wagonjwa kwa nchi nzima.
Rais Kikwete alitoa ahadi hiyo wakati akizungumza na wananchi wa mji wa Mkwajuni wilayani Chunya mkoa wa Mbeya.
Ahadi
hiyo itakuwa mtihani mzito kwa Rais ajaye ambaye atatakiwa kuitekeleza
kwa kuwa baadhi ya maeneo, hususani ya vijijini, bado yanaendelea
kukabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa magari ya kubebea wagonjwa ili
kuwawahisha kwenye hospitali kubwa. Waathirika wakubwa wa tatizo hili
huwa ni kina mama wajawazito, hivyo ni mtihani wa aina yake.
3. UJENZI WA 'FLY-OVERS'
Miongoni
mwa ahadi maarufu za serikali ya awamu ya nne ni ujenzi wa barabara za
juu (fly-overs) kwenye makutano ya barabara kubwa za jiji la Dar es
Salaam kama Mandela/Nyerere na Mandela/Morogoro, lengo likiwa ni
kupunguza makali ya foleni. Licha ya ahadi hii kurudiwa mara kadhaa,
bado haijatekelezwa hadi sasa.
Rais
ajaye atalazimika kufanya kazi ya ziada kuhakikisha kuwa inatekelezwa
ili kutimiza kiu ya maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam waliojawa
na matumaini waliyopewa na serikali yao ya sasa kwa kuamini kuwa hilo
likifanyika, adha wanayoipata ya kutumia muda mwingi wakiwa kwenye
foleni za magari itapungua kwa kiasi kikubwa.
4. UJENZI RELI YA KATI
Wakati
wa kampeni za uchaguzi mkuu 2010, Rais Kikwete akiwa wilayani Nzega,
mkoani Tabora, aliahidi kuwa serikali yake ingejenga reli mpya kutoka
Dar es Salaam hadi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Aidha,
akizungumza na wananchi wa wilaya ya Pangani, mkoani Tanga Septemba 10,
mwaka 2010, aliahidi pia kujenga reli kutoka Tanga kwenda Arusha hadi
Musoma.
Hata
hivyo, hadi kufikia sasa hakuna utekelezaji wa kuonekana kwa vitendo
katika kutimiza azma hiyo ya kuwa na reli mpya. Kwa sababu hiyo, Rais
ajaye na serikali yake watalazimika kuifanyia kazi ahadi hii ili
kuboresha sekta ya uchukuzi wa reli hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi.
5. AHADI YA MELI ZIWA VICTORIA, TANGANYIKA
Hii
ni ahadi mojawapo maarufu ambayo bado haijatekelezwa na kuna kila
dalili kuwa haitatekelezwa katika kipindi kilichobaki, hivyo kumpa
mtihani wa aina yake rais ajaye.
Katika
kampeni za uchaguzi mwaka 2010, Rais Kikwete alitoa ahadi ya kununua
meli kubwa kuliko ya Mv Bukoba iliyozama mwaka 1996. Alitoa ahadi hiyo
Agosti 24, mwaka 2010 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa
hadhara uliofanyika Bukoba Vijijini.
Aidha,
katika mkutano wake Bukoba Vijijini, Rais Kikwete aliahidi pia kujenga
uwanja wa ndege ili kuwarahisishia usafiri wananchi wa mkoa wa Kagera.
Akiwa
katika wilaya ya Nkasi, mkoa wa Rukwa Agosti 28, 2010, Rais Kikwete
aliahidi kuwa serikali yake itanunua meli mpya itakayokuwa inatoa huduma
katika Ziwa Tanganyika.
Aliahidi pia kununua meli mpya yenye uwezo wa kubeba tani 400 katika Ziwa Nyasa. Hadi sasa hilo halijafanyika.
Mrithi
wa Rais Kikwete katika serikali ijayo ya awamu ya tano, atalazimika
kuumiza kichwa na serikali yake ili kuhakikisha kuwa pamoja na mambo
mengine, ahadi hii pia inatimizwa.
AHADI NYINGINE
Ahadi
nyingine zilizowahi kutolewa na Rais Kikwete na ambazo utekelezaji wake
bado haujafanyika ni pamoja na ya kuwapelekea kivuko wakazi wa Buchosa
mkoani Mwanza. Akizungumza na wananchi wa jimbo hilo Agosti 23, 2010,
Rais Kikwete aliahidi kununua kivuko cha Maisome ili kuwaondolea adha
wananchi wanaotaka kuvuka kwenda maeneo mengine. Hilo hadi sasa
halijafanyika na hivyo rais ajaye atakuwa na kazi ya ziada kutekeleza.
Zipo
pia ahadi nyingine kadhaa zilizoibua matumaini mapya kwa Watanzania
lakini hadi sasa utekelezaji wake haujafanyika kwa asilimia mia moja.
Baadhi ya ahadi hizo ni ujenzi wa barabara za pembezoni (ring roads)
jijini Dar es Salaam, kukamilisha katiba mpya, kumaliza madai ya walimu,
uraia wa nchi mbili, kuufanya mji wa Tanga kuwa wa viwanda na pia
kushughulikia tatizo la ukosefu wa ajira.
MAFANIKIO SERIKALI YA JK
Licha
ya changamoto zilizopo, serikali ya awamu ya nne imefanikiwa katika
maeneo kadhaa yaliyotokana na ahadi zilizotolewa wakati wa chaguzi
zilizopita, hivyo kumpa kibarua cha ziada rais ajaye katika kuhakikisha
kuwa serikali yake inaongeza juhudi ili idumishe mafanikio hayo.
Baadhi
ya maeneo ya mafanikio ni ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, ujenzi wa
mtandao mkubwa wa barabara za lami na pia ujenzi wa madaraja makubwa
kama la Mto Malagarasi.
Mafanikio
mengine ni kuwapo kwa shule nyingi zaidi za sekondari nchini, kushamiri
kwa vyuo vikuu na kuongezeka kwa ufanisi katika sekta ya Bandari ni
miongoni mwa maeneo ya mafanikio, sawa na ilivyo katika harakati za
kuimarisha amani na utulivu katika visiwa vya Zanzibar kupitia Serikali
ya Umoja wa Kitaifa.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment