Kwa Jina la Mwenyezi
Mungu, Mwingi wa Rehma, Mwenye Kurehemu
UMOJA WA WANAWAZUONI WA
KIISLAMU TANZANIA
(HAY-ATUL ULAMAA)
TAMKO LA WANAWAZUONI
KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2015 NA HATMA YA AMANI YA NCHI YETU
Ndugu
wanahabari
na watanzania kwa ujumla,
Nchi
yetu inapita katika kipindi kigumu na hatari, kipindi cha uchaguzi mkuu wa
madiwani, wabunge, wawakilishi na Raisi mwaka 2015.
Katika
hali ya kawaida, mchakato wa uchaguzi
haupaswi kutia watu wasiwasi wala hofu ya uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi.
Lakini barani Afrika, harakati za uchaguzi zimekuwa chanzo kikubwa cha migogoro
ya kisiasa, uvunjifu wa amani na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokana na
uchu wa madaraka na kutokutendeka haki kwa wasimamizi wa uchaguzi.
Tumeshuhudia
matokeo ya chaguzi hizi za kidemokrasia yakileta maafa ya vita vya wenyewe kwa
wenyewe katika nchi za DR Congo, Ivory Coast, Kenya, Sierra Leone na hivi
karibuni Burundi.
Tumelazimika
kutoa tamko hili kutokana na hali inayojitokeza ambapo malalamiko ya wagombea
kutokutendewa haki, matumizi ya rushwa kama kishawishi cha kuchaguliwa na kauli
zinazoashiria hatari vimeanza kusikika wazi wazi.
Kauli
kama ile iliyotolewa na kiongozi mmoja wa chama tawala (CCM) na kunukuliwa na
vyombo vya habari likiwemo gazeti la Mwananchi la tarehe 23 Juni kwamba “CCM
itashinda tu hata kwa goli la mkono” ni kauli ya kukemewa kwani inaashiria
kujiandaa kwa wizi wa kura jambo ambalo ni hatari kwa amani na utulivu wa nchi
yetu.
Tunampongeza
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva, kwa kuikataa kauli
hiyo na kuahidi kwamba tume haitaruhusu jambo kama hilo kutokea.
Kauli
za kuashiria hatari kutoka upande wa upinzani ni pamoja na ile iliyonukuliwa na
vyombo vya habari kwamba kiongozi mmoja wa UKAWA akihutubia jijini Mwanza
aliliambia jeshi la polisi nchini kwamba “Hatutapiga
magoti na kuomba, kama ushindi utapatikana kwa njia halali hatuna tatizo,
lakini tukiona mambo yanakwenda ndivyo sivyo tunasema polisi mtatusamehe,
mabomu hayatatosha”.
Ndugu wanahabari na wananchi, katika
mazingira haya, sisi viongozi wa dini ya kiislamu tumetafakari kwa kina na
tunaiona hatari iliyo mbele yetu kama taifa. Tunaiona hatari hii kutokana na
mambo yafuatayo:-
i)
Chama tawala hivi sasa kinauguza
majeraha ya mpasuko wa ndani kwa ndani uliojitokeza kule Dodoma, mpasuko ambao
unaweza kuliathiri taifa.
ii)
Vyama vya upinzani vinaona ni
LAZIMA safari hii vitashinda na kuingia Ikulu.
iii)
Vituo vya polisi vinavamiwa,
polisi kuuawa na silaha kuibiwa na watu wasiojulikana.
iv)
Chama tawala kinajiandaa
kuhakikisha kinashinda hata kwa “goli la mkono”.
v)
Matumizi ya rushwa na vurugu katika
kampeni za uchaguzi kuanza kujitokeza.
vi)
Matukio yanayozidi kila uchao ya
wananchi kukosa ustahamilivu na kujichukulia hatua mikononi.
Katika mazingira haya, hekma
busara, na kuweka mbele maslahi ya taifa ni lazima vitawale katika kipindi
chote cha kampeni, uchaguzi na hata baada ya matokeo ya uchaguzi kutolewa
vinginevyo amani na utulivu ulioshamiri kwa miongo kadhaa nchini vinaweza
kutoweka mwaka huu.
Ndugu wanahabari na wananchi,
Ili
kuhakikisha uchaguzi huu unamalizika kwa amani na usalama, wadau wa mchakato
huu ambao ni vyama vyote vya siasa, tume ya taifa ya uchaguzi, Ofisi ya msajili
wa vyama vya siasa, vyombo vya ulinzi na usalama, serikali za mitaa, vyombo vya
habari, viongozi wa dini zote, asasi za kiraia na wananchi kwa ujumla TUNAPASWA
KUTANGULIZA MBELE MASLAHI YA TAIFA KULIKO KITU CHOCHOTE KILE NA KUTUMIA NJIA ZA
AMANI KUTATUA MIGOGORO ITAKAYOJITOKEZA.
Tumeitisha
mkutano huu na wanahabari ili tutoe tamko letu kwa wadau hawa mbali mbali kama
ifuatavyo huku tukiamini kwamba viongozi wa dini hawapaswi kusubiri mpaka mambo
yaharibike ndio watoe matamko;
TUME
YA TAIFA YA UCHAGUZI
Tume
ya taifa ya uchaguzi ndiyo mshika dau mkubwa na ni kama baruti inayoweza
kulipua bomu kwa sababu ndiyo inayosimamia zoezi zima la uchaguzi kuanzia uandikishaji
wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura, kugawa vifaa vya kupigia
kura, kuhesabu kura na kutoa matokeo.
Iwapo
tume ya taifa ya uchaguzi itafanya kazi yake kwa haki na uadilifu bila
upendeleo, kila upande ukaona haki siyo tu imetendeka bali imeonekana kutendeka
wazi wazi, vyama vya siasa na wananchi watakubali matokeo na hapo hakutakuwa na
sababu ya hofu ya uvunjifu wa amani.
Swali
linabaki, katika mazingira haya ya tume kuteuliwa na mmoja wa washindani katika
kinyang’anyiro hiki cha madaraka (serikali ya CCM) inaweza kusimamia uadilifu
kwa vyama vyote? Jibu ni kwamba tume inaweza kabisa kutenda haki lakini
inategemea dhamira za viongozi wa tume hiyo na kuweka kwao mbele maslahi ya
taifa badala ya kuegemea upande fulani.
SERIKALI
ZA MITAA
Sambamba
na hili la tume ya taifa ya uchaguzi ni kwa serikali za mitaa kuanzia chini
hadi wakurugenzi wa wilaya, miji na majiji. Huko ndiko vifaa kura hupelekwa, kura
kupigwa, kuhesabiwa na matokeo kutolewa kwa kila kata au jimbo kabla ya
kuwafikia watu wa tume ya taifa ya uchaguzi.
Uadilifu
mkubwa unahitajika sana kipindi hiki ili kulivusha salama taifa letu. Kumekuwa
na malalamiko ya kila mara kutoka kwa vyama vya upinzani kwamba baadhi ya
viongozi wa serikali za mitaa wanafanya kazi kama mawakala wa chama tawala badala
ya mawakala wa tume ya taifa ya uchaguzi.
Nasaha
zetu kwa tume ya taifa ya uchaguzi na serikali za mitaa, wekeni mbele maslahi
ya nchi yetu na vizazi vijavyo. Kutokutenda kwenu haki ndiyo sababu kubwa ya
kupelekea uvunjifu wa amani kwa sababu mtu aliyenyimwa haki kuizuia nafsi asikasirike
si rahisi. Kwa hiyo msiwatie majaribuni wengine kwa vitendo vyenu mkapendelea
upande wowote au mgombea yeyote yule katika uchaguzi.
VYAMA
VYA SIASA
Kwa
vyama vya siasa hasa CCM na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) nasaha zetu
kwao ni hizi zifuatazo.
Kwa
UKAWA; ni wazi kutokana na malalamiko ya uonevu katika chaguzi zilizopita na
hakukuwa na mabadiliko kwa tume ya taifa ya uchaguzi, mtakuwa mnaingia katika
uchaguzi huu huku tayari mioyo yenu ikiwa haina imani sana na tume ya taifa ya
uchaguzi.
Hili
ni jambo hatari sana kwa sababu kukosa kwenu imani na tume ya taifa ya uchaguzi
kunaweza kuwasukuma kuyakataa matokeo ya uchaguzi hata kama mkishindwa
kihalali. Nasaha zetu za dhati kwa UKAWA pamoja na maandalizi yenu makini na
imani ya kushinda mwaka huu ni busara pia kujiandaa kisaikolojia kukubali kushindwa
kwani hili linaweza kutokea.
Viongozi
wa UKAWA wamekuwa wakisema “CCM ijiandae kisaikolojia kuachia madaraka”. Lakini
pia ni muhimu zaidi kwa vyama vya upinzani kujiandaa kisaikolojia kukosa
madaraka. Kufanya hivyo kutasaidia kujiandaa kuyapokea matokeo yoyote yale hasa
iwapo tume ya taifa ya uchaguzi itatenda haki.
Kwa
Chama Tawala CCM
Tunajua
kupoteza madaraka ni jambo lisilowapendeza hata kidogo na bila shaka hampendi
hata kulifikiria. Lakini lolote linaweza kutokea kama alivyosema hivi karibuni
mwana CCM ndugu Salim Ahmed Salim kuwa “Chama chochote kinaweza kushinda”.
Katika hili CCM inafanana kabisa na mtoto aliyezoea kunyonya jinsi ambavyo
inakuwa vigumu kukubali kuachishwa ziwa.
Nasaha
zetu kwa CCM ni kujiandaa tu kisaikolojia kwa lolote linaloweza kutokea kwani
hiyo ndiyo siasa. Kujaribu kung’ang’ania madaraka haitakuwa jambo la maslahi
kwa CCM yenyewe wala taifa. Ikitokea kushindwa waamini kuwa inawezekana kuishi
nje ya madaraka kama ilivyotokea kwa UNIP ya Zambia, KANU ya Kenya na MCP ya Malawi.
Somo
pekee CCM inapaswa kujifunza kwa kushindwa vyama hivyo vikongwe ni wao kujiandaa
kimkakati jinsi ya kuwa chama cha upinzani mahiri. Kwa hali ilivyo, UKAWA haitarajiwi
kushinda majimbo mengi ya uchaguzi na madiwani kuliko CCM. Kwa hiyo inaweza tu
kuwa chama madhubuti cha upinzani kwa kuwa na bunge lenye idadi kubwa ya
wabunge wake na se
Ikitokea
UKAWA wakashinda, hali hii itawapa wakati mgumu sana kutawala nchi hata kama
wakishinda uraisi na kuunda serikali. Huwezi kutawala nchi ipasavyo ukiwa na
bunge linalodhibitiwa na chama cha upinzani tena kikongwe kama CCM. Hili ndilo
ambalo vyama vilivyoondolewa madarakani katika nchi jirani havikujiandaa nalo -jinsi
ya kuwa chama cha upinzani makini baada ya kutoka madarakani.
Kwa
vyama vyote vya siasa, tunawanasihi kudhibiti hamasa, jazba na hasira za
wanachama wao na malalamiko yoyote yale ya kutokutendewa haki katika uchaguzi
yapelekwe mahakamani badala ya kuhamasisha vurugu, fujo na uvunjifu wa amani.
VYOMBO
VYA ULINZI NA USALAMA
Kwa
vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, ninyi ndio washika dau wakubwa wa kulinda
amani yetu kwa sababu askari na silaha ziko mikononi mwenu. Kama vyombo vyetu vya
ulinzi na usalama vitajiepusha na ushabiki wa kisiasa kwa kupendelea upande
fulani tangu wakati wa kampeni hadi kutangazwa matokeo ya uchaguzi, bila shaka nchi
yetu itavuka salama.
Nasaha
zetu ni kwa vyombo hivi kubakia bila upande (neutral) kama viapo vyenu
vinavyowaelekeza kulinda Tanzania, watanzania na mali zao.
VIONGOZI
WA DINI ZOTE
Kwa
viongozi wa dini zote nchini, huu ndio wakati muhimu zaidi wa kuzidisha kuwachunga
na kuongoza waumini wetu kwa kuwajenga zaidi kiimani, kuwapa hekima na busara
na kuwahimiza kuwa wavumilivu na wasamehevu.
Tukumbuke
kuwa nje ya majumba ya ibada utakuta wana-CCM, UKAWA, ACT-wazalendo, TLP, TADEA
na kadhalika. Lakini wote hawa wakiingia katika majumba ya ibada anuani yao ni moja
tu-WAUMINI ima waislamu, wa
Viongozi
wa dini tusikubali uchaguzi huu kutawaliwa na upendeleo wowote ule kidini,
jinsia, kabila, rangi, hadhi wala tofauti za kiuchumi kwa sisi wenyewe
kushiriki kufanya hivyo au kuwavumilia wale wanaofanay hivyo. Kuruhusu hili ni
sawa na kuingia na moto katika chumba chenye petrol. Ni wazi nyumba yetu, taifa
letu litaungua.
OFISI
YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA
Msajili
wa vyama vya siasa anao wajibu mkubwa kuangalia mwenendo mzima wa vyama vya
siasa ili visivunje masharti ya kusajiliwa kwao kwa maslahi ya taifa.
Huko
nyuma, ofisi hii imekuwa ikilalamikiwa kwa kukipendelea chama tawala kama
inavyotuhumiwa tume ya taifa ya uchaguzi. Safari hii mazingira ni tete hivyo watendaji
wa Ofisi ya Msajili wa Vyama waweke maslahi ya taifa mbele.
VYOMBO
VYA HABARI
Vyombo
vya habari vinao mchango mkubwa kuhatarisha amani au kuilinda. Ushawishi wenu
kwa wananchi kwa kutengeneza mitazamo katika jamii (public opinion) kupitia
habari zenu utumike vizuri katika uchaguzi mwaka huu.
Vyombo
vya habari viripoti kuhusu mchakato huu kwa uadilifu pasina kupendelea wala
kupokea rushwa. Mkimjenga mgombea mbovu wananchi wakamchagua au mkishabikia
vitendo vinavyohatarisha amani mjue kuwa mtakuwa mmetumia tasnia yenu
kuhatarisha amani ya taifa letu na vizazi vijavyo vitawahukumu.
ASASI
ZA KIRAIA NA ZA KIDINI (AZAKI)
Asasi
za kiraia na za kidini ni wadau muhimu katika uchaguzi huu. Nasaha zetu kwao ni
kuhakikisha kwamba kunakuwa na haki sawa (fair play) katika uchaguzi na si
kuchochea mitazamo ya kuwagawa wananchi kwa misingi ya kibaguzi.
MAHAKAMA
ZA KISHERIA
Mahakama
ndiyo kimbilio la wale wote watakaohisi kuonewa. Tungependa kutoa wito kwa wagombea
wote, vyama vyote vya siasa na wananchi kwa ujumla kujenga tabia ya kupeleka
malalamiko yao mahakamani ili wapate ufumbuzi wa kisheria.
Kama
matokeo ya uchaguzi yanaweza kupingwa mahakamani, kwa nini chama au wananchi
wajichukulie hatua mikononi mwao? Wito wetu kwa mahakimu na majaji wajiandae
kutenda haki kuhusu kesi za uchaguzi.
Hili
ni muhimu sana kwa sababu wananchi wakikosa imani ya kupata haki zao mahakamani
bila shaka watashawishika kufanya fujo na vurugu ambazo zitapelekea uvunjifu wa
amani.
WANANCHI
WOTE
Mwisho
kabisa kwa wananchi wote, wanasiasa mbali na madai yao ya kutaka kuwatumikia
wananchi pia wanacho kitu
wanachokipigania. Kitu hicho ndicho kinachowapelekea kutoa au kupokea rushwa, kufanyiana
fitna, majungu, siasa za kuchafuana na hata wako tayari amani ya nchi yetu
iharibike iwapo watakikosa kitu hicho. Kitu hicho ni MADARAKA.
Lakini
wanasiasa wanahitaji kuungwa mkono na wananchi ili wayafikie malengo yao hayo.
Iwapo sisi wananchi tutakuwa wakomavu na kuweka mbele maslahi ya nchi yetu
kwanza kwa kuhakikisha chochote kinachoashiria au kuhatarisha amani hakipewi
nafasi, tutakuwa tumeliepusha taifa letu na uvunjifu wa amani.
Ndugu
wanahabari na watanzania,
Nchi
hii ni yetu sote. Kila mmoja wetu ajiulize maslahi gani mazito kwake; maslahi
ya mtu mmoja mmoja au maslahi yetu sote kama taifa? Ni kweli madaraka kuwa
mikononi mwa watu waadilifu ni jambo la muhimu, lakini tukumbuke nchi kuwa
katika hali ya amani na utulivu ni jambo muhimu zaidi.
Asanteni
sana.
No comments:
Post a Comment