PICHA ADIMU ZA TANU, JULIUS NYERERE NA WAZALENDO WALIOSAHAULIKA KATIKA HISTORIA YA KUDAI UHURU WA TANGANYIKA 1954 - 1961
Written By Mohamed Said on Saturday, May 2, 2015 | 11:25 AM
Abdulrahman Ali Msham sasa ni mtu mzima na ana umri wa miaka 65.
Wakati TANU inaasisiwa Dar es Salaam mwaka 1954 yeye alikuwa mtoto wa
miaka minne. Majuma machache yaliyopita alikisikia kipindi kilichorushwa
na Radio Kheri 104.10 FM kuhusu safari ya Mwalimu Nyerere UNO mwaka 1955. Kwa kauli yake mwenyewe anasema kipindi kile kilimrudisha nyuma sana akamkumbuka marehemu baba yake Ali Msham ambae alikuwa moja wa wazalendo waliokuwa mstari wa mbele katika kupambana na ukoloni. Abdulrahman Ali Msham
akawa na hamu kubwa ya kukutana na aliyekuwa akieleza safari ile ya
kihistoria. Alikuwa na hamu kwa kuwa na yeye alikuwa na machache
angependa kueleza nini baba yake Mzee Ali Msham alifanya katika TANU katika ile miaka ya 1950. Abdulrahman
alianza kwa kueleza kuwa baba yake alikuja Dar es Salaam kutoka Kilwa
katika miaka ya 1950 akiwa fundi seremala na likuwa akifanya shughuli
zake za kutengezeza samani Mtaa wa Kariakoo na Congo. TANU ilipoasisiwa
mwaka wa 1954 baba yake alijiunga na kuwa mwanachama kwa kukata kadi ya
TANU. Makazi yake yalikuwa Mtaa wa Jaribu Magomeni Mapipa ambako alikuwa
akiishi kwenye nyumba yake mwenyewe. Katika hamasa zile za kupambana na
ukoloni baba yake alitoa chumba kimoja katika nyumba yake akafungua
tawi la TANU na yeye mwenyewe akiwa mwenyekiti. Katika harakati zile za
kupambana na ukoloni alisikitiswa na hali ya ofisi ya Mwalimu Nyerere
pale New Street kwa kuwa hakuwa na samani za maana katika ile ofisi
yake. Baba yake alirejea kwenye kiwanda chake pale Mtaa wa Kariakoo na
Congo akatengeneza meza ya ofisi ya hadhi ya rais wa TANU pamoja na viti
kadhaa. Mzee Ali Msham alimwalika Mwalimu Nyerere kwenye tawi la TANU la Magomeni Mapipa ili makabidhi samani mpya kwa ajili ya ofisi yake. Mwalimu Nyerere alifika pale kwenye tawi la TANU na katika sherehe fupi Mwalimu Nyerere akakabidhiwa samani ile.
Kumaliza mazungumzo yetu Abdulrahman Msham alikabidhi picha za
baba yake za wakati ule wa kupigania uhuru. Picha hizo nami naziweka
hapa kwa ajili ya kuhifadhi na kuthamini mchango wa wazee wetu mashujaa
waliopigania uhuru wa Tanganyika lakini kwa bahati mbaya michango yao
haijathaminiwa.
Picha hiyo hapo chini inamwonyesha Mwalimu Nyerere akipokea samani hiyo iliyotengezewa na Mzee Ali Msham. Aliyesimama wa kwanza kulia ni Mzee Ali Msham mwenyekiti wa tawi la TANU Magomeni Mapipa wakati TANU inawaunganisha wananchi kupigania uhuru wa Tanganyika.
Ali Msham aliyekaa katikati katika moja ya mikutano ya ndani ya TANU aliyokuwa akifanya uani nyumbani kwake Mtaa wa Jaribu, Magomeni Mapipa |
Kushoto Wakwanza Ali Msham |
Ali Msham (kushoto aliyesimama) akiwahutubia wanachama wa TANU uani nyumbani kwake katika mkutano wa ndani
Tawi hili la TANU
Magomeni Mapipa lilikuwa na nguvu na viongozi mashuhuri wa TANU walifika
mara nyingi kuzungumza na wanachama na viongozi wao. Picha ya chini
wanaonekana Zuberi Mtemvu (aliyeshika tama) aliyekuwa Katibu Mwenezi wa TANU akiwa na Sheikh Suleiman Takadir Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU na kushoto yake Mzee John Rupia Makamu wa Rais wa TANU wakiwa katika moja ya hafla za TANU katika tawi hilo. Rais wa TANU Mwalimu Nyerere haonekani amezibwa na John Rupia lakini mlinzi wake katika vijana wa BANTU Group anaoenakana amesimamakaribu yake amevaa lubega.
|
Kushoto: John Rupia, Julius Nyerere, Zuberi Mtemvu Waliosimama nyuma yao ni BANTU Group Vijana Walinzi wa Viongozi wa TANU |
Ofisi ya TANU
Mtaa wa Jaribu Magomeni Mapipa kama ilivyokuwa ikionekana katika miaka
ya 1950 ikiwa imezungikwa na wanachama wake. |
No comments:
Post a Comment