Kenya, Nigeria zagoma kuiazima Tanzania BVR
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Posted Jumanne,Marchi17 2015 saa 9:16 AM
Posted Jumanne,Marchi17 2015 saa 9:16 AM
Kwa ufupi
Uamuzi
wa NEC wa kutaka kuazima vifaa hivyo ni kutokana na mchakato wa
uandikishaji kukwama kwenda kama ulivyopangwa kutokana na BVR 250
zilizopo kutokuwa na uwezo wa kuandikisha wapiga kura wote nchini.
Dar
es Salaam.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian
Lubuva amesema ofisi yake ilijaribu kuazima vifaa vya kielektroniki vya
Biometric Voters Registration (BVR) katika nchi ya Kenya na Nigeria kwa
ajili ya kuandikisha wapiga kura, lakini nchi hizo zilikataa.Uamuzi wa
NEC wa kutaka kuazima vifaa hivyo ni kutokana na mchakato wa
uandikishaji kukwama kwenda kama ulivyopangwa kutokana na BVR 250
zilizopo kutokuwa na uwezo wa kuandikisha wapiga kura wote nchini.
Kitendo
hicho kinaweza kusababisha Kura ya Maoni iliyopangwa kufanyika Aprili
30, 2015 mwaka huu kushindikana kwani mpaka sasa ni mkoa wa Njombe pekee ambako
uandikishaji unaendelea kufanyika na unatarajiwa kumalizika Aprili 12, 2015.
“Tulitaka
kuazima Kenya lakini wakasema wanavitumia hata kama wamemaliza uchaguzi
lakini mchakato wao wa uandikishaji unaendelea kutokana na kwamba watu
wao wanapofikisha umri wa kuandikishwa wanawaingiza katika daftari lao,”
alisema Jaji Lubuva na kuongeza:
“Tulikwenda Nigeria nako walitueleza wanazitumia. Kuazimana siyo jambo geni kwetu na huu ndiyo ukweli wake.”
Kuhusu
mchakato wa uandikishaji mkoani Njombe alikoweka kambi alisema:
“Uandikishaji huku unakwenda vizuri licha ya kauli mbalimbali na mimi
nimekuwa nikiwahamasisha kujitokeza na tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa.”
Katika
uchaguzi wa Ghana uliofanyika mwaka 2013 mfumo wa BVR ulitumika na
kuonyesha mafanikio makubwa. Hata hivyo, Malawi iliukataa mfumo huo
katika uchaguzi wa mwaka 2014 baada ya kuonyesha udhaifu mkubwa katika
uchaguzi wa mwaka 2005.
Katika
mahojiano maalumu na viongozi, wahariri na waandishi wa habari wa
Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) inayochapisha magazeti ya
Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen makao makuu ya kampuni hiyo Tabata
Relini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
alisema, NEC ilianza mchakato huo bila vifaa ikitegemea kuazima.
“Tulipokwenda
Kenya na TCD (Kituo cha Demokrasia Tanzania) kuangalia walivyofanikisha
mchakato huo wakatueleza kuwa NEC walikuja hapa kuazima BVR za
kuandikisha... tulikuwa na mawaziri pale yaani ilikuwa aibu na
walitueleza kama hadi Novemba hamjanunua hamuwezi kuandikisha. Walisema
walikuwa na BVR 15,000 Kenya na waliandikisha wapiga kura milioni 14 kwa
zaidi ya siku 45 hadi 60, sisi tuna matatizo.
“Wanatupa
wasiwasi mkubwa, ikiwa lengo ni kuandikisha wapiga kura wote
haiwezekani tukawa na kura ya maoni Aprili 30, 2015 lakini ukiwa unahitaji
lazima uandikishe kwanza halafu ufanyike uhakiki wake, lakini muda huo
hautoshi?
Kauli hiyo
ya Profesa Lipumba kuhusu kusimamishwa kwa kura ya maoni pia ilitolewa
Februari 12, 2015 na viongozi wa vyama 22 vya siasa walipokutana na NEC
kujadili mchakato huo wa uandikishaji kwa kutumia BVR.
Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema: “Mchakato huu ni
muhimu na kama hautafanyika vizuri tutaichafua nchi yetu. Wadau
washirikishwe na waridhike kwani kusipokuwa na uwazi kutaleta shida huko
mbele.”
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe alisema: “Ilitakiwa kutuhusisha katika hili
mwanzo hadi mwisho. NEC wanatuonyesha hardware (vifaa vya kompyuta)
badala ya software (programu
ya kompyuta) zinavyofanya kazi ambayo tuna haja ya kuifahamu. Nani
anatuuzia hizo hardware na nani anatuuzia software hizo?”
Profesa
Lipumba alisema: “Serikali inatakiwa kujikita zaidi katika uandikishaji
wapiga kura lakini Serikali haina fedha, bajeti ya Sh144 bilioni haipo
sasa itakuwaje tunaingia katika kura ya maoni?
Mchakato wa Katiba
Kuhusu
mchakato wa Taifa kupata Katiba Mpya chini ya utawala wa Rais Jakaya
Kikwete, Profesa Lipumba alisema hakuna matumaini hayo na kinachofanyika
ni kutaka kuhalalisha utaratibu ambao haukuwa na uhalali kutoka kwa
wananchi.
Alisema
Februari mwaka 2013 wakati Rais Kikwete akizindua Vitambulisho vya
Taifa, alisema vitambulisho hivyo vingeweza kutumika pia katika kupiga
kura lakini hakuna utaratibu wowote uliotumika kuhakikisha Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (Nida) na NEC wanashirikiana.
Profesa
Lipumba alisema baadaye Jaji Lubuva alinukuliwa akisema kazi ya
uandikishaji itafanywa na tume yake na si mtu yeyote kwani haiwahusu.
Alisema
bajeti ya mchakato huo ni Sh297 bilioni lakini alipotizama katika kasma
ya tume kulikuwa na Sh7.01 bilioni, fedha za maendeleo na fedha za tume
hazikuonekana.
“Ukienda
kuchambua fedha ziko wapi huzioni, mimi nikauliza mbona bajeti ni kubwa
lakini haijulikani iko wapi? Hata ukifanya ukaguzi unatakiwa kujua
fedha hizo, katika maombi yake Tume iliomba Sh144 bilioni kwa ajili ya
Kura ya Maoni lakini nayo haionekani katika vitabu vya Serikali sasa
unajiuliza mchakato huo utakwendaje na fedha zimekwenda wapi?” alihoji
na kuongeza:
“Suala
la muda halitekelezeki, awali tume ilisema uandikishaji ungeanza
Septemba, 2014, lakini ilishindwa, Desemba, 2014 ikafanya majaribio ya
uandikishaji na katika Jimbo la Kawe wameandikisha wapiga kura kama
15,000 na ushee katika maeneo ya Bunju na Mbweni.
Walisema
wamevuka malengo lakini ukienda katika takwimu za Sensa za mwaka 2012
za Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) haziendani. Bunju wapo 51,000 lakini
hawa wameandikisha 15,000 wanasema wamevuka lengo sasa hapa kuna ukweli
wowote?”
“Makambako
walisema wataandikisha wapiga kura kama 31,000 lakini kwa Sensa ya mwaka
2012 ina wapiga kura zaidi ya 53,000 sasa utasemaje umevuka lengo na
Jaji Lubuva alishatamka kwamba daftari la mwaka 2010 limechakaa hivyo
wakisema tutumie daftari hilo haiwezekani.”
No comments:
Post a Comment