Sunday, February 8, 2009

SOMO LA AFYA BORA NA. 5

Kutoka kwa Dr. Wilbert Bunini Manyilizu, wa Chuo Kikuu Mzumbe, Tanzania,
Jumapili, Februari 8, 2009.

Article 5

DALILI ZINAZOASHIRIA UPUNGUFU WA MAJI MWILINI, JAPO HUJISIKII MGONJWA

Midomo, ngozi kupauka na kutoa vumbi, mikwaruzo myeupe hubaki kwenye ngozi ikikunwa, kiu, mkojo kupungua (kuwa kidogo), kukojoa mkojo wa njano, kinyesi kigumu. Kwa mtu anayeharisha au kutapika, macho yaweza kuingia ndani, ngozi kuonekana nyeupe kama haina damu, ngozi husinyaa kama ya kikongwe, mapigo ya moyo kuenda mbio, kulegea na kuishiwa nguvu, presha kushuka na hata kuzimia na kufa.

Maumivu ya kichwa ni sehemu ya muhimu inayotumiwa kukumbusha upungufu wa maji mwilini. Maumivu hayawezi kuondoka kama shida haijaondolewa, hivyo wengine wamedhani wana ugonjwa wa kudumu na wamehangaika kutafuta tiba na kupata nafuu ya muda mfupi na shida huendelea kuwepo. Wengi wamekata tamaa, wakadhani hawawezi kupona. Uzoefu wa madaktari ambao wamejifunza umuhimu wa maji katika tiba, umesaidia wengi. Baadhi ya madaktari hawa wameonekana wagunduzi kumbe ni sayansi rahisi waliyojifunza awali. Madaktari wengine wameiacha kuitia katika matumizi, badala yake wanazingatia madawa tu ya viwandani. Madaktari wengi hawaulizi wateja wao katika chumba cha uchunguzi kama wanatumia maji ya kutosha katika maisha ya kila siku. Isitoshe madaktari wenyewe hawana uzoefu wa kunywa maji ya kutosha mpaka pale wanaposukumwa na kiu. Tena wanapokuwa na maumivu hukimbilia tiba zingine wakisahau fiziolojia waliyoijua sana. Hii itawakumbusha wapendwa madaktari wenzangu kutumia wanachokijua tayari, wawasaidie wagonjwa wetu na kujisaidia wao wenyewe. Itawapatia wagonjwa wetu nafuu ya kudumu pale wanapotumia dawa za kawaida wakitumia na maji kwa wingi. Swali linakuja, maji kwa wingi ni kiasi gani? Hili litajadiliwa katika aya zifuatazo. Lakini cha msingi ni kwamba, dawa zingine zitumike tu pale inapobainika kuwa shida siyo kwa sababu ya upungufu wa kunywa maji. Kwa sababu si salama kuuzoesha mwili kutumia madawa hata pasipokuwa na ulazima. Kwani madawa yote yana viwango tofauti vya kusababisha madhara yasiyotazamiwa, hata panadol iliyozoeleka sana kwa kutuliza maumivu ina madhara kwa afya. Maji yakinywewa kwa mdomo hayana madhara, yanayozidi hutolewa kwa njia za mkojo, jasho na hewa. Wanasayansi wengi wameonesha uzoefu kuwa kwa mtu wa umbo la kawaida (kilo 60 hadi 70) anayesumbuliwa na maumivu ya kichwa akinywa bilauri moja ya maji kila baada ya dakika kumi kwa muda wa saa moja nzima, maumivu hutoweka. Maumivu ya kichwa yasipotoweka basi mtu huyu aende kwa tabibu kwa uchunguzi.

Kiasi gani cha maji kinatosha?

Kwa mtu wa umbo la wastani angalau bilauri nane kwa siku, vinginevyo hutegemea ukubwa wa umbo lake, joto la mazingira aliyopo, aina ya kazi anazofanya, kadri mtu anavyofanya kazi zaidi ndivyo anavyotakiwa kunywa zaidi. Anayechimba mtaro barabarani ni dhahiri atahitaji maji mengi kuliko anayefanya kazi kwenye chumba chenye kiyoyozi.

Wataalamu wengine hupendelea kunywa lita moja kwa kila kilo 30 za uzito wa mtu. Mwandishi wa kitabu hiki anapendelea mbinu rahisi isiyohitaji kutafuta mizani kujua uzito, bali kunywa maji mpaka mnywaji ahakikishe anapata mkojo unaofanana na rangi ya maji safi ya bomba. Maji ya kawaida yafaa sana kuliko ya baridi, sababu baridi kali inayotofautiana na joto la mwili (nyuzi 37) huushtua mwili na kufisha ganzi neva za fahamu. Na kufanya mtu asinywe maji ya kutosha kwani huridhika mapema kana kwamba kiu yake imetoshelezwa kwa kiasi kidogo tu cha maji ya baridi. Joto la maji ya kunywa na lile la mwili wa mnywaji maji halitakiwi kutofautiana kwa kiasi kikubwa. Fikiria mfano rahisi wa bilauri ya maji ya moto inapomwagiwa barafu. Fanya jaribio hili uone kitakachotokea. Ndivyo inavyokuwa kwa mtu mwenye kiu kali anayetoka juani, anapokunywa maji ya baridi sana mwili unavyoshtuliwa hata wakati mwingine kusababisha maumivu ya koo. Kazi zingine za maji ni pamoja na kutumika kama tiba ya magonjwa mbalimbali ndani na nje ya mwili. Tatizo la kunuka harufu mbaya kinywani laweza kuondoka msomaji anapojenga mazoea ya kunywa maji ya kutosha kurahisisha mzunguko wa mate kinywani. Ni muhimu pia kujua kuwa kunuka mdomo kwaweza kutibiwa kwa kunywa maji mengi na kutunza kinywa kwa usafi.

No comments:

Post a Comment