Friday, May 7, 2010

DHIHAKA YA MHIMILI WA UTAWALA KWA MAHAKAMA TANZANIA

IMENAKILIWA HUMU LEO HII TAREHE 7 Mei, 2010, na Mwatawala, Zainab M.

MAZOWEYA YA MHIMILI WA UTAWALA TANZANIA KUKEJELI, KUDHARAU, KUBEZA NA KUDHIHAKI MHIMILI WA UTOAJI HAKI (MAHAKAMA)

1. Katika Kitabu kiitwacho LAW AND JUSTICE IN TANZANIA: QUARTER OF A CENTURY OF THE COURT OF APPEAL, kilichohaririwa na Peter, C.M. na Kijo-Bisimba, H. (2007), aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa [CAT] na ambaye sasa ndiye Jaji Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Augustino Ramadhani aliandika makala iitwayo “Twenty Five Years of the Court of Appeal of Tanzania and the Establishment of the East African Court of Justice” [Miaka 25 ya Mahakama ya Rufaa Tanzania na Uanzishwaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki] ianziayo ukurasa 223 wa kitabu hicho.

Katika Ukurasa wa 227 ametoa maeneo matatu ya Maagizo ambayo Mhimili wa Utawala (The Executive) nchini Tanzania umeshindwa kutekeleza kutokana na tabia yake ya kudharau, kubeza, na kudhihaki Mhimili wa Utoaji haki kama ifuatavyo:

1. Malipo ya Mafao kwa Majaji Waondolewao Madarakani

Katika hili Mahakama ya Rufaa ilishauri kuwepo na Orodha ya Makosa yanayomnyima Mafao Jaji atiwaye hatiani au Chombo kinachotoa hukumu hiyo (tribunal) kitamke endapo Jaji Mkosaji anastahili au hastahili malipo ya mafao (terminal benefits) katika kesi ya MOSES J. MWAKIBETE V THE PRINCIPAL SECRETARY (Estab.) AND THE ATTORNEY GENERAL, Court of Appeal of Tanzania at Arusha, Civil Appeal No. 27 ya 1992 (haikuripotiwa).

Hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na Serikali hadi wakati wa kuchapishwa kitabu hicho mwaka 2007 toka mwaka 1992.

2. Malipo ya Mawakili wa Kujitegemea Wateteapo Wahalifu Kwa Mujibu wa Sheria

Mahakama ya Rufaa ilipendekeza mwaka 1991 kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali [AG] (Andrew Change – Bwana Vijisenti) kupitia upya malipo haya yaliyolipwa kati ya Tshs.120/= na Tshs.500/=; wakati huo ikilinganishwa na kiasi cha chini ya nusu dola ya Kimarekani ($).

AG hakuwahi kutekeleza agizo hili hadi miaka mitano (5) baadaye wakati CAT ilipoamua yenyewe kuongeza kiasi hicho hadi kufikia Tshs.100,000/= kwa kutumia fursa iliyojitokeza katika kesi ya THE ATTORNEY GENERAL V N.I.N. MUNUO NG’UNI [1998] TLR 464.

3. Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984

CAT ilipendekeza masuala ya kutafsiri Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na masuala mengine nyeti ya Kikatiba yasiyofikishwa CAT kwa uamuzi yatazamwe na yafikiriwe kubadilishwa katika kesi ya SEIF SHARIFF HAMAD V SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR (SMZ) [1998] TLR 48.

Jambo hili halikufanyiwa kazi na miaka mitano (5) baadaye CAT ikalikumbusha pendekezo lake kwamba Mamlaka zinazohusika pande mbili za Muungano zichukue hatua za makusudi kuoanisha vipengele viletavyo migongano ndani ya Katiba zote mbili; ile ya Zanzibar ya mwaka 1984 na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977. HAYA HAYAJATEKELEZWA.
[mwisho wa sehemu iliyoandikwa na Jaji Mkuu)

4. MTAFARUKU ULIOPO SASA WA MGOMBEA BINAFSI
Ijumaa, Februari 12, 2010, Bw. Philip Marmo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, alisema kuwa katika uchaguzi mkuu ujao suala la kuwepo Mgombea binafsi kama ilivyoamuliwa na Mahakama Kuu tarehe 5 Mei, 2006 na kufafanuliwa na CAT haliwezi kupata nafasi kwa kuwa muda wa maandalizi hautoshi.

Kauli hiyo ililenga kukejeli, kupinga, kudharau, kuasi na kubeza tamko la Mahakama ya Rufaa la Feruari 10, 2010 lililobariki amri iliyotolewa na Mahakama Kuu tarehe 5 Mei, 2006.